Saturday, July 21, 2007

Happy Birthday Madiba

Nelson Rolihlahla Madiba Mandela

Naandika makala hii kwa heshima kubwa ya mwanaharakati chipukizi kabisa, mwanafunzi wa sekondari, Elizabeth David wa Arusha. Ni moja ya hazina zinazochipuka kwa taifa hili wakiwa na moyo wa uzalendo kwa Taifa hili, nikipata nafasi nitaeleza kirefu kuhusu yeye.

Leo namzungumzia Nelson Rolihlahla Madiba Mandela, kwangu huyu ni mmoja kati ya zawadi ambazo Mungu aliamua kuutunuku ulimwengu, namwita shujaa na hilo halihitaji ufafanuzi wala wakati wa mjadala. Maisha yake yanajieleza.

Alizaliwa kitongoji cha Transkei nchini Afrika ya Kusini tarehe 18, julai 1918, hii ina maana kwamba wiki iliyopita tarehe 18, jumatano mwana huyu wa Afrika alitimiza miaka 89. Kwa faida ya wasomaji wa safu hii, shujaa huyu alizaliwa na baba ambaye alikuwa chifu wa kabila la Watembu, aliitwa Henry mandela.

Miongoni mwa mambo mengi ambayo pengine wengi wetu hatuji labda kwa sababu hayajaripotiwa sana, ni kwamba kwa taaluma Mandela ni mwanasheria aliyehitimu shahada yake katika chuo kikuu cha Witwatersrand mwaka 1942 kabla hajawa mwanasiasa kwa kujiunga na ANC mwaka 1944

Kuishi maisha ya miaka 89 katika ulimwengu huu uliochanganyikwa si kitu kidogo hasa kwa mtu kama mandela aliyepitia karibu robo ya maisha yake. Kati ya misukosuko ikiwemo kuwekwa gerezani kwa miaka ipatayo 27.

Unaweza kumwita Mandela shujaa, jasiri, mapambanaji au mwanamapinduzi. Alipinga uonevu wa kila namna, alikataa ukandamizaji na aina ya maisha ya watu waliotaka kujifanya miungu wa dunia hii. Kwa nini nasema haya yote! Sikiliza mandela alivyosema mwenyewe:

Anasema “Nimepinga utawala wa watu weupe, nimepinga utawa wa watu weusi. Nimeheshimu mpango wa kidemokrasia na jamii iliyo huru ambapo watu wote wataishi pamoja kwa amani pamoja na fursa sawa. Ni mpango ambao nitaishi kwa ajili hiyo na kuufanikisha. Lakini ikibidi, basi ni mpango ambao nimejiandaa kufa kwa ajili yake”

Maneno haya ni mazito sana, Mandela aliyasema haya alipohukumiwa kifungo cha miaka mitano katika kesi fulani hivi, eti kwa kosa la uhaini, lakini uhaini uliodiwa na maadui zake ni kile kitendo cha yeye kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika ya Kusini. Hiyo ni mwaka

Kwa wale amabo wamefuatilia maisha ya harakati ya Madiba wanaweza kukubaliana na mawazo yangu kwamba Mandela hakuwa tu msemaji bali pia mtu wa vitendo, na si hivyo tu bali pia alianza kutenda kabla ya kusema, upo hapoo? Baada ya kutafakari hayo, nikajikuta nakumbuka aya fulani ya Biblia inayosema “kitabu kile cha kwanza nalikiandika, Theofilo, katika habari ya mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha” Matendo 1:1 Unaona hapo, watu wanaanza kutenda na kisha kusema au kufundisha.


Je wakoje wanasiasa wetu wa leo, unaweza kuwafananisha na Mandela? Je wanamfikia hata kwa mbali? Wangapi angalau wanatenda wanachokisema? Mandela alianza kutenda kabla hajasema, alianza kupigania uhuru wa waafrika hata kabla Afrika haijajua dhamiri yake, kabla waafrika hawajajua, kabla hatamka hadharani kuwa amejitolea maisha yake kuipigania Afrika!

Kwa nini nasema kuwa alianza kutenda kabla hajasema? Tuirejee kwanza sehemu ya kauli yake “Ni mpango ambao nitaishi kwa ajili hiyo na kuufanikisha. Lakini ikibidi, basi ni mpango ambao nimejiandaa kufa kwa ajili yake”

Angalia maisha yake kabla ya kuwekwa gerezani, alipigania uhuru wa weusi, kitu ambacho wazungu walikitafsiri kama uhaini na hivyo kumtupa lupango.

Je, alipigana kabla ya kutoa kauli hiyo gerezani?
Ndiyo, hii ni bada ya chama chake cha ANC kupigwa marufuku kuendelea kuwapo nchini Afrika ya Kusini mwaka 1960. Je Mandela akaishia hapa? Hapana, kitendo cha ANC kufungiwa kilichochea moto wa harakati za mandela kwani kwa ushawishi wake baadhi ya maodfisa wa ANC walikubali kuunda kikundi kingine cha harakati za ukombozi kilichojulikana kwa jina la Umkhonto we Sizwe kikiwa na malengo yale yale ya ANC, wao walikitafsiri kikundi hiki kama ubawa (wing) wa ANC. Kwa kitendo hicho, ilipofika mwaka 1962, Mandela alikamatwa na kuhukumiwa kifungo miaka mitano pamoja na kazi ngumu akiwa gerezani, hatia kubwa kwa mujibu wa wazungu ni kwamba, eti Mandela alikuwa akitaka kuipundua serikali yao nchini humo. Ndio maana nasema alianza kupambana kwa ajili ya ndugu zake waafrika, hata kabla hajawaambia kuwa atapambana kwa ajili yao! Tuko pamoja?

Mwaka 1964, July, 14, Mandela na wenzake walihukumiwa kifungo cha maisha. Kitendo hicho kilikuwa kama kinauamsha ulimwengu kuanza kujua hasa Mandela alikuwa nani kwa Waafrika.

Nelson Mandela aliachiwa huru februal 11, 1990 . Je aliacha kutekeleza ahadi yake kwa waafrika? Hapana kwani kwa moyo wake wote akajikita zaidi katika mapamano kama alivyokuwa ameahidi, alipigfania kutimiza ndoto zake. Ndoto gani? Alisema hivi “Nimepinga utawala wa watu weupe, nimepinga utawa wa watu weusi. Nimeheshimu mpango wa kidemokrasia na jamii iliyo huru ambapo watu wote wataishi pamoja kwa amani pamoja na fursa sawa. Ni mpango ambao nitaishi kwa ajili hiyo na kuufanikisha. Lakini ikibidi, basi ni mpango ambao nimejiandaa kufa kwa ajili yake”
Ndio maana mwaka 1991, katika kongamano la kwanza la ANC, Mandela alichaguliwa kuwa rais wa ANC huku swahiba wake Oliver Tambo akiwa Mwenyekiti.

Tangu wakati huo, Mandela hajaacha kupambana, wiki iliyopita huku akiadhimisha miaka 89 ya kuzaliwa kwake, alizindua kikundi cha viongozi mashuhuri, wazee wenye hekima duniani kikiwa na lengo la kutatua matatizo yanayoikabili dunia kwa sasa.n Kikundi hiki kikiongozwa na Mandela mwenyewe kwa kusaidiana na mkewe Graca Machel na mwenyekiti wake, Askofu mkuu mstaafu, Desmond Tutu watatumia hekima walizojaaliwa na mwenyezi Mungu kuikwamua dunia kutoka mahali pabaya ilipofika. Unaweza kuona sasa, kwamba Mandela bado anapambana.

Swali langu ni hili, je viongozi wetu wa leo watakuaje watakapofika umri huu wa Mandela? Je watakumbukwa na kuenziwa kama tunavyomuenzi mzee huyu? Mbona baadhi yao wameanza kuchokwa na watu wao, majimboni, wilayani, na kwinginekeo wakati hata miaka 60 bado? Hii ni changamoto, Mandela hajatumia uchawi, uchawi wake mkubwa ni moyo wake wa kujitoa kwa ajili ya watu wake, na wala sio kujaza matumbo tu kwa kula vya wananchi.

Nilikwambia naandika makala hii kwa heshima kubwa kabisa ya wanaharakati akiwemo binti mdogo Elizabeth David, je wao watakuwaje? Kwa mfano, Elizabeth anampend sana Mandela, basi ni vizuri akatamani pia moyo wa Mandela, ili afanikiwe na kisha kuenziwa baadae!

Nimalizie kwa kumtakia kila la heri, mzee Nelson Rolihlahla Madiba Mandela, heri yake ya siku ya kuzaliwa!