Thursday, June 28, 2007

AMINA CHIFUPA, ALINISUTA!

Amina Hamis Chifupa, kama kweli amekufa, basi na tuyakubali matokeo! Lakini kama kuna mahali kafichwa Amina, ni maombi yangu kwa Mungu kwamba siku moja utaonekana na kufa tena kwa mapenzi ya Mungu!
Umenifundisha kwamba umuonavyo mtu sivyo alivyo, na kwamba tabia za mtu huweza kubadilika, kitu kimoja nitakukumbuka ni ujasiri wako na uchungu (kama ulitoka moyoni) juu ya maisha ya vijana yanayoharibiwa na dawa za kulevya!
AMINA HAMIS CHIFUPA




Je unaweza ukafikiri ni uchungu kiasi gani mama huyu amepata, angalia anavyolia, je unapata hisia yoyote hapa? Hamisha nafsi ungekuwa wewe ndiye huyu mama hapa! fikiria kupoteza binti mbichi kama Amina. Basi huyu ni mama yake Amina Chifupa Judy Mbaga, akilia kwa namna ambayo imezidi hata ule tunaoweza kuita ni uchungu, sijui tusemeje?

Kama kweli umekufa, Buriani!

Nasema kama kweli Amina kafa, basi nasema buriani, kama nitapata nafasi kuna siku nitakuambia ni kwa nini nahisi kuwa Amina hajafa! Akili yangu inakataa kuwa Amina Kafa, hata mimi sijui kwa nini, namuona Amina, lakini sijui yuko wapi, lakini kama kweli kafa basi BURIANI!
"Siku nikilala, lala mauti, hakuna awazeae kuniamsha
Ndugu na jamaa, watalia, lakini hata hivyo sitawasikia
Utakuwa mgeni wa nani, wakati kifo kikifika?"


Hili ni shairi la muimbaji wa nyimbo za Injili Tanzania, Epharaimu Mwansasu. Ni saa nne kasoro za usiku kwa saa za Afrika Mashariki, nimekaa nyumbani napitia magazeti. Mara simu yangu inaita, siijui namba hii wala hata kuikumbuka kama nimewahi kuitumia. Naipokea na yule mtu anauliza “aisee wewe ni Daniel Gingo” Kwanza napata mashaka, kwa sababu karibu kila siku baadhi ya watu wananitabiria kudhurika eti kwa sababu ya kuandika makala zinazoishambulia serikali, lakini baadae nikajibu kuwa mimi ndie, mara anasema “Amina Chifupa hatunaye”

Nikahisi kuwa masikio yananidanganya, nikauliza “unasemaje” kama sikosei nadhani yule mtu alinijibu hivi “ndio hivyo” Sikumbuki ni saa ngapi niliacha lile gazeti nililokuwa nalo, nikainuka kukimbilia chumbani ambako ndiko iliko maktaba yangu na kufungulia redio ili kujaribu kuthibitisha kifo hicho, hali ilikuwa tata, nikajikuta naishiwa nguvu, na hivyo kukaa kitandani kwa muda mrefu kidogo bila kujua nafanya nini.

Makala yangu ya mwisho kuandika kuhusu Amina ilikuwa ni juu ya tuhuma dhidi yake kuwa alikua na uhusiano na Mbunge mwenzake, Mheshimiwa Zitto Kabwe, katika masuala ya dini, tuhuma hizo huitwa uzinzi. Niliuandikia umma kwamba tusishangae Amina kuwa na tuhuma za jinsi hiyo, maana yeye nae ni mwandamu, haukna kunyoosheana vidole, maana uzinzi ni ugonjwa wa wengi, wakiwamo mashehe na maimu, mapadri na wachungaji. Nilisema uzinzi ni dhambi inayomnyemelea kila mmoja. Ni wajibu wa kila mmoja kujilinda! Baada ya taarifa za kifo chake kesho yake nilifungua Internet kwenye blogu yangu kuisoma tena ile makala na picha iliyopamba makala ile, kuna picha ya Amina alipokuwa akiapishwa bungeni.

Kitu ninachotaka kuandika hapa siandiki kwa sababu Amina amekufa, tumeshuhudia watu wengi wakimpa sifa Amina lakini ukiwatazama usoni ni unafiki umewajaa! Ni bora kuwa kimya, kuliko kuzungumza vitu vya kinafiki. Hata hivyo tumezoea hayo. Sifa alizopewa Amina utafikiri sio yule aliyekua akindikwa kwa kashfa kila kukicha magazetini!

Ninachandika hapa ni kutaka kuonesha kwamba mimi ni mmoja wa watu ambao marehemu Amina alitusuta, siko hapa kumpamba, niko hapa kueleza ninachokijua.

Wakati anaanza harakati zake za kuwania ubunge wa viti maalumu kupitia UVCC kuliibuka mijadala mitaani, kila mtu alisema lake. Mmoja kati ya watu ambao walipinga Amina kuwania kiti hicho kwa herufi kubwa ni MIMI. Tulibishana na watu japo wengi hawakuwa na hoja za kunishawaishi kwamba kwa nini Amina anafaa. Mimi nilikataa kwanza kwa sababu ya umri wa Amina wakati ule, akiwa na umri wa miaka 24, jambo la pili na kubwa ni zile habari zake za mitaani na magazetini.

Kama alivyosema Kulwa Mzee katika gazeti la Majira la Juni 28, 2007

“Umri wako(Amina Chifupa) mwanzo uliowagopesha watu(mimi ni mmoja wao) na kuwafanya wahisi kwamba hautaweza kufanya chochote bungeni lakini ulionesha maajabu kwa kuanza kushughulikia mambo ya msingi ambayo hata hao waliokuwa wakionekana kwamba ndio walistahili kufanya hivyo hawakuweza kufanya hivyo”

Kwa wakristo tunaamini kuwa imani yoyote huja kwa kusikia, kusikia na kusoma vyombo vya habari kulinifanya nijenge imani hasi kwa Amina hasa katika suala la yeye kuwa Mbunge. Niliamini na bado naamini kuwa nafasi hiyo ni nzito na yenye kuhitaji watu makini zaidi na wanaojua wanachokifanya!

Habari za Amina zilitawala zaidi magazeti yale yanayoitwa ya Udaku, habari zingine zilikuwa na ukweli mtupu ndani yake, maana mengine yalishuhudiwa mitaani na mengine kuendelea kufikirika na kudhanika.

Hisia zangu hasi hazikumzuia Amina kupata nafasi ya ubunge, alitinga bungeni, hata hivyo kuingia kwake bungeni bado hakukunifanya nifarijike na kuamini kua anaweza.

Amina alianza kunisuta kuwa imani zanguhazikua sahihi dhidi yake, ni pale alipoanza kutoa michango bungeni, alinimaliza na kunifunga mdomo kwenye suala la madawa ya kulevya. Hapo nikaanza kujua kua hisia zangu zilikua kweli lakini si sahihi (unataka ufafanuzi hapa?)

Suala la Amina kusiamama hadharani na kesema yuko tayari kutaja majina ya wahusika wakuu wa dawa za kulevya nchini, hata kama atakuwa ni mama yake ilikua ni kauli kali ambayo ingezungumzwa na mtu jasiri na mzalendo tu! Mtu aliyekubali kujitoa mhanga! Kauli hii bei yake ni ghari mno, wengi wameshindwa wakiwamo wabunge wa miaka nenda rudi kakatika bunge la Tanzania! Kauli hii haiwezi kutolewa na wabunge maslahi waliowadanganya wananchi kuwa watawawakilisha, kwamba watakua sauti zao, halafu wakafika na kupumbazwa na viti vizuri vya jumba la bunge na hata kufikia hatua ya kusinzia wakati wa vikao vinavyojadili mustakabali wa Watanzania walioko majimboni mwao.

Kitendo cha Amina kusimama kidete ndicho kilichonisuta mimi, narudia kusema kwamba sisemi haya kwa lengo la kutubu, sifanyi hivyo kwa sababu kwa wakati ule hisia zangu zilikuwa sahihi, kwanza sikuwahi kumuana Amina akiwa Mbunge (japo hili si zito sana)


Wachambuzi wengine wamesema, Amina alijitoa mhanga kupambana na watu hatari kwani wahusika wengi wa baishara hiyo ni watu wakubwa wakiwamo pia baadhi ya vigogo na wafanya biashara wakubwa ambao wako tayari kufanya lolote kwa yeyote yule anayekwamisha biashara hiyo.
Hili ndilo ninalo sisitiza kwamba limenisuta na kujifunza kwamba usiusemee moyo, kwangu Amina ni kama Anne Kilango Malecela, ikumbukwe hivi karibuni aliijia juu serikali kwa uamuzi wake wa kuachilia baadhi ya bidhaa kupita bila kukaguliwa. Kitendo cha Anne Kilango kimenifanya nimtazame kwa upya, nimuone kama mwanamke wa shoka. Imenifundisha kwamba kumbe wako watanzania wanaoweza kusimama kidete kutetea maslahi ya nchi hii bila kutetereka!

Kumbe wako wabunge wanaoweza kusema hapana kwa yale ambayo ni maovu na madhara kwa Taifa hili.

Kama kweli amekufa basi naomboleza kifo cha Amina kama mwanadamu yeyote, imeniuma kama ilivyoniuma kw mtu mwingine angekufa. Siwezi kumpongeza kwa sasa maana hayupo tena.

Nasema kama kweli amekufa basi, Amina amelala, Amina hawezi kuamka, amelala kama tutakavyolala wengi! Mitaani tayari kumeanza kusemwa mengi! Huko sitaki kujiingiza, ukweli unabaki kuwa Amina hatunaye tena.

Binti mdogo mwenye ndoto kubwa, aliyenisuta kuwa nilivyokua nikimdhania sivyo, nilikubali na kuanza kupata matumani kuwa sasa ataweza, ndio maana tukaamini kuwa anahitaji kuungwa mkono, ukiondoa kashfa za hapa na pale!

Kama mwanadamu naweza kusema kwamba, Amina ni miongoni mwa binadamu waliopitia misukosuko mingi katika maisha, kifamilia, kisiasa na kijamii kwa ujumla.

Sina namna nyingine ya kumpamba, kwa sababu sikua karibu naye, sitaki kujikosha kwa familia yake kwa kusema yale nisiyoyajua. Amina nilikuwa nikismsikia na kumsoma tu kwenye vyombo vya habari. Kama kweli amekufa basi salamu zangu za rambirambi ni kwa wanaharakati wote wa haki na usawa, wapiga vita wote wa kila aina ya uharamia duniani, najua tumepoteza kiungo! MUNGU ATUSAIDIE WOTE!