Monday, March 19, 2007

Hata tusipokuwa wanasiasa tunaweza kuleta mabadiliko


Na Daniel R. Gingo

Siku za nyuma kidogo niliandika makala ilikuwa na kichwa kisemacho, “ninyi nanyi mtatupa lini nafasi”? Niliwahoji wanasiasa ambao wamekuwa mstari wa mbele majukwaani kukilaani chama cha mapinduzi, eti kwa kung’ang’ania madaraka. Nilihoji uhaliali wao wa kuinyooshea mikono CCM hali wao nao hawataki kuachia wengine kuongoza vyama hivyo. Je ulisoma makala ile?

Kwa wale ambao hawakubahatika kusoma makala hiyo, hiki ni kipande tu cha yale niliyoandika katika makala ile.

Unajua tumekuwa kama wajinga Fulani au watu tuliolishwa dawa ya kutupumbaza hasa nyakati za uchaguzi. Wakati wa uchaguzi vijana wamekuwa nyenzo muhimu sana kwa wagombea, wao wamekuwa wahamasishaji wazuri huku wakiachwa hohe hahe, wametumikishwa bure huku malipo yakiwa ni chupa za maji ya uhai na shilingi miatanomiatano. Kama yule mwanaharakati alivyosema, wakati mwingine huwa wanasukuma magari ya wagombea wakati mafuta yamejaa tele na wala hayana hitilafu yoyote ya kiufundi.

Hizi si hadithi hata kidogo, mwak 1995 wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyma vingi Tanzania, nilishuhudia vijana wa kijiji cha Kandete kule Rungwe Mbeya wakilisukuma gari la Agustine Mrema baada ya mkutano wa Kampeni. Toka alipoanza harakati za kutaka kuingia Ikulu Mrema hajwahi na hana dalili za kuingia huko. Lakini hata sasa hajakata tama bado.

Ni huyu huyu Mrema alikuwa chama cha NCCR-Mageuzi, alipewa huko cheo na kuwa Mwenyekiti, baadae unakumbuka alihamia TLP-Mageuzi, oooh! Samahani hii haiitwi TLP mageuzi, ni TLP tu hivyohivyo. Huko Mrema kafnya mapinduzi ya kufa mtu, akasababisha waasisi wa chama hicho wakiwemo wakina Thomas Ngawaiya wakihame chama hicho. Usisahau kuwa aliwahi pia kukosana na mwasisi wa NCCR-Mageuzi bwana Mabere Marando. Sasa Bwana Mrema ndiye bosi wa TLP japo mitaani kuna habari kuwa kuna watu bado hapatani nao ndani ya chama.

Sasa angalia Mrema anavyotukuna wanachi akiwa jukwaani. Anasema CCM imepitwa na wakati, imekaa muda mrefu madarakani, ni ving’ang’anizi, kwa kusema hivyo anaomba wananchi waiondoe madarakani CCM kwa sababu tu pamoja na kukaa miaka mingi wakishikiria dola bado hawajaleta maendeleo katika nchi. Kisha rudi kwenye vyama alivyopita Mrema uone ni maendeleo gani ameleta kama kiongozi wa juu. Au fikiria au muulize Mrema ikiwa amewahi kukubali kuachia madaraka kwa wengine badala yake. Mrema ni mzee, wakati ulishafika wa yeye kuachia wengine nafasi hasa vijana. Anathubutu vipi kutoa kibanzi cha jicho la mwingine wakati boriti ya jicho lake inamngoja?

Huyo ni Mrema, rudi kwa Seif sharif Hamad, huyu ndugu naye yupo kwenye duru za kisiasa tangu miaka ya themanini au nyuma zaidi. Uliza wapi aliwahi kukubali kushindwa. Kwa busara zangu ndogo kama mbegu za haradani mwaka jana nilidhani Seif angewaachia wengine hasa vijana nafasi, sio ya kugombea urais tu, hata katika ngazi ya chama cha CUF, maana si chao kile, ni chama cha wananchi kama mimi na wengine. Wako vijana wazuri sana kama wakina Mbowe, John Mnyika na Zito Kabwe wa CHADEMA. Wanathubutu vipi kuizodoa CCM kuwa imekaa muda mrefu madarakani hivyo iondoke wakati wao nao wanasubiriwa na wanachi watangaze kuwaachia nafasi wenye damu changa ili nao wajaribu?

Seif na Lipumba wamegombea nafasi za urais mara tatu bila mafanikio, bado hawajasema kama wanaanda watu wengi wa kuchukua nafasi zao au la. Hii ni dalili kuwa wanajipanga upya ili warudi kwenye kugombea tena.

Wakati wao wanajipanga, na vijana tujipange, tusingoje wakati wa Kampeni watulemaze na kofia na tisheti na maneno matamu kuliko asali……..

Baada ya makala hiyokutoka, msomaji mmoja akanitumia ujumbe mfupi kupitia simu yangu ya mkononi. Akanishauri kuwa mimi na wasomi wenzangu (kama alivyotuita mwenyewe) tuanzisha chama cha vijana ili wao watufuate. Na kwa ushauri wake, alitaka chama hicho kiwe cha vijana.

Jumatano iliyopita, msomaji wangu huyu amerudia tena kutoa ushauri wake, nikaona si vyema nikae kimya, nimeona nimjibu yeye na wengine wenye ushauri kama wake. Lakini pia nataka nitoe elimu kwa watanzania kuhusu mabadiliko ya nchi yetu na Siasa.

Moja kati ya vitu ambavyo naendelea kujifunza katika nchi hii ni kwamba tunaweza kuleta mabadiliko katika nchi yetu bila kuwa wanasiasa. Sisemi kusiwe na wanasiasa, nasema sio lazima tuwe wote wanasiasa.

Wengi tunafikiri kuwa ni mpaka tuwe wanasiasa ndipo tunaweza kufanya kile ambacho wanasiasa walitakiwa kufanya. Kuna umuhimu wa kutumia mifano hai katika nchi yetu kuona dhima ya vyama vya siasa katika nchi yetu. Fikiria tu kwa makini, je tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa uanze hapa nchi, unaelekea kutufikisha kule tunakotaka? Unaitafsiri vipi tabia ya wanasiasa kutoka na kurudi CCM? Je ni maendeleo hayo? Wapi tabia hii itaifikisha Tanzania katika mchakato wa Demokrasia.

Huko siko kwa leo, hapa nataka nikwambie kuwa kama unafikiria uwe mwanasiasa ndipo ulete maendeleo katika nchi hii umechelewa, maendeleo hayataletwa na wanasiasa pekee, tunanahitaji sura mpya za watu, hizi naziita WANAHARAKATI, hebu sema kwa sauti, WANAHARAKATI. Hapa sizungumzii NGO’s, maana nazo ni harakati, lakini ikumbukwe kuwa nyingi zimepoteza imani kwenye macho na mioyo ya jamii, kwa sababu wengi wako kwa ajili ya pesa, na mapinduzi au maendeleo hayaletwi na pesa, yanaletwa na fikra safi na pevu.

Kam unakumbuka wiki iliyopita nlikuambia kuwa nchi yetu inahitaji watu wenye kufikiri na kuchukua maamuzi sahihi kwa wakati sahihi. Hatuhitaji kungoja tena ahadi za wanasiasa, ambao wengine hulala tu bungeni, wengine huacha miswada isiyo na manufaa kwa wanyonge ipite. Tunahitaji watu wa harakati za maendeleo. Ifahamike mapema kuwa harakati ni gharama. Harakati ni pamoja na kukubali kuibadilisha akili yako, kuileta kwenye zama mpya pamoja na kukabiliana na kila hila kutoka kwa wapinga maendeleo.

Usingoje uwe na chama cha siasa, zungumza na watanzania wenzako kuhusu hatima ya nchi hii, unapotoka darasani acha kuzungumza habari za upuuzi, usizungmzie mavazi aliyovaa mwalimu siku hiyo, tafuta vitu vya maana kuhusu mustakabali wa Taifa lako. Kama huna wa kuzungumza naye, nenda chumbani kwako fikiria utafanya nini, unapokuwa kwenye daladala usizungumze haba za Amina Chifupa kuachana na Mumewe, hazitakusaidia na wala hazikuhusu. Zungumza na watu kuhusu taifa lako, unaweza kuniambia kuwa kuzungumza pekee hakutoshi, sawa, kitu namaanisha hapa ni kwamba, jenga roho ya uzalendo ndani ya mioyo ya Watanzania wenzako.

Muda mwingi unaotumia kuangalia mechi za Chelsea na Arsenal, zungumza na watoto wako kuhusu Tanzania. Japo kwa kutafakari tu. Alinifurahisha mwalimu wangu mmoja Chuoni, alisema hivi, kulikuwa na Mtanzania mmoja aliyekuwa akiishi nchini Uingereza, alipokuwa huko alikuwa akiwaambia watoto wake tangu wakiwa wadogo, kwamba London sio kwenu, kwenu ni Tanzania. Huu ndio uzalendo, na hatimaye huyu jamaa amerudi nchini baada ya maiaka 25. Nakosa lugha rahisi kukutolea kile kilicho ndani ya moyo wangu. Nasema tuanze kuelimisha watoto wetu vile wanavyotakiwa kuwa wakiwa watu wazima, kila unapozungumza nao, zungumza nao kwa habari ya kuinasua Tanzania kutoka katika rushwa, waeleze watoto wako madhara ya rushwa. Zungumza nao juu ya dhuluma na madhara yake. Waeleze pia kwa nini mahabusu wanagoma kushuka kwenye makarandinga, uwaambie adai ya mahabusu hao, waeleze chanzo cha kugoma kwao, na nini wao kama watanzania waje wafanye wakija kuwa na ufahamu wa kutosha.

Wajengee watoto wako na watanzania wengine nidhamu ya kujisomea historia ya nchi hii, ilikotoka, wasome makala za wachambuzi mbalimbali katika magazeti na vyombo vingine vya habari. Lakini wachambuzi wale tu ambao hawanunuliwi na kuisaliti jamii ya Watanzania.

Haya yote uyaanze wewe, ndipo uwafuate wengine, hii ni moja tu kati ya harakati rahisi sana kwa ajili ya manufaa ya mbeleni mwa nchi hii. Ukiwa mvivu na mbinafsi hutaiweza, na usipowza harakati rahisi kama hii, hutaweza zile walizofanya wakina Martin Luther King, Jr wakina Malcom X na wengine wengi. Wakati mwingine harakati zao ndugu hawa zilihitaji fedha nyingi sana, ambazo wewe leo huna.

Kwa kumalizia tu, hebu soma hotuba hii ya Martin Luther kwa ufupi upate kidogo maana yangu.

Everybody can be great, because everybody can serve. You don’t need a college degree to serve.You don’t have to make your subject and verb agree to serve. You don’t need to know about Plato and Aristotle to serve. You don’t have to know the second theory of thermodynamics to serve. You only need a heart full of grace. A soul generated by love. You don’t have to know Einstein’s Theory of Relativity to serve. You just need a heart full of grace.

MAKALA ZANGU KABLA SIJAWA NA BLOGU, ZISOME ZITAKUSAIDIA PIA!

Mheshimiwa Rais, Jakaya Mrisho Kikwete, akiwaahidi watanzania mambo kemkem wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2005

MGOMO WA MAHABUSU, JE TUMEPATA SOMO?


Wiki iliyopita vichwa vilivyotawala magazetini hapa nchi ni juu ya mgomo wa mahabusu. Mahabusu hao waligoma kushuka kutoka katika makarandika, kwa maneno mengine ni kusema kwamba, walisitisha shughuli za mahakama, japo kuna kesi zingine za kawaida ziliendelea kama kawaida. Mahakama za Kisutu na Temeke ni miongoni mwa wahanga wa mgomo huo.

Mgomo wa mahabusu umetokana na kitendo cha mtuhumiwa wa mauaji ya bila kukusudia na aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri kupewa dhamana na kutoka rumande. Mahabusu wamelalamika kuwa iweje kesi yake imeenda haraka kiasi hicho hali kuna watu miongoni mwa mahabusu hao wana kesi za miaka mingi nab ado hawajapewa dhamana? Hili swali ni la maana sana, kila mtu alijiuliza, kulikoni? Wengine tumewasikia mitaani kuwa hawajashangaa, hawajashangaa kwa sababu kesi ya Dito ni kesiya mtu Mkubwa, kwa hiyo mahakama inamlinda mkubwa (si madai yangu, ni watu mitaani)

Narudia tena kauli ambayo nimekuwa nikiitoa mara kwa mara, kwamba sio kila tetesi za mitaani ni za kupuuza, japo wazungu walisema ‘no research no right to speak’ eti bila utafiti huna haki ya kuzungumza. Najiuliza, ni watanzania wangapi wanajua maana ya utafiti? Wangapi wanajua kufanya utafiti? Wangapi wanajua kuandika taarifa (ripoti) baada ya utafiti? Kuna watanzania wengi wanafahamu ukweli (facts) lakini hawajafanya utafiti, mazingira na uhalisi wa mambo umewapa kujua ukweli.

Hebu tutoke huko, tayari Dito yuko nje kwa dhamana. Na pia elewa tu kuwa, chanzo cha mgomo huo ni baada ya kuachiwa kwa dhamana kwa aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Tabora, yeye anakabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia Novemba 4, mwaka jana. Moja kati ya vitu vilivyonitia moyo katika mgomo huu ni matamko yaliyotolewa na wanaharakati na wanasheria mbalimbali nchini.

Kwa mfano Mkurugenzi wa kituo cha haki za binadamu (LHRC) Helen Kijosimba alinukuliwa na vyombo vya habari kwamba amefurahishwa na mgomo huo kwa kua unaonyesha namna mahabusu hao wanavyofahamu jaki zao.

Mwingine ni Mkurugenzi wa chama cha waandishi wa habari wanawake (TAMWA) Ananilea Nkya, alinkuliwa akisema kuwa kama suala la ucheleweshwaji kesi unatokana na upungufu wa vitendea kazi na maofisa upepelezi, ni heri serikali ikaongeza bajeti ili kurekebisha mapungufu yaliyopo.

Nimefurahishwa pia na hatua ya Mwenyekiti wa chama cha DP, mchungaji Christopher Mtikila, huyu wengi wanamchukulia kama hamnazo, lakini kama kuna watu wenye mchango mkubwa kwa demokrasia ya nchi hii, basi Mtikila ni mmoja wapo. Mtikila ameamua kumshitaki tena Ditopile kwa mauaji.

Sielewi kwa upande wa Watanzania wenzangu wameuchukuliaje mgomo wa mahabusu hawa. Lakini kwangu moja kwa moja nilizikumbuka filamu mbili nilizowahi kuangalia tangu nikiwa mdogo. Filamu hizi ni ‘Escape from Sobibor na ile fiamu ya Afrika ya kusini, ‘Sarafina’ je umewahi kuzngalia filamu hizi.

Baada tu ya kufuatilia mgomo ule ilinijia picha ya Wayahudi waliokuwa wakiteswa na Manazi wa dikteta Adolph Hitler wa Ujerumani. Hitler aliwachukua Mayahudi hawa na kuwaweka kwenye kambi moja iliyoitwa Sobibor, wanahistoria wengine wameiita kambi hii ‘Jehanam ya Sobobor’ au Kambi ya mauti. ilifananishwa na jehanamu kwa sababu ya mateso ambayo Askari wa Hitler waliwapa Wayahudi. Watu walichomwa moto wakiwa wanajiona, walipigwa risasi hadharani. Wanawake waliteswa uchi mbele ya waume na watoto wao. Kila walipo jaribu kutoroka haikuwezekana, kwanza ulinzi ulikuwa imara, nje na ndani ya kambi. Baadhi ya maeneo hayo kulitegwa mabomu.

Lakini siku moja Wayahudi Fulani wachache waliamua kujitoa mhanga, walianza mauaji ya siri kwa askari mmoja mmoja wa Hitler ikiwa ni katika harakati za kutoroka jehanamu ile.

Kama kumbukumbu yangu iko swa, basi kuna Myahudi mmoja alisimama na kuwatangazia wenzake kuwa, wakati wa kuondoka umefika. Akatangaza kuwa katika kutoroka kwao ni kujitoa muhanga, na kwamba katika zoezi lile si kila mmoja angepona, kwamba wengi wangekufa, lakini akawataka wale watakaobahatika kupona waende wakaiambie dunia mambo ambayo walikabiliana nayo na habari ya ndugu zao watakaokufa katika zoezi la kutoroka. Ikumbukwe kwamba kambi ilizungukwa na minara ya walinzi wenye silaha, lakini Wayahudi hawakulingalia hilo, baadhi ya sehemu ambzo wangepita kulitegwa mabomu, hilo hawakulitazama. Njia mbazo wangepita zilizibwa na seng’enge, hilo nalo hawakulijali. Unajua kwa nini? Walichoka! Hili ndio jibu rahisi ninaloweza kukupa.

Inasemekana kuwa mpaka mwisho wa harakati hizo, takribani Wayahudi 250,000 walikufa, na ni wafungwa 48 tu walionusurika.

Ukirudi kwa upande wa Sarafina, huko nako utakutana na hali ya ubaguzi ilivyokuwa nchi Afrika ya kusini. Waafrika waliishi kama wafungwa katika nchi yao wenyewe. Wanafunzi wa shule moja huko Soweto waling’amua kuwa wako matesoni. Mara nyingi walifanya harakati zao chini kwa chini, hii ilitokana na uoga, waliwaogopa makaburu. Mara nyingi Makaburu waliwatesa kwa kuwabiga mijeredi wanafunzi hawa, si hivyo tu, walivuka mipaka kwa kuwapiga risasi. Lakini siku moja ilifika, walisema maneno haya, “Mnaweza kutuumiza, lakini hamuwezi kuzuia, mnaweza kutuua, lakini tutaishi tena” Hizi zilikuwa ni salamu maalumu kwa Makaburu, ambao waliringia silaha zao za moto, lakini ulifika wakati Wanafunzi hawa waliringia umoja wao. Wakiwa wanasema maneno hayo, mbele yao kulikuwako vifaru, kulikuwapo mitutu ya bunduki, lakini kamwe hawakujali. Unajua kwa nini? Walichoka!

Ninachotaka nikuambie hapa ni hiki, kwamba jamii yoyote ikichoka manyanyaso, basi huamua lolote, liwe la madhara kwa upande wao au upande wa pili. Hili ni somo ambalo watawala wanapaswa na kulazimika kujifunza kila siku, hata kama hawataki, nasema wanalazimika kujifunza. Jamii inapochoka manyanyaso, hata ungenyoosha mitutu ya bunduki zinazowaka moto, kamwe huwezi kuwarudisha nyuma.

Yeyote anayedhani yuko juu, na kwamba kwa sababu tu yuko juu, basi anaweza kuwafanya lolote wale walio chini yake, basi ajifunze somo hili. Mahabusu waliamua kutoshuka kwenye makarandinga. Chini ya makarandinga hayo, walikuwepo askari wenye silaha, hilo halikuwapa shinda mahabusu wale. Unajua kwa nini? Walichoka!

Madai ya mahabusu ni ya msingi mno, madai yao yaliambatana na maswali ambayo mtu yeyote mwenye akili timamu angejiuliza. Hautuwezi kuingilia uamuzi wa mahakama, lakini hatuwezi kuzuia hisia, kwamba kwa nini kesi ya Ditopile imeenda haraka wakati kuna mahabusu wana kesi ambazo hazijakamilika kwa miaka kadhaa sasa? Jamni hili ni swali la maana. Mahabusu wakaona hawana jinsi, ikabaki kugoma, Inawezekana kuna waliowatahadharisha kuwa wakigoma wangepigwa virungu, lakini wao hawakujali virungu, walitazama mbele, kudai haki zao za msingi kikatiba.
Sitaki kuzama sana huko, nilitaka tu nikuonyeshe na kutahadharisha kuwa jamii au mtu yeyote akichoka, basi hakuna namna unayomzuia, ni vizuri tukakinga kabla ya kutibu. Maana tiba ni ghali kuliko kinga. Kila anayestahili kupewa haki katika nchi hii na apate haki yake kwa wakati na bila mizengwe.

Tafadhali, nimetoa mawazo yangu tu hapa, naomba nisije itwa mchochozi, badala yake tuungane na kuona namna ambavyo tutazuia ya kina Sobibor na Sarafina yasitokee kwetu.

MWAKA MMOJA WA KIKWETE IKULU NA MATUMAINI YA WATANZANIA!



Naombeni sana sana , mnifikishie salamu hizi kwa Rais wangu mpendwa, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Wiki hii na iliyopita kumeandikwa mengi sana katika vyombo vya habari kuhusu siku 365 (mwaka mmoja) za rais Kikwete kuwepo madarakani. Yamesemwa mengi, wapo waliopongeza utendaji wake na wapo waliobeza.

Haya yote ni ya kawaida katika jamii, ndani ya wale wanaopongeza wako wanafiki wanaotaka tu kumpamba rais wetu pengine kwa lengo la kumpumbaza ili apunguze kasi yake ili wao wapate nafasi ya kufanya uharamia.

Kwa upande wa wale wanaobeza huko nako kuna wanafiki, hawa pengine wanaponda na kukejeli bila kuelewa A wala B ya kile wanachofanya, ni mkumbo tu! Katika makundi hayo mawili bado wapo walio makini wenye uelewa na umakini wa kile wanachofanya.

Kwenye gumzo hili la leo, sina mengi ya kusema juu ya utawala wa Kikwete kwa siku 365, ninachoweza kusema ni kumtia moyo na kumpa ukweli kuwa akaze buti, hali bado ni rhumba kali. Safari bado ni ndefu! Nikiwa kama mzalendo wa nchi hii sina sababu ya kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa, nimeshuhudia watu wengi wanapoanza kuzungumzia utawala wa Kikwete mara hurejea kwenye hotupa zake na kwenye mikutano ya kampeni. Akiwa mgombea wa urais kupitia C.C.M Kikwete aliwakuna sana watanzania kwa ahadi zake kemkem. Ahadi hizo zilikua nzito na nzuri, akadiriki hata kusema wazi kuwa kama kuna ahadi ambazo atasahau basi ruksa kukumkumbusha.

Aliwapa matumaini makubwa sana watanzania, mara nyingine ninaporudi nyuma kuangalia historia ya viongozi wa nchi hii najikuta namuonea huruma rais Kikwete. Namuonea huruma kutokana na ukweli kwamba je asipotimiza ahadi hizo atawaeleza nini watanzania? Ni ahadi nzito na nyingi mno, huruma yangu inazidi nikiwaza ikiwa alitoa ahadi hizo ili apate kuingia Ikulu au kwamba kweli amedhamiria kweli kuikwamua nchi hii.

Unajua kwa nini nasema namuonea huruma? Watanzania ni miongoni mwa Waafrika wanaosota kimaisha kutokana na pengine sera mbovu za wanasiasa au ufisadi na ubinafsi wa viongozi wa nchi zao. Watanzania wamesubiri kwa hamu kubwa kiongozi kama Kikwete, ambaye anaweza akakiri tatizo hadharani bila kuficha wala kupamba kwa unafiki ili kuonekana kiongozi mzuri bila kujali kuwa anaua watu wake. Watanzania hawajasahau dharau na ubabe wa viongozi wao kama ule wa Basil Mramba aliyekuwa waziri wa fedha katika serikali ya awamu ya tatu, aliyeidhinisha ununuzi wa ndege ya rais kwa mabilioni ya shilingi huku nchi ikikabiliwa na janga la njaa.

Na mramba kwa jeuri kubwa akasema bora watanzania wale majani kuliko kuacha kununua ndege ya rais, eti watanzania wale majani? Kila ninapoikumbuka kauli hii, hushikwa na uchungu na machozi hunilenga. Hivi kweli Mramba alitudharau kiasi hiki watanzania? Sisi ambao nchi hii ni mali yetu na wala si wakimbizi au wavamizi. Anatusimanga katika nchi yetu wenyewe?

Kidonda hiki cha wananchi hakijapona bado, kilitoneshwa zaidi pale waliposikia kuwa Mramba yuko tena ndani ya baraza la mawaziri, sio kila mtu alimwangalia vizuri Mramba a.k.a ndege ya rais, tukadhani atajirekebisha.

Baada ya muda tukasikia kuwa amemdanganya rais kuhusu ujenzi wa barabara ya shekilango na Sam Nujoma jijini Dar es salaam , kama hiyo haitoshi nasikia kule Mtwara au Lindi aliwahi kumkera hata waziri Mkuu, Mh. Lowassa.

Mramba kaja kuboa zaidi baada ya kutangaza kubadili jina la uwanja wa ndege wa Mwalimu Juliasi (Julius ni kizungu) kambarage Nyerere kwa kisingizio kuwa eti wazungu wanashindwa kutamka jina hilo . Yaani sisi (na Kikwete) bado tunatawaliwa na fikra na maamuzi ya wakoloni wetu wa zamani?

Huyu ndiye Mramba! Viongozi wababe na viburi kama huyu Mramba wamewachosha watanzania, wanamwangalia kwa hamu kubwa rais Kikwete kuona kuwa je, atarudisha niadhamu ya watu serikalini wakiwemo mawaziri. Je atajenga tabia ya mawaziri kuenenda kama watumishi na sio wafalme na masulutani au la?

Watanzania wana hamu kubwa sana kuona ubabaishaji na mizengwe inakomeshwa serikalini. Wasingependa kuona tena mikataba ikisainiwa kimizengwe zengwe bila taarifa kwa wananchi ambao ndio wenye nchi hii, kufanya mambo kwa siri ni kutowatendea haki wananchi.

Baada ya kutangaza kuwa mikataba yote yenye utata serikali yake (Kikwete) itapitia upya ili kubaini mianya ya rushwa, watanzania walisubiri kwa hamu sana kuona mikataba ya awamu ya nne itakuwaje.

Leo wamekuja hawa wanaoitwa Richmond Development ili watuzalishie umeme, baada ya kuwa kizani kwa takribani mwaka sasa. Tayari minong’ono imeanza mitaani. Mara nyingi huwa nashauri kuwa mazungumzo na tetesi za mitaani sio za kupuuza sana . Watu wanaisema vibaya Richmond hata kabla haijashusha mashine zake.

Ibrahim Msabaha aliyekuwa waziri wa niashati kabla hajabadilishwa na kupelekwa wizara ya Afrika Mashariki. Yeye aliwaahidi watanzania kuwa umeme ungekuwa tayari kufikia Oktoba 15 mwaka huu. Kufikia wakati huo umeme haukuwa hata na dalili. Kwa hali hiyo watanzania tukaanza kukumbushwa mizengwe, ubabaishaji na udanganyifu, kwa imani waliyokuwa nayo watanzania kwa Kikwete hawakutegemea ubabaishaji huu kutoka kwa mawaziri wake.

Kusema hivi haimaanishi kuwa hakuna zuri ambalo Kikwete amakwishalifanya. Wote ni mashahidi kuhusu hali ya ujambazi ilivyokuwa nchini. Ilikuwa kana kwamba imetangazwa kuwa kutofanya ujambazi ni kosa la jinai, lakini rais wetu alilivalia njuga. Kusema ujambazi umeisha ni kosa, ujambazi upo, ila kwa kiwango kikubwa raia wamarejea katika usalama. Wamebaki vibaka mitaani ambao wanasumbua sana raia. Wakazi wa Tandika wanaelewa ninachosema. Hivi karibuni nilikatwa viwembe mkononi na vijana ambao walitaka kunipora simu yangu, tena ni karibu kabisa na kituo cha polisi. Kabla ya hapo kuna vijana walifanikiwa kunipora simu pale uwanja wa Taifa. Vibaka ni wengi sana mitaani. Tuna imani kuwa kasi aliyoianza rais dhidi ya uhalifu nchi itaendelea na kutokomeza kabisa. Haya ndio maombi ya wazalendo wote wa chi hii.

Kikwete pia ameonyesha kuwa ni kiongozi asiyependa makuu, ameonyesha kuwa karibu mno na wana nchi wa Tanzania .

Narudia kusema, kuwa yako mengi mazuri ambayo Kikwete amefanya lakini kwa wale wasomaji wa Biblia wanaelewa fika kuwa Bwana Yesu aliwahi kusema “chachu kidogo huchachua donge zima” Bila shaka rais Kikwete anaelewa fika hili, kwamba umeme na mambo mengine yametia doa utawala wake, kauli za baadhi ya mawaziri kama vile aliyekuwa waziri wa Nishati na madini Ibrahim Msabaha, kwa kiasi Fulani vilichafua utawala wa rais wetu mpendwa. Mtu kama Basil Mramba, anasemwa mengi sana mitaani, huyu anatia doa uatawala wa Kikwete, nani asiyejua vituko na ubabe wa Mramba dhidi ya wananchi tangu awamu ya tatu kama nilivotangulia kusema hapo juu.

Kikwete una safari ndefu baba, binafsi niko nyuma yako, tunakuombea na kukutia moyo, songa mbele. Hongera kwa juhudi, lakini ongeza maarifa. Uliwaahidi mengi sana watanzania, muombe Mungu akusaidie, kukusifia siwezi, maana nakutakia mema baadae, nataka uondoke tukiwa tunaendelea kukutamani na kuenzi uongozi wako.

Una nia njema na taifa letu, ndivyo unavyoonekana kama hutakuja kutugeuka, lakini uwe makini sana na watendaji ulionao. Hapa nina maana ya mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya. Usiwaamini moja kwa moja, watakuponza na kukuangusha. Kumbuka mheshimiwa rais kuwa hii nchi ina wenyewe, kumbuka mlipotaka ridhaa ya wana nchi kuwaruhsu muingie Ikulu haukua peke yako, alikuwepo Lipumba, Mbowe, Mvungi, Mrema, Shayo, na wengine wengi. Lakini Tanzania ikakuamini wewe, imani yao kwako isije ikageuka kuwa majuto, umekubali urais umekubali majukumu mazito sana . Yabebe kwa miaka hii mitano.

Usiruhusu mafisadi wafanye mizaha na maisha ya watanzania daima dawamu, uwe unawauliza na kudadisi matatizo yao . Kamwe usije ukalewa madaraka na kujiona Mungu katika nchi hii.

Ulipewa tu hii nchi kwa muda, una deni kwa watanzania, pigana kiume uhakikishe unalipa deni hilo . Rejea hotuba yako ya bungeni kwa mara ya kwanza, rejea yale uliyoyasema kwenye viwanja vya kampeni sehemu mbalimbali katika nchi hii, kaa chini omba ushauri kwa watanzania, sio lazima wawe wakina Mramba na Msabaha, wako watu kama wakina Kristofa (Christopher ni Kizungu) Mwakasege kwa masuala ya kiuchumi na kina Natanaeli Rusumo na wengine wengi.

Tunao wasomi na wasio wasomi wengi sana , lakini wenye mchango mkubwa wa kimawazo kwa ajili ya nchi yetu. Kaa na wanaharakati na wanahabari kama wakina Privatus Karugendo, Joseph Mihangwa, Ndesanjo Macha na wengine wengi ambao sijawataja, Sisemi uwape ukuu wa mikoa au wilaya au cheo chochote serikalini, Lah! sio hivyo, ila sio mbaya kama utawaita siku moja moja, uwe kama unafanya nao mazungumzo ya kawaida, naamini watakusaidia hawa. Kuna watanzania wana mawazo mengi sana ya maan.

Usiwaogope waandishi wa habari au vyombo vya habari na wanahabari. Jenga nao urafiki, ni watu muhimu sana hawa, sijajua ni kwa nini bado vyombo vya habari havijatangazwa kuwa ni mhimili wa nne wa serikali. Watakusaidia sana sana . Waondolee hofu, wahakikishie ulinzi na wajengee moyo wa uzalendo na ujasiri kwa ajili ya Taifa lao. Rejea makala yangu ya wiki mbili zilizopita.

Tunapoandika makala kama hii, lengo sio kukutukanisha, kukupaka matope, kukuvunja moyo au kukuzodoa, tunakusaidia, si unajua kuwa vita hii ya kuijenga nchi peke yako huiwezi? Shirikiana sana na vyombo vya habari, watakusaidia sana katika kukupa taarifa muhimu. Wape meno hawa, lakini sio meno bandia wakageuka kuwa ‘toothless dogs’. Fuatilia sana mijadala kuhusu muungano na mgogoro wa kisiasa Zanzibar katika magazeti, naamini waandishi wana mchango mkubwa sana .

Mheshimiwa rais, si kwamba nakufundisha kazi, natoa tu ushauri, hapa nataka nikushauri jambo lingine, kwamba uwe na uso gumegume, usifanye kazi ya kumfurahisha wala kumkwaza mtu. Fanya kazi ili kulikwamua Tiafa letu kutoka mahali lilipokwama, enzi za kulindana na kuoneana haya zikomee hapa kwenye awamu ya nne! Usimwangalie mtu kwa uso wa huruma, anayestahili kuinuliwa muinue lakini baada ya kuona kazi yake njema, anayestahili kushushwa ashushwe haraka kabla hajaharibu na kutuangamiza. Cheka na watu lakini huku ukijilinda wewe, ukiilinda heshima ambayo watanzania wamekupa na kuwalinda watanzania.

Niruhusu niongeze ushauri mwingine wakati namalizia, kwamba uwe makini sana na wazungu, ni rafiki wazuri sana lakini mh…… ungekuwa ni mtu unayepatikana kirahisi ningekuletea kanda ya mwimbaji mmoja ambaye anaimba kuhusu ushirikaiano kati ya wazungu na waafrika, na lengo la wazungu katika ushirikiano huo, mwimbaji huyu anaitwa
Faustine Munishi, ni mtanzania anayeishi jijini Nairobi, Kenya.

Kanda hii imelaumiwa sana , lakini ningeomba usikilize, pengine wanamlaumu mwimbaji kwa sababu ya kusema ukweli. Kama ungependa kuisikiliza kanda hiyo, nijulishe tu nitumie njia gani kukufikishia. Nataka uisikilize sio kwa ajili ya kujiburudisha, isikilize ili ujue ukae vipi na wazungu wanapojaribu kuonyesha fadhili zao kwetu kama taifa, kumbuka nimekwambia sio kila neno la mtu asiye kiongozi ni la kupuuza.

Hongera kwa kutimiza mwaka mmoja, lakini lengo bado, safari ni kama inasua, japo ni katika baadhi ya mambo. Kumbuka uliahidi maisha bora kwa kila mtanzania, pia uelewe kabisa kuwa wewe ndio umeahidi kuwa Tanzania yenye neema inawezekana, watanzania walishasahau hilo, walijichokea, jua na mvua kwa ilikua sawa, liwike lisiwike kwao kutakucha tu, sasa umewakumbusha kuwa Tanzania yenye neema inawezekana, ulisema pia serikali yako haitakuwa na ubia na mtu (nafikiri uliwalenga watendaji wabovu na wazembe katika serikali yako hasa mawaziri) Wananchi wamesimamisha masikio yao, wamekodoa macho yao kuona na kusubiri utekelezaji! Kila la heri, tuko nyuma yako.



LOWASSA, TUNGEPAMBA KWANZA NDIPO TUSHEHEREKEE!


Leo nina ujumbe kwa ajili ya watanzania kupitia ofisi ya waziri mkuu. Kwa taarifa tu ni kwamba kuna watanzania wengi sana wanashangaa kuhusu maadhimisho ya miaka 45 ya uhuru. Hivi ni uhuru wa Tanganyika au Tanzania ? Kwani Tanzania iliwahi kutawaliwa na nchi gain. Eti kwa mujibu wa walimu wang wa historian a kumbukumbu zangu, Tanganyika (si Tanzania ) ndio iliyopata uhuru mwaka 1961. Ni haki yangu kuhoji swali hili, ni muhimu, historia isipotoshwe. Naomba mhariri aruhusu mjadala katika hili. Kwa nini tusheherekee uhuru wa Tanzania badala ya Tanganyika ? Nasikia Rais Kikwete aliwaimbisha watanzania ‘happy birthday’ mimi nadhani haukuwa muda mwafaka kuimba wimbo huu wakatai wa uhuru. Mahali pake ilikuwa ni tarehe 26 mwezi wa nne wakati wa sherehe za Muungano. Hapo ndipo Tanzania ilizaliwa.

Mimi ni mmoja wa watanzania waliopigwa na mshangao juu ya michango iliyoendeshwa na ofisi ya waziri mkuu kwa ajili ya kusheherekea miaka 45 ya uhuru. Tena wengi wa wale wanaolalamika ni watu wa hali chini kimaisha. Unaweza ukanihoji, kwa nini sikuandika wakati zoezi lile likiendelea? Sio siri nilikuwa nasubiri kujua ni kiasi gain kingepatikana, licha ya hayo hata ningeandika kwa uzoefu tu siamini kama zoezi hilo lingesitishwa.

Nilishtuka sana baada ya kusikia kupitia vyombo vya habari kuwa jumla ya michango ilipatikana ni 330 mil. Baada ya kusikia kiasi hicho cha fedha haraka akili yangu ilijaa maswali mengi bila majibu. Simlamu Lowasaa na wasaidizi au washauri wake, pengine alipitiwa, nadhani kama atapata taarifa za makala hii atakiri kuwa kweli alipitiwa, japo si hadharani, hii ni ngumu sana kwa watawala wetu.

Nilijiuliza, hivi kwa ni lazima tusheherekee siku ya uhuru? Kwa nini? Ni kanuni gain au kifungu gain cha Sheria za nchi hii kinachoibana Serikali kuandaa sherehe hizi kila mwaka? Nani atatushtaki tusipofanya sherehe hizo?

Kilichoniumiza mpaka kujihoji maswali haya yote si kingine ni hayo mamilioni yaliyopatikana baada ya michango. Nikipitia gazeti moja la kila siku, linaripoti kuwa katika sherehe za mwaka huu, rais alitimiza ahadi, kwamba zingekuwa za kishindo na shamrashamra nyingi (mbwembwe)

Eti sababu kubwa ya kufanya sherehe hizo kuwa zaina yake ni kuamsha ari ya uzalendo miongoni mwa wananchi. Hivi kweli uzalendo unaletwa kwa kufuja pesa kiasi hicho wakati hao wanatakiwa kuwa wazalendo wana hali mbaya kimaisha?
Usikasirike mheshimiwa waziri mkuu. Wewe ni mtanzania na mimi ni mtanzania, tunasaidiana kwa kushauriana kama hivi, wala usinielewe vibaya, na kama lugha ninayotumia ni kali sana, jaribu kunivumilia tu!

Nauliza hivi, kwa nini tunasheherekea? Tunasheherekea nini? Matunda ya uhuru tulionao au uhuru wenyewe hata kama hakuna maana wala faida ya kuwa huru? Haya ni maswali ambayo nadhani yanahitaji mjadala miongoni mwa wananchi. Tunahamiaje kwa mbwembwe kwenye nyumba ambayo bado iko kwenye msingi?

Nikichukua mizani katika ufahamu wangu na kupima kati ya umuhimu wa kuchangia sherehe za uhuru na matatizo yanayotukabili kama taifa, najikuta sioni uhalali wa kufanya sherehe hizo.

Sherehe zina mbwembwe nyingi kuliko uwezo wa taifa na wananchi wake. Najikuta tena kuwa pengine nia ya Serikali kuandaa sherehe hizo kwa mbwembwe kiasi kile ni kutaka sifa. Lakini ili iweje.

Mbwembwe za aina ile zinampatia faida au ahueni gain mkulima wa korosho kule Masasi, mkulima wa nyanya kule bumbuli Lushoto, mkulima wa chai kule Tukuyu, Mbeya na Amani Tanga.

Sipingi kusheherekea kama ni muhimu, napinga matumizi ya fedha kwa kiasi kile kwa sherehe ya siku moja tu.

Hivi kweli waziri mkuu hakuona vitu vya kuitishia mchango katika nchi zaidi ya Desemba 9. Hajui au kasahau kuwa Tanzania ina matatizo. Kama hajui anakubali vipi wadhifa wa kuwa kiongozi. Maana ninachojua kiongozi ni mtu anayeonyesha njia kufika kulikokusudiwa. Sasa kam hajui njia anangoja nini kuwapa nafasi wengine.

Wanafunzi wa vyuo vikuu bado hawajakauka kile kidonda au jeraha lililosababishwa na Serikali yao . Serikali ilitangaza kwamba haitatoa mikopo kwa wanafunzi wa kiume isipokuwa wale tu wenye daraja la kwanza. Sikiliza! Wavulana hawatapewa mikopo mpaka wapate daraja la kwanza, hata kama wana sifa za kujiunga na vyuo vikuu. Kwa upande wa wasichana wao watapewa mikopo kuanzia daraja la pili na la kwanza tu! Angalia ubaguzi huu! Niliwahi kumbiwa kuwa sababu iliyopelekea hayo yote ni uhaba wa fedha kwa Serikali yetu.

Kama suala ni fedha, kwa nini ofisi ya waziri mkuu isiitishe michango hiyo ili bodi ya mikopo ya wanafunzi ipate fedha za kuwakopesha wanafunzi. Fedha zilizotumika kwenye sherehe za uhuru zimekwenda hazitarudi tena. Lakini ikiwa michango itapita na kuipa bodi hiyo, fedha hizo hazitapotea bure, kwanza tutakuwa tu,epata wasomi, halafu fedha hizo wanafunzi hawachukui moja kwa moja, watazirudisha!

Hapa nashauri tu, kwamba kuliko kusheherekea, tupambe kwanza, nchi ipendeze. Na moja ya rangi za kuipendezesha nchi yetu ni elimu, kuwa na wasomi. Kusheherekea uhuru wakati hatuna wasomi ni kazi bure. Tuwe wavumilivu, tutasheherekea tu siku moja.

Hakuna mtu asiyejua tatizo la umeme katika nchi hii sasa hivi. Tunaambiwa kuwa chanzo chake ni kukauka kwa mabwawa ya kuzalishia umeme. Kwa nini tunasheherekea kabla ya kupamba? Kwa nini eneo la sherehe liko giza ? Nasema kwa nini tusiwashe taa kwanza ili hata wale wageni tuliowaalika wawe nuruni? Umeme ndio rangi ingine ya kupamba nchi ndipo tushereherekee. Nashauri na hapa, kwa sababu ofisi ya waziri mkuu imeonekana kuwa nzuri katika kuhamasisha michango, basi si vibaya kama ofisi ya waziri mkuu itachangisha tena mamilioni kujenga mabwawa. Kwa kuchangia milioni 330 kwa ajili sherehe za uhuru, inaonyesha watanzania wanaweza kuchangia kwa ajili kutatua tatizo la umeme. Aanze rais kuchangia, wafuate wabunge na mawaziri, madiwani, wanasiasa na wananchi wengine wa kawaida.

Waziri mkuu anafahamu (au kasahau?) kuwa wanafunzi hasa wa Dar es salaam wanapata shida kusafiri kwenye mabasi wakati wa kwenda shule na kurudi nyumbani. Naambiwa kulikuwa na mradi wa mabasi ya wanafunzi. Sijui uliishia wapi? Kuna mwanafunzi mwezi wa juzi alikanyagwa na gari katika harakati za kugombea kupanda gari wilayani Temeke. Vyombo vya habari vimeimba wimbo huu bila magari. Wazazi wamelalamika bila majibu. Sasa waziri mkuu ametuonyesha njia, kwamba michango ya wananchi inaweza kufanya makubwa kukiwa na hamasa chni ya usimamizi wake. Nashauri baada ya Sherehe hizi, ofizi ya waziri mkuu ichangishe tena kwa ajili ya kununua mabasi ya wanafunzi ili kuondoa kero hii.

Mapema mwaka huu, Rais Kikwete katika moja ya ziara yake alishuhudia makazi duni ya watu muhimu katika jamii. Hawa ni polisi wa usala wa raia na mali zao. Alishuhudia wakiishi kwenye mbavu za mbwa. Sio siri, nyumba za askari wetu ni duni, hazina hadhi kulinganisha na kazi kubwa wanayofanya. Umefika wakati mzuri sana wa waziri mkuu kuitisha michango kwa ajili kujenga nyumba za askari wetu. Hili ni muhimu sana kuliko kuchangisha mamilioni kwa ajili kulipua fataki, michezo ya kizungu isiyo na faida yoyote kwa maisha ya wazalendo wa kitanzania. Nashauri kuwa tupambe kwanza, ndipo tusheherekee.
Tunasheherekeaje wakati kuna wengine wanalia wanalia? Kufurika kwa watu uwanja wa taifa wakati wa sherehe hizo haimaanishi kwamba watu wale hawana matatizo. Hayo niliyoandika hapo juu ni baadhi tu!

Si vibaya nikashauri kwamba, kusheherekea kunatakiwa, lakini uliona wapi watu wanasheherekea siku zao za kuzaliwa wakiwa kwenye matanga, kwenye matatizo? Ndivyo tulivyofanya sisi. Huu ni ushauri kwa Serikali hii na Serikali zitakazofuata, kwamba tusitumie fedha katika kuanda sherehe kama hizi wakati hatujapiga hatua tunayopasa kupiga. Serikali na viongozi wawe na uchngu.

Uzalendo sio kuchangisha fedha kwa ajili ya siku moja tu kwa kisingizio cha kuamsha ari ya uzalendo miongoni mwa watanzania. Huo si uzalendo, uzalendo ungekuwa kuwahamasisha watanzania kuipenda nchi yao na kuwawezesha kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo yao binafsi na taifa kiujumla.

Wacha tuhenye kwa sasa, ikifika siku ya uhuru ni bora vyombo vya habari vikatangaza tu ili kuwakumbusha wananchi, wataadhimisha hata wakiwa majumbani mwao kuliko kutumia mapesa ambayo yangefanya kitu kingine muhimu kulikwamua taifa letu kiuchumi.

Labda nieleze wazi, kuwa najisikia vibaya kwa sababu tu zile milioni 330 zilitumika kwa siku moja tu. Na kilichoniongezea uchungu zaidi katika kuiandika makala hii ni taarifa za gazeti la Mwananchi la tarehe 11 Desemba, kuwa umeme wa Richmond ulikuwa bado.

Napenda pia kuchukua nafasi hii kumuuliza Waziri mkuu, kwamba ni hatua gain ofisi yake na Serikali kwa ujumla inachukua katika kuhakikisha kuwa inapata pesa za kuchimbia mabwawa kwa ajili ya kuzalisha umeme?

Serikali itapata wapi pesa za kuiwezesha bodi ya mikopo ya wanafunzi kuwapatia wanafunzi mikopo hiyo? Bila shaka waziri mkuu ana habari kuwa bodi hiyo inalazimika kukopa fedha kutoka taasisi mbalimbali za fedha kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi wenye sifa. Habari hii ni kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi la tarehe 9 Desemba siku ya uhuru. Hebu fikiria sasa! Ndio maana nikashauri kuwa ofisi ya waziri mkuu ichangishe fedha zingine ili kuisadia bodi hiyo.

Tuna mambo mengi yanahitaji fedha kwa ajili ya kuikwamua nchi yetu kutoka matatizo iliyo nayo. Ni vema tukayapa kipaumbele hayo ili tusonge mbele kimaendeleo. Viongozi wa Serikali wasifikiri kila maamuzi wanayo fanya ni sahihi na kwamba wananchi wanayafurahia. Baadhi ya waamuzi yanawakera sana wananchi wa Tanzania . Ukiwakuta wanalalamika mitaani utawaonea huruma, waweza dhani ni wakiwa au yatima walioachwa na wazazi wao wapendwa.

Wapo walio diriki kusema heri angekuwa mkoloni nchi hii tujue moja. Mimi sihitaji wakoloni warudi, siwataki, siwapendi. Nataka tujitawale weyewe, lakini katika kujitawala huko tuheshimiane. Kila mtu amhesabu mwenzake kuwa ni bora.

Watawala wakumbuke kuwa waliwekwa na wananchi madarakani. Wasifanye kila jambo kwa sababu tu wao wameona linafaa, japo usemi wa aliyeshiba hamjui mwenye njaa unafanya kazi. Viongozi wawe karibu na wananch na wafuatilie kwa karibu matatizo yao na kutafuta njia ya kuayatatua kwa pamoja.

Ningependa pia niwashauri viongozi wa Tanzania , wawe wacha Mungu. Pamoja na kwamba tunawaombea, lakini hili ni lao kwa kiasi kikubwa. Waombe hekima na busara ya namna ya kufanya maamuzi, naamini Mwenyezi Mungu ni mwaminifu, na hakika atawapa njia. Uzoefu na taaluma walizo nazo hazitawasaidia sana bila kumshirikisha mwenyezi Mungu. Maamuzi yenye busara ndio yatakayotupeleka kule tunataka kufika.

Tusisheherekee kwa sababu kuna nchi zinafanya hivyo siku za uhuru wan chi hizo, huo ni ulimbukeni, tuijenge nchi yetu kwanza katika mambo ya msingi na kasha tusheherekee. Natoa ushauri kwamba sherehe za mwakani za uhuru, wananchi tuambiwe, ni uhuru wa nchi gani? tunasheherekea, wa Tanganyika au Tanzania ? Kama Tanzania wananchi nasi tuhoji, mbona Tanzania haikuwepo mwaka Desemba 9, 1961? Kama ni Tanzania bara, nayo bado inaitwa Tanzania , Tanzania ni muunganiko wa majina ya nchi mbili, Tanganyika na Zanzibar .

Pili, sherehe za mwakani zilenge katika kutathimini mwenenndo mzima wa nchi katika kila eneo. Kiuchumi, kijamii na hata kisiasa. Tuangalie, je baada ya kupata uhuru, utamaduni tulionao ni wetu au wa kikoloni? Je badi hatutawaliwi kifikra na kiuchumi? Tufanye nini ili kujikwamua?

Ibara ya 18(a) cha katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania inanilinda. Hayo ni mawazo tu ya mimi Mtanzania. Pamoja na kuwa ni mawazo yangu, bado si busara kuyapuuza. Kwa sababu naamini kuwa Mheshimiwa waziri mkuu yuko ‘busy’ kiasi kwamba sidhani kama atapata muda kupitia kila gazeti, naomba wewe ambaye ni mtu wa karibu naye, uwe mjomba, kaka, dada, au hata jirani yake, mpelekee taarifa hizi.

Nilipata taarifa kwamba kuna ‘send off’ (jumatano iliyopita) ya binti wa waziri mkuu, nilitamani sana kuwepo huko, lakinmi nani anialike. Unajua kwa nini nilitamani? Si kwa sababu ya maakuli, lahasha, nilitaka niombe miadi naye ‘appointment’ ili nizungumze naye. Naamini nina mawazo mengi kama mwananchi na kama walivyo wananchi wengine wa Tanzania .

Au hata kama hatakuwa na nafasi ya kuonana na mimi, anipe nafasi ya kumwandikia barua ndefu ambayo ningependa aape, kama alivyoapa alipopewa wadhifa wa kuwa waziri mkuu. Aape kwamba pamoja na urefu wa barua hiyo, atakuwa mwaminifu kuisoma.
Wasalaam, wako mtanzania mpenda nchi yake,