Wednesday, November 21, 2007

Ni kweli wanatafuta vipaji au wanawadhalilisha vijan wetu?

Unaona hawa? Hawajali jua wala mvua, tena wengine hawajaaga hata makwao, wanawania gari na kurekodi bure! Angalia wale wengine wamechoooka, nani akumbuke kuwapa viti vya kupumzikia wakati shida ni yao wenyewe? Kwani walifungwa kamba kuwa ni lazima waje?
Hebu angalia hawa nao, kwa haraka haraka wako zaidi ya hamsini hapa, lakini pia wanajua kuwa anatakiwa mmoja tu kushinda, kwa kweli wengi wao wanasubiri kwenda kuambiwa hawajui kuimba bila kuambiwa ni kwa nini au ni mapungufu gani waliyonayo! mmh! Watatoka wamenuna badala ya kufikiria namna nyingine ya kutoka bila mgongo wa BenchMark! haya bwanaa!!

Huyu ni Salama jabir, ni mtangazaji wa TV na redio kule Dar es salaam! Naye ni mmoja wa majaji wa kuchagua mwanamuziki bora wa Tanzania!


Huyu ni John Kitime, meneja wa Kilimanjaro Band.

Huyu ni Joachim Kimaryo, wengi humuita Master J, yeye naye ni mmoja wa Majaji




Huyu anaitwa Rita Paulsen ni mkurugenzi wa BenchMark LTD, waandaaji wa shindano, eti naye ni jaji. Mumy usijisikie vibaya, mimi ni mwanao, natoa tu maoni yangu, nakupenda sana!







Si vibaya nikitoa utabiri wangu kinachoweza kutokea mwishoni mwa makala hii. Kwamba wako wale watakaoniona mmoja kati ya waleeee waliopitwa na wakati, siwazuii kufanya hivyo, huu ndio ulimwengu wa Utandawazi, tuliyataka wenyewe, kila mmoja anatoa lake, ndio maana huoni nguvu ikitumika sana kuzuia mmomonyoko wa maadili, yote ni utandawazi! Upoo?

Nataka kuua ndege wawili kwa wakati mmoja, naandika kuhusu kile kinachitwa ‘Big Brother Africa’ na ‘Bongo Star Search’, nianze na lipi hapa? Naanza moja kwa moja na Bongo ‘Star search’

Haya ni mashindano au Kampeni? Vyovyote lakini mwisho wa yote wahusika wanasema kuwa wanataka kumpata mwimbaji mahiri/nyota wa Bongo yaani Tanzania. Wanaalikwa watanzania weeengi, na hasa vijana, lakini mwisho wa siku anatoka mmoja. Sijui kwa wengine, lakini kwa upande wangu sikua navutiwa na kampeni hii, nilikua nikisikia tu kuwa kuna kipindi kama hicho kinachorushwa na kituo cha ITV.

Lakini jumapili iliyopita nilitaka nikae nione kinachofanyika, jinsi nyota huyo anavyosakwa, ndipo nilipojionea kile kipindi, na mwishoni kichwa changu kilijaa maswali na tafsiri nyingi sana.

Niliangalia wale vijana wanaojipitisha mbele ya wale wanaoitwa majaji (Salama Jabir, John Kitime, Rita Paulsen na Joakim Kimaryo au Master J) Kwa haraka haraka tu niseme mapema kwamba sikuwaelewa wale majaji, sikuelewa vigezo vilivyotumika kuwapa nafasi hiyo ya ujaji.
Ngoja nikuambie kwa nini nasema hivi;
Rita Paulsen yeye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni iliyoandaa shindano hilo, Benchmark Productions Ltd, hatujawahi na wala haijulikani ni wapi na lini alikuwa muimbaji/mwanamuziki kiasi cha kuwa na sifa za kuchagua wanamuziki tena nyota wa Tanzania. Kuwa bosi wa kampuni inayoandaa muziki si kuwa mwanamuziki!

Salama Jabir
Salama Jabir, yeye ni mtangazaji wa kituo cha East Africa Radio na Channel 5, ambao ni ndugu na Bench Mark, anafahamika na wengi kuwa si mwanamuziki hata ukisiliza tu sauti yake. Tuendelee! Inashangaza kama kigezo cha utangazaji kinampa sifa ya kutafuta na kumpitisha mwanauziki nyota wa Tanzania.


Master J yeye ni mtayarishaji wa muziki, si mtunzi wala muimbaji kwa anavyofahamika na wengi.
John Kitime, huyu ni mwanamuziki na meneja wa bendi ya Kilimanjaro, lakini ni jaji anayeonekana kutokua na sauti katiaka maamuzi ya shindano hili tofauti na wale wasio wanamuziki, yaani Slama, Rita na Master J.

Kwa hiyo tukiamua kuwa makini, katika shindano hilo kuna jaji mmoja tu ambaye ni kitine kwa maana ya taaluma yake.

Jambo lingine lililonisumbua ni kwamba, hata kama wangekuwa ni majaji, je, wanatumia vigezo gani kumpata mwanamuziki wanayemtafuta? Je ni unyororo wa sauti? Ujumbe katika nyimbo? Madoido ya kucheza? Au nyimbo tu wanazozipenda majaji ambazo zimewahi kuimbwa na wanamuziki wengine?

Katika suala la majaji, waandaaji wangeiga mfano wa Mamu pale kariakoo ambapo yye huwatumia wanamuziki waliokubalika zaidi kili kuzipitia na kuzijaribu kazi za wanamuziki wanaoinukia!

Hata hivyo, suala lingine ni kwamba waandaaji wa shindano hilo nao wanaumwa ule ugonjwa wa kuendekeza utamaduni wa nje hasa suala la lugha, wanajua fika kuwa wanamtafuta mwanauziki nguli wa Tanzania, na sio Marekani wala Hispania, lakini ajabu ni kwamba mpaka jina la shindano ni la kizungu, ndilo linalotumika kutangaza kwenye vyombo vya habari, kuna ubaya gani kuliita shindano hilo, SHINDANO LA KUMSAKA au KUMTAFUTA MWANAMUZIKI NYOTA WA TANZANIA? Hata kama ni refu, lakini si ndio lugha yenu? ukiangalia majaji wamekuwa mahodari kwenye kushangilia nyimbo za magharibi, za kizungu, kwa hiyo kama vizazi baadae vitakuja kusaka na kuhumu wahumu wa utamaduni wa Tanzania hususani kwenye lugha, BENCHMARK LTD hawawezi kukwepa hukumu hiyo!

Kwa taarifa tu ni kwamba huo ulikuwa ni utangulizi wa makala hii kuhusu Bongo Star Search! Shindano lisilo na vigezo!

Lakini binafsi nimejifunza kwa watanzania wenzangu hasa vijana, na nimegundua na kuendelea kujua kwamba dezo au vya bure vitaendelea kutumaliza tusipo kubali kugeuka. Maradhi ya kupenda dezo ni mardhi yaliyolikumba hata Taifa letu, kuendelea kutegemea hisaniza Wazungu katika kujenga uchumi wetu, wakati tuna mbuga, mito, bahari, milima na wataalamu mbalimbali.

Nina maana gain? Wengi walioenda kujipitsha mbele ya majaji ili kuchaguliwa wana uwezo mkubwa wa kufanya mazoezi yao ma kuja kuibuka kuwa waimbaji mahiri bila hata ya kupitia BenchMark, na hivyo kuepuka na kukwepa udhalilishaji wanaofanyiwa na majaji na ule wanaojifanyia wenyewe. Aliyekaa kwa makini na kufuatilia kipindi kile atagundua kuwa uamsikini au unyonge na dezo ndio iliyowapeleka wengi pale leaders club ili kubahatika kuchaguliwa! Masikini vijana watanzania, wanaenda pale na kukutana na watu kama Salama jabir ambaye haangalii kama wewe una wadogo zake kama yeye, au umemzidi kwa namna moja ama nyingine na kukujibu hovyo! Nimeona vijana wengi wakidhalilishwa bila wao kushituka, lakini siwalaumu ni kuna nadharia kadhaa hapa, kwanza umasikini au dezo na kutaka umaarufu wa haraka!

Wanachokimbilia wengi ni kupata mkataba wa kurekodi albamu zao bure, pesa (kama zipo) na gari la bure! Sielewi kwa nini wasikubali kuwa masikini jeuri, kwamba kama mtu ameamua kukusaidie hebu na afanye hivyo bila kukusimanga na kukudhalilisha, vinginevyo tafuta kutoka kivyako!

Ninayo mifano ya wanamuziki kama Ephraim Mwansasu, faustine Munishi, Neema Mushi, Bahati Bukuku, David Nyanda, Sipho Makabane, Jabu na wengineo wa ndani na nje ya nchi ambao walisota sana kaba ya kutoka! Matokeo ya kutegemea mashindano kama haya ambako utaambiwa hujui kuimba wakati unajua ni kujichelewesha mwenyewe na kwenda kuvunjika moyo na kuacha kuchochea kipawa chako! Si ajabu kwamba hata wale amabo wamepitishwa na watu wengine si waimbaji ka wewe uliyekatishwa tama kwa kuambiwa na Master J au Salama, au Rita kuwa hujui kuimba!

Nakumbuka wakati nilipokuwa nataka kufikisha makala zangu magazetini waliponiambia kuwa sijui kuandika, niliamua kuandika kwenye madaftari ya shuleni na kuyahifadhi, kasha nikiwa kidato cha sita nikaomba walimu waniruhusu nianzishe kagazeti kangu, humo nikawa naandika mawazo yangu na kufikisha kwa wanafunzi wenzangu, mara nyingine niliwahi kufika shule mapema na kuweka ujumbe wangu kwenye ubao wa darasani, ni mpaka mwalimu alipofika ubao ulifutwa! Sasa ninaweka maandishi yangu kwenye blogu, tembelea www.amkenitwende.blogspot.com , sisahau pia kwamba niliambiwa na wazazi wangu kuwa sina sauti nzuri ya kuimba, sikukubali, nikaacha kuimba mbele za watu, nikawa naingiza sauti kwenye kaseti, mpaka watu Fulani waliponiona na kutaka nikarekodi nao, hata hivyo mambo hayajakwenda sawa, masomo yamenibana, lakini nitarekodi, sasa naandika nyimbo na nawapa wengine wanazitumia! Sikukubali!

Kama moto wa kuimba unawaka ndani endelea kuimba, wakati unaoga au wakati unavaa suruali au sketi yako chumbani, imba usiogope, imba sio mpaka Salama Jabir au Master J akuone, sio mpaka BenchMark wakuone!

Usikubali watu watumie kukosa kwako pesa ya kurekodi wakudhalilishe, na usikubali kudhalilika, kuna njia nyingi za kutoka kimuziki, muweke Mungu mbele, enzi za kina Munishi, Mzungu Four, Patrick Balisidya, Msanii Kyande, Charles Jangalason hakukuwa na BenchMark LTD na bado walitoka!
Itaendelea wiki ijayo!