Monday, January 28, 2008

KWA NINI ULIENDA SHULE? KWA NINI UNASOMA?


Huu ni ushauri wangu, siuzi, usiogope kuuchukua kwa kudhani utagharamia kitu!



Niseme mapema, mimi si mwandishi mahiri wa makala, kwa hiyo usitarajie mtiririko mzuri kama ule wa waandishi mahiri nchini, lakini zingatia zaidi ujumbe.

Naandika makala hii kwa uchungu utokao kutoka kilindi cha moyo wangu. Naandika pia kwa majonzi makubwa nikiwa njia panda nisijue hatima ya jambo Fulani nitakalokueleza muda si mrefu ujao katika makala hii.

Nina swali ndugu zangu, swali langu ni hili; kwa nini tunaenda shule? Sijauliza kwa nini tulisoma? Hapana nimeuliza “kwa nini tunasoma” Swali hili haliwahusu wale ambao tayari wako maofisini, wanafanya biashara, mawaziri na wabunge. Swali langu ni kwa wale tu ambao bado wako mashuleni na hasa vyuoni, hususani vyuo vya elimu ya juu au vyuo vikuu. Hawa ndio walengwa wangu hapa.

Nimewahi kukaa na wanafunzi, ninapokutana nao kwenye daladala, shuleni, mitaani na hata wale ambao huja kunitembelea na kuwauliza swali hili. Wengi wao wamenijibu jibu ambalo hata wewe ambaye unasoma makala hii pengine ungelitabiri na kupatia au kunijibu. Wameniambia kwamba wanasoma ili waje kuwa na maisha mazuri hapo baadae, wapate kazi nzuri, basi, wakishapata kazi nzuri yatosha.

Na si ajabu watakwambia kwamba wanasoma ili wapate kazi Benki kuu, T.R.A, Ikulu, au kwenye wizara mbalimbali ambako wanafunzi hutiana moyo kwamba kuna kazi na maslahi mazuri. Wanasahau kwamba tuna wasomi wengi mitaani waliochoka kimaisha, wanaosota kwa kukosa ajira, lakini hawasumbui akili zao kujiuliza ni nani anasababisha ajira zisiwepo. Je katika kusababisha uhaba huo wa ajira, hakuna wanaoitwa wasomi? Tunajua kuwa serikali haina ajira zote, lakini ina uwezo wa kuandaa mazingira ya uwepo wa ajira kwa wananchi wake, nini kimetokea? Na kasababisha? Je, wasomi hawahusiki humo?

Wachache huwaza kusoma ili wawe walimu wa sekondari na msingi, hilo huliweka mwisho tena ikitokea wakafeli. Kaa na mtanzania mwenzako, muulize kwa nini anasoma? Sikiliza jibu lake, litafakari jibu hilo kisha pambanua na kuona usahihi wake.

Wengine wapo tu, wanasoma ili waje kuwa wazungumzaji wazuri wa Kiingereza (lugha ya kikoloni) kwao ni ufahari kuzungumza kiingereza kuliko Kiswahili, usipojua kiingereza unaonekana mshamba, unaonekana huna akili timamu, waulize wanafunzi wa vyuo vikuu watakwambia hili. Ni watumwa wa kingeereza, wanasahau kwamba kingereza ni lugha kama kinyakyusa, kingoni, kisukuma, kichaga na zinginezo. Wanasahau au hawajui kwamba kutokujua kingereza ni haki ya mtanzania mzawa wa hapa, si dhambi maana hawakuzaliwa nayo!

Wengine wanasoma ili nyumba zao baadae zipambwe na vyeti vya shahada na stashahada ukutani, hilo tu basi! Wanasoma ili na wao watembee vifua mbele wakiwa wanaitwa wasomi mitaani, waitwe mainjinia wakati mitaa yao inatiririka maji machafu kama ile ya Sinza kwa kukosa mitaro ambayo tulitegemea wasomi hao watumie taaaluma yao kutatua tatizo hilo. Wanataka waitwe wasomi mitaani wakati baba zao, mama zao, kaka na dada zao vijijini wanadhulumiwa mazao yao kwa kulazimishwa kuuza mazao kwa bei isiyowakwamua kiuchumi.

Wanataka waitwe wasomi wana sheria wakati wameshindwa kabisa kutetea mahabusu ambao pengine kesi zao zinacheleweshwa bila sababu za msingi, wameshindwa kutatua tatizo hili sugu. Wanataka waitwe wana habari wasomi huku wakiwa wameigeuzia kisogo jamii yao kwa kukubali kupokea pesa ya bia (rushwa) kuliko kuandika habari za kufichua ufisadi nchini, wanakubali kuisaliti jamii ya wasio na sauti kwa kuhongwa ili kuwaandika vizuri wanasiasa wanaowanyonya mamilioni ya watanzania masikini kwa uroho, ubadhirifu na dhuluma! NK

Hapa najiuliza, nini tafsiri ya msomi? Msomi ni nani? Je, tumwite mtu msomi kwa sababu kahitimu miaka mitatu ya masomo yake Chuo Kikuu cha Tumaini, Mlimani, Mzumbe au Mtakatifu Augustine wakati hana mchango wowote kwa jamii yake zaidi ya kuisaliti? Kwa hali ilivyo sasa, kwa wasomi kushindwa kutumia taaluma zao kututatulia matatizo katika nchi hii, jamii inawalaani, hivyo kuitwa msomi ni kama laana au kujilaani. Kwamba ni laana kuitwa msomi katika nchi hii.

Sasa kwako wewe uliyeko shuleni, kwa nini unasoma? Kwa nini umeamua kusomea fani unayosomea? Je, ni kwa vile wazazi au rafiki zako wamekushinikiza? Je, ni kwa sababu unataka kujipatia viza kwenda kuishi London, New York, Amsterdam? Kisha iweje? Je, unasoma ili upate kazi nzuri? Fikiria mtu kama Daud Balali, aliyekuwa gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (B.K.T) si alikuwa msomi? Kazi yake si ilikuwa nzuri? Amelifanyia nini Taifa? Tafakari!

Sikiliza, nataka nikushawishi, nataka nikugeuze fikra zako leo, kama ulikuwa unasoma kwa ajili ya mambo hayo hapo juu badilika. Tunataka mapinduzi. Hii ni kwa ajili yako wewe uliyeko shule, hata wewe utakaye hitimu hivi karibuni, hujachelewa, bado una muda wa kubadilika.

Nataka nikwambie kwamba kuanzia sasa, kama ulikuwa hujui basi ANZA KUSOMA KWA AJILI YA TANZANIA. SOMA KWA AJILI YA TAIFA LAKO.

Kama vijana wa Tanzania wanasoma kwa ajili tu ya kupata pesa za kula wao na familia zao basi niko njia panda. Maana hii ni ubinafsi na hatima ya Taifa letu iko mashakani. Unaweza ukadhani nakurudisha kwenye zama za ujamaa, lakini ukweli ndio huo!

Sikiliza kijana, Taifa linakusubiri, watanzania wanakusubiri! Si kwamba usome ili uje uwamwagie mapesa, lahasha, wanataka wasomi wa kizazi kipya, wasomi waadilifu, wenye moyo wa uzalendo, si wale wanaolitumikia Taifa huku wakiwa na urai wa nchi mbili, ili kwamba baada ya kuwaibia watanzania waukane uraia wa Tanzania. Taifa linakungoja, soma ili uje ulikwamue kutoka katika matope lilipokwamishwa na wasomi wabinafsi, waliosoma ili wapate kazi/ajira nzuri.

Fikiria kuhusu aliyekuwa waziri wa Fedha wakati wa awamu ya tatu, Basil
Mramba, aliyetangaza bila huruma, bila aibu kwamba ni bora watanzania wale nyasi lakini ndege ya rais inunuliwe, je, hayakuwa matusi kwa watanzania? Je, Mramba si msomi? Usomi huu una tija kwa watanzania? ‘sitaki kuamini kwamba aliyasema haya akiwa amedhamiria kuwatukana watanzania’

Fikiria kuhusu wabunge wasomi walioko kwenye bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao huelewa fika kwamba wanaposimama na kutetea itikadi za vyama vyao kuliko maslahi ya Taifa katika kufikia maamuzi mazito ya mustakabali wa Taifa hili ni kuturudisha nyuma kimaendeleo. Watanzania (hata kama hawasemi) mioyo yao ina shauku ya kuwa na wasomi watakaoweka mbele utaifa kuliko u-CCM, u-CHADEMA, u-CUF, u-TLP nakadhalika! Hii ndio shauku ya watanzania! Ni wewe uliyeko shule ukikubali kubadilika na kuweka utaifa mbele.

Taifa letu ni sawa na kwamba limeuzwa, nani atalikomboa? Kila kitu wamepewa matajiri wa nje, utamaduni wetu umeuzwa, uadilifu, utaifa, mashirika, viwanda, madini, pengine bado sisi tu kuuzwa. Ni wewe uliyeko shule usome ili kuwamilikisha uhuru halisi watanzania. Inawezekana kama utaamua. Ukiwa mbinafsi mwendo ni uleule, sote kulitumbukiza taifa hili shimoni, na maendeleo tutayasikia kutoka uropa na marekani.

Soma kijana, soma mtanzania, mama, baba, dada, kaka zako wanakusubiri uje utumie taaluma yako ya sheria kuja kusababisha sheria za kibabe/onevu kufutwa, uje utumie taaluma hiyo hiyo kufuta sheria mbovu za madini zinazowawezesha mabepari kufaidi urithi wetu wa madini tuliokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Soma ili uje utumie taaluma yako ya udaktari kuwahudumia watanzania kwa moyo safi, wa huruma na uadilifu, maslahi yatakuja tu! Soma ili uje utumie taaluma yako kulinusuru Taifa hili. Yaliwezekana kwa wazungu yatawezekana kwetu pia, tuamue tu.

Tusome kwa ajili ya Taifa, weka uzalendo mbele. Hata kama unapanga kuwa mwasiasa baada ya kuhitimu, waza kuwa mwanasiasa kwa ajili ya Tanzania na sio CCM au chama kingine chochote, vyama hivyo viwe njia tu lakini si hatima, ndio maana naunga mkono harakati za kuruhusu wagombea binafsi wa ngazi mbalimbali za uongozi katika nchi hii.

Ukiniuliza mbona viongozi wetu wa leo ni wasomi mahiri lakini nchi bado iko nyuma, nitakuambia kwa urahisi tu kwamba walisoma ili wapate kazi nzuri, si kwa ajili ya taifa lao, kama sivyo niambie nini kimetokea? Nini kimewakwamisha? Hapana shaka kwamba tuna viongozi wabinafsi japo ni wasomi. Fikiria tena kuhusu watuhumiwa wa ufisadi BOT, walio tajwa na ambao bado hawajatajwa bado, wengi ni wasomi wazuri walioaminiwa kututumikia. Lakini walichotufanyia wewe na mimi tumekiona!

Nina mengi ya kusema, nikipata nafasi tena nitayasema.
Kwa mara nyingine tena, nataka nikwambie kwamba kuanzia sasa, kama ulikuwa hujui basi
ANZA KUSOMA KWA AJILI YA TANZANIA, SOMA KWA AJILI YA TAIFA LAKO! Kila la heri!

0713 550 778
Barua pepe: ilovejesustz@yahoo.com