Wednesday, May 30, 2007

HIMA WATANZANIA, AMKENI KUMEKUCHA!


Hapa Rais Kikwete akiomba kura kwa Watanzania!





Hawa si unawajua? - >
Kuna msemo wa wazungu unasema ‘information is power’ Kwa Kiswahili rahisi kabisa tungeweza kutafsiri msomo huo kama, taarifa ni nguvu. Mtu mwenye taarifa nyingi au kidogo hawezi kufanana kamwe na yule ambaye hana taarifa na wala hapendi kusoma kwa lengo la
kujihabarisha.
Nimebahatika kusoma baadhi ya magazeti, napenda sana kusoma magazeti, na sio kwa lengo la kujipa burudani bali kujihabarisha ili kupata taarifa.

Pengine kwa mara ya kwanza kwa upande wangu wiki iliyopita nilisoma magazeti mawili tofauti yenye makala zinazofanana kana kwamba waandishi wake walipanga kuandika ujumbe unaofanana.

Magazeti hayo ni Mwananchi na Tanzania Daima, kwenye Tanzania Daima nilikuta tahariri moja na makala tisa za waandishi tofauti. Pamoja na utofauti huo wa waandishi wake na vichwa vya makala zote hizo, ukisoma kwa makini utagundua kuwa zote zina ujumbwe mmoja! Hii ni kwa mtazamo wangu.

Jaribu kupitia magazeti hayo ambayo ni Tanzania Daima toleo namba 908, Mei 30, 2007 na Mwananchi namba 02543 la siku hiyo hiyo, pengine utagundua kitu nilichogundua mimi. Katika kupembua makala hizo, mwenzenu nimegundua kuwa ujumbe wa makala zote nimeupa jina la UKOMBOZI WA MTANZANIA!

Sio siri makala hizo zimenitia moyo sana, kupitia makala hizo nimejifunza kwamba kuna mambo mawili au matatu yanatokea kwa pamoja hapa nchi sasa hivi!

Mosi; watanzania tumeanza au tayari tumegundua jinsi hali ya hewa ya nchi hii inavyokwenda, tumeanza kuelewa nini kinafanyika nyuma ya pazia la Taifa letu, na hasa katika suala zima la siasa na utawala. Inatia moyo kwamba yale ambayo tulidhani kuwa hayapo, yapo. Na yale ambayo wahusika walidhani kuwa watanzania hawayajui na hata kuhakikisha kuwa wanayaficha yanakuwa siri, ukweli ni kwamba hakuna siri tena. Nasema watanzania wamenaza kung’amua mambo.

Je unataka kuamini kuwa sasa tunaanza kuujua ukweli, msome Absalomu Kibanda katika makala yake ya wiki iliyopita, anasema hivi
“…Leo hii najiona mwenye bahati kulitambua hilo na kufahamu namna majemadari hawa wa CCM walivyo tayari kucheza rafu za kila aina kuwanyonga wapinzani wao wa kisiasa…..”

Huyu ni mhariri wa gazeti la Tanzania Daima, hapa najiuliza swali, je ni wahariri wangapi leo wanaweza kusimama kwa uajsiri kusema aliyoyasema Kibanda katika makala yake ile? (tafadhali kaipitie) Je ni wahariri wangapi wamegundua yale aliyoyagundua Kibanda?

Msome pia Elias Msuya aliyeandika kwenye gazeti la Mwananchi ukurasa wa 12 siku hiyo, yeye anasema

“Na kwakuwa watawala wanaujua udhaifu wetu, basi wanaamua kuwekeza kwenye biashara hii. Chama tawala sasa kimekuwa maficho ya matajiri na mafisadi. Walio walafi wanajitolea kufadhali chama ili walindwe, hawa wanaangalia maslahi yao kulik yale ya nchi”

Unaweza kuona kuwa. Elias naye amegundua ukweli wa mambo ulivyo katika chama tawala, chama kilichpewa dhamana ya kuliongoza Taifa hili. Hakuishia hapa, Elias pia amegundua kwa upande mwingine kuwa Watanzania na sisi tuna tatizo, huu ni ugunduzi na utambuzi mzuri sana, anasema

“….Je ni kweli hali ya maisha yetu zinaboreka hata tushawishike kukipa ushindi wa kishindo chama tawala kila tunapoingia kwenye uchaguzi? Je wapiga kura wetu wanaelewa wakifanyacho? Au kwa kapelo na fulana zinatosha kuwazubaisha kwamba kweli dhamira ya chama tawala ni maisha bora kwa kila Mtanzania. Je hivi Watanzania ni mambumbu wa kiasi gain? Je ni kwa nini waendelee kuruhusu wanaisasa wachezee akili, hisia zao na maisha yao kila mara?”

Huyo ni Elias Msuya. Nimewahi kusema mara nyingi, nab ado nasisitiza kuwa kwa sehemu watanzania tunashiriki kulihujumu taifa hili, ikiwa ni pamoja na kuwapa kura viongozi wasiostahili, kwa kudanganywa na maji ya uhai ya shilingi miatano, doti za kanga, kofia na mafulana, haya ambayo baadae yanatugharimu kwa miaka mitano au kumi. Watanzani tuna kasumba ya kurudirudia makosa tuliyofanya awali. Hili ni tatizo la viongozi wetu pia, kwamwe baadhi yao hawajifunzi kutokana na makosa.

Katika mfululizo huo, kana kwamba waliambiana, Boniface Makene naye anagundua jambo, anasema;

“Chama hiki kwa sasa kina kundi kubwa la wanachama wasio kifahamu vema. Wengi wa hawa ni wafanya biashara na kundi jingine linasaka madaraka”

Makene anaongeza kusema;

“Kuingia kwa awamu ya nne kunaambatana na kuibadili CCM kuwa chama cha wafanya biashara na wawekezaji”

Bila shaka Makene anafahamu vema madhara ya chama cha siasa na hasa kile kilichopewa dhamana kuongoza nchi kuhodhiwa na wafanya biashara!`

Pili; baada ya watanzania kuanza kung’amua ukweli wa mambo, sasa inaonekana dhahiri kuwa wamechoka, nasema tena kuwa wamechoka! Wamechoka visa, dhuluma, ulafi na uroho wa wachache. Wamechoka kufanywa wajinga na watoto wadogo, siasa za maneno matupu yaisyojenga nchi, wamechoka kila aina ya vituko vya baadhi ya watawala na wanasiasa. Kauli zao zinathibitisha haya;

Angalia Kristofa Kidanka anavyosema hapa;

“Mengi yalitufanya tunyamaze, mojawapo ni kuwa rais Kikwete alisema Uingereza bado wanachunguza kwa kina suala hilo (rada) na kwamba tutadai ‘chenji’ yetu iliyozidi katika ununuzi ule……Tunataka maelezo kutoka kwa mzee Mkapa, na katika hili tunamuomba Rais Kikwete akae pembeni. Asimkingie kifua. Tunataka atueleze japo kifupi sana, kwa nini alitumia muda aliokuwa Ikulu kufanya biashara”

Hivi unapata somo hapa wewe? M.M.Mwanakijiji naye hakubaki nyuma, utadhani wameambiana na Kidanka, Mwanakijiji ansema;

“Kwa bahati nzuri (mbaya kwa serikali) nyakati za kunyamazisha watu kuhoji matendo ya serikali zimepitwa na wakati wa wa wananchi kuona aibu kuwaambia viongozi wetu ukweli umekwisha. Tutawaambia hata kama hawapendi kuusikia na kwa hakika tutapaza sauti zetu zaidi ili hata waliotia pamba masikioni mwao na watusikie”

Watu kama M.M.Mwanakijiji ni picha halisi ya watanzania wengi wasio na sauti za kusema “TUMECHOKA”
Hivi unaweza ukathubutu kusema hawa watu walipanga kwa pamoja waandike ujumbe mmoja siku hiyo, tena kwenye magazeti tofauti? Kama sivyo, unapata picha au somo gain hapa? Ni rahisi, ni kwamba, watu wameanza kugundua ukweli, maana ukweli haufichiki, ukweli haufi, hata ungeamua kuuzamisha ndani ya bahari ya Hindi pale Dar es salaam, kuna siku utapata taarifa kuwa umetokea kwenye bahari hiyo hiyo ya Hindi kule Tanga au Mbombasa. Omba tu asiwepo anayependa ukweli akauona, maana kwa hakika ataufuata, kuuchukua na kuutumia.

Niliwahi kusema kuwa nchi hii inahitaji mapinduzi, nilisema mapinduzi haya hayahitaji mitutu ya bunduki wala mabomu, hayahitaji mizinga wala mapanga, hayahitaji lugha za matusi.

Ndugu zangu, nasema pengine tunahitaji kidogo sana nacho ni mapinduzi ya kifikra. Fikra zetu kubadilika, zisafishwe upya, ziyeyushwe, maana zimeganda. Wansiasa na hasa wale watawala wamechangia kugandisha fikra zetu. Kugundua tatizo ni hatua moja kubwa sana kwa ajili ya utatuzi wa tatizo hilo.

Ushauri mdogo ninaoweza kukupatia hapa jinsi ya kubadilisha na kusafisha fikra ni kupenda kujihabarisha juu ya masuala mbalimbali yanayolihusu Taifa lako. Anza kupenda kusoma magazeti yanayokujengea moyo wa uzalendo, kuwa mfuatilialiaji wan chi jinsi inavyokwenda. Nunua katiba ya nchi yako, humo utaelewa haki na wajibu uliona kwenye taifa hili.

Kupitia Katiba utajua nini cha kuhoji kuanzia kwa mjumbe wako wa nyumba kumi mpaka rais wako. Kwa mfano kifungu cha 18 (2) kinasema “Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii”

Soma kifungu hicho kisha linganisha na taarifa za vyombo vya habari kuhusu mikataba ambayo nchi hii inaingia na wawekezaji wa nje

Acha kusoma magazeti yanayonajisi fikra zako, huu si wakati wa anasa na burudani zilizokithiri, huu ni wakati wa kujenga nchi hii.

Acha kuharibu fikra yako kwa kutazama na kusikiliza vipindi vinavyokupumbaza na kusahau wajibu wako kwa Taifa hili. Sikatazi watu kutazama wakina Rebecca na Kamila, isipokuwa nakumbusha tu kuwa wale jamaa walishajenga nchi zao, hatufanani nao kabisa. Mtu mmoja akaniambia kuwa wenzetu wametupita miaka 400 mbele!

Wewe unayekwenda kwenye Internet, usilihujumu Tiafa lako kwa kuangalia na kusoma vitu vinavyo najisi fikra zako. Nchi inahitaji watu makini ikiwa ni pamoja na wale wanaopenda kujihabarisha, kwa sababu “information is Power”