Sunday, December 2, 2007

Tanzania ilipata uhuru lini na kutoka kwa nani?

“Mnamo tarehe 30/06/07 kamati kuu ya utendaji ya Tanzania Association ilikuwa na kikao katika ofisi zake za muda zilizopo huko Tottenham London.Kati ya mengi yaliyojadiliwa ilikuwa ni kuadhimishwa kwa siku ya uhuru wa Tanzania na watanzania waishio hapa UK”

Hiki ni kipande cha taarifa ya Jumuiya ya Watanzania waishio nchini Uingereza kwenye mtandao. Angali kwa makini lile neno nililolikoleza kwa wino mweusi. Nilishtuka, nikajua kwa vyovyote kuna watanzania wengi wanaweza kuwa wanafikiri hivyo, kwamba Tanzania inasheherekea uhuru wake. Na hapa napenda ifahamike tu natoa maoni yangu ikiwa ni moja kati ya kusheherekea siku hiyo ya uhuru!

Siko hapa kuwabeza wala kuwadharau wale wenye mawazo kwamba Tanzania inasheherekea siku ya kupata uhuru! Kukaa kimya kunaweza kuchangia kuendelea kupotoshwa kwa historia, kwa hivyo kwa kutumia hekima, uungwana na busara ni vizuri tukakumbushana yale yaliyo ya muhimu kwa ajili ya historia ya nchi yetu.

Swali linaanza hivi, Je, ni kweli tunasheherekea uhuru wa Tanzania? Kuna ukweli hapo kihistoria? Ili kulijibu swali hili hebu tuanagalie maana ya Tanzania.

Tanzania ni muunganiko wa majina mawili ya zilizokuwa nchi mbili, yaani Tanganyika na Zanzibar. Nchi hizi mbili ziliungana mwaka 1964 na kuunda Jamhuri ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo baadae ikaitwa Tanzania. Ikumbukwe pia kwamba, kabla nchi hizo hazijawa nchi moja Tayari Tanganyika iliyokuwa koloni la Mwingereza ilikuwa tayari imepata uhuru wake mwaka 1961, miaka miatatu kabla ya muungano huo.
Kwa hiyo wakati Tanganyika inapata Uhuru, nchi au kitu kinachitwa Tanzania hakikuwepo/haikuwepo. Zanzibar yenyewe ilikuja kupata uhuru wake kutoka kwa Sultani mwaka 1964 kwa njia ya mapinduzi. Kwa hiyo siku za uhuru wa Tanganyika kama nchi, na Zanzibar kama nchi pia ni tofauti. Kwa kusheherekea, Tanganyika ina siku yake ya uhuru na Zanzibar vivyo hivyo.
Kwa huoni kuwa kuna walakini kusheherekea uhuru wa Tanzania ambayo haijawahi kutawaliwa? Unapozungmzia Tanzania unazungumzia Tanganyika na Zanzibar, kwa nini tusheherekee uhuru wa nchi mbili tofauti, zilizopata uhuru kwa miaka na tarehe tofauti kabisa.
Sisemi haya kwa nia mbaya, ni kwa ajili ya wale wanaodhani tunasheherekea uhuru wa Tanzania. Hebu soma hii nayo hapa;
“Kuelekea maadhimisho ya miaka 47 ya Uhuru wa Tanzania Bara na 46 ya Jamhuri nimepata wazo. Angalia yale maneno yaliyokolezwa. Ni wakati wa kuiinua bendera yetu juu kama ishara ya umoja wetu na kama ishara ya utaifa wetu”
Huyu ni mchambuzi mahiri wa masuala ya kijamii hapa nchini, yeye anaishi nchini Marekani kwa sasa, anaitwa M. M. Mwanakijiji. Yeye kasema wazi kuwa ni uhuru wa Tanzania Bara, ni bora. Lakini hata hivyo kuna nchi inaitwa Tanzania Bara? Hili tuliache, tutalijadili wakati mwingine tukijaaliwa.
Kuna wakati niliwahi kusoma uachambuzi wa mwandishi fulani akihoji kwa nini historia ya Zanzibari inapotoshwa kuhusu mapinduzi, nadhani pia naanza kuona kuwa kuna mambo tukikaa kimya bila kuruhusu mijadala yenye kujenga tutaipoteza historia halisi na maana ya uhuru tulioupata.
Mwaka jana niliwahi kuhoji kwa habari hii ya Tanzania kuwa na sherehe za uhuru, lakini sikuzama kwa undani hivi, lengolisema hivi “Hivi ni uhuru wa Tanganyika au Tanzania ? Kwani Tanzania iliwahi kutawaliwa na nchi gain. Eti kwa mujibu wa walimu wang wa historian a kumbukumbu zangu, Tanganyika (si Tanzania ) ndio iliyopata uhuru mwaka 1961. Ni haki yangu kuhoji swali hili, ni muhimu, historia isipotoshwe. Naomba mhariri aruhusu mjadala katika hili. Kwa nini tusheherekee uhuru wa Tanzania badala ya Tanganyika ?” kama nilivyokwisha kusema kabla ni kuibua mjadala ili tuone kama tuko mahali sahihi au tumejisahau.
Bado swali langu liko pale pale, Tanzania kwa maana ya nchi, ilipata lini uhuru? Ilitawaliwa na nani? Kwa nini navyofahamu mwaka 1961, Tanzania ilikuwa haijazaliwa bado, kwa wale wanaotumia neno Uhuru wa Tanzania waache kufanya hivyo, kwani ni kupotosha historia, Tanzania haijawahi kuwa Koloni, Yaani tangu Tanganyika na Zanzibar ziungane na kuwa nchi moja, nchi hiyo (Tanzania) baada ya mwaka 1964 haijawahi kuwa chini ya Ukoloni.

Pengine kama tuna maana ya ukoloni wa kimawazo (kifkra) na kiuchumi, kwamba bado tunatawaliwa kiuchumi na kifikra na mataifa ya Magharibi. Ndio maana tunaendekeza hadi lugha yao na kuona kiswahili ni takataka na laana kwetu. Ndio maana asilimia 40% ya bajeti yetu tunategemea kutoka kwao. Hata kama ndivyo, kwamba tunatawaliwa kiuchumi na kifikra je uhuru tumeupata? Lini, tarehe ngapi?

Lakini pia hivi hamfikirii kwamba kuendelea kusheherekea uhuru wa Tanganyika ni kuendelea kuitambua Tanganyika? Wana makosa gani sasa wakina Mtikila wanapojinadi kuwa wao si watanzania, bali watanganyika? Kwa nini tusisheherekee tu uhuru wa Tanzania kama upo au tubakie tu na sherehe za Muungano ambao nao una mkanganyiko?

Chonde ndugu zanguni, popote mlipo,lengo langu ni kuwakumbusha wale wanaopenda kutumia neno uhuru wa Tanzania badala ya Tanganyika, na tena nimesema kwamba kama tunasheherekea uhuru wa Tanganyika ina maana kwamba tunakiri na kuungana na kina Mtikila kwamba bado kuna nchi inaitwa Tanganyika, je Katiba inasemaje? Je tuna katiba ya Tanganyika bado? Siku moja nitaleta uchambuzi kuhusu suala la Muungano, ili ujue kwamba kuna mambo mengi bado tunayafanya lakini huku tukiwa hatuelewi bado maana yake au yakiendelea kutuchanganya! Lazima tufanye haraka kurekebisha ili vizazi vijavyo visije vikatuhukumu.

Wednesday, November 21, 2007

Ni kweli wanatafuta vipaji au wanawadhalilisha vijan wetu?

Unaona hawa? Hawajali jua wala mvua, tena wengine hawajaaga hata makwao, wanawania gari na kurekodi bure! Angalia wale wengine wamechoooka, nani akumbuke kuwapa viti vya kupumzikia wakati shida ni yao wenyewe? Kwani walifungwa kamba kuwa ni lazima waje?
Hebu angalia hawa nao, kwa haraka haraka wako zaidi ya hamsini hapa, lakini pia wanajua kuwa anatakiwa mmoja tu kushinda, kwa kweli wengi wao wanasubiri kwenda kuambiwa hawajui kuimba bila kuambiwa ni kwa nini au ni mapungufu gani waliyonayo! mmh! Watatoka wamenuna badala ya kufikiria namna nyingine ya kutoka bila mgongo wa BenchMark! haya bwanaa!!

Huyu ni Salama jabir, ni mtangazaji wa TV na redio kule Dar es salaam! Naye ni mmoja wa majaji wa kuchagua mwanamuziki bora wa Tanzania!


Huyu ni John Kitime, meneja wa Kilimanjaro Band.

Huyu ni Joachim Kimaryo, wengi humuita Master J, yeye naye ni mmoja wa Majaji




Huyu anaitwa Rita Paulsen ni mkurugenzi wa BenchMark LTD, waandaaji wa shindano, eti naye ni jaji. Mumy usijisikie vibaya, mimi ni mwanao, natoa tu maoni yangu, nakupenda sana!







Si vibaya nikitoa utabiri wangu kinachoweza kutokea mwishoni mwa makala hii. Kwamba wako wale watakaoniona mmoja kati ya waleeee waliopitwa na wakati, siwazuii kufanya hivyo, huu ndio ulimwengu wa Utandawazi, tuliyataka wenyewe, kila mmoja anatoa lake, ndio maana huoni nguvu ikitumika sana kuzuia mmomonyoko wa maadili, yote ni utandawazi! Upoo?

Nataka kuua ndege wawili kwa wakati mmoja, naandika kuhusu kile kinachitwa ‘Big Brother Africa’ na ‘Bongo Star Search’, nianze na lipi hapa? Naanza moja kwa moja na Bongo ‘Star search’

Haya ni mashindano au Kampeni? Vyovyote lakini mwisho wa yote wahusika wanasema kuwa wanataka kumpata mwimbaji mahiri/nyota wa Bongo yaani Tanzania. Wanaalikwa watanzania weeengi, na hasa vijana, lakini mwisho wa siku anatoka mmoja. Sijui kwa wengine, lakini kwa upande wangu sikua navutiwa na kampeni hii, nilikua nikisikia tu kuwa kuna kipindi kama hicho kinachorushwa na kituo cha ITV.

Lakini jumapili iliyopita nilitaka nikae nione kinachofanyika, jinsi nyota huyo anavyosakwa, ndipo nilipojionea kile kipindi, na mwishoni kichwa changu kilijaa maswali na tafsiri nyingi sana.

Niliangalia wale vijana wanaojipitisha mbele ya wale wanaoitwa majaji (Salama Jabir, John Kitime, Rita Paulsen na Joakim Kimaryo au Master J) Kwa haraka haraka tu niseme mapema kwamba sikuwaelewa wale majaji, sikuelewa vigezo vilivyotumika kuwapa nafasi hiyo ya ujaji.
Ngoja nikuambie kwa nini nasema hivi;
Rita Paulsen yeye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni iliyoandaa shindano hilo, Benchmark Productions Ltd, hatujawahi na wala haijulikani ni wapi na lini alikuwa muimbaji/mwanamuziki kiasi cha kuwa na sifa za kuchagua wanamuziki tena nyota wa Tanzania. Kuwa bosi wa kampuni inayoandaa muziki si kuwa mwanamuziki!

Salama Jabir
Salama Jabir, yeye ni mtangazaji wa kituo cha East Africa Radio na Channel 5, ambao ni ndugu na Bench Mark, anafahamika na wengi kuwa si mwanamuziki hata ukisiliza tu sauti yake. Tuendelee! Inashangaza kama kigezo cha utangazaji kinampa sifa ya kutafuta na kumpitisha mwanauziki nyota wa Tanzania.


Master J yeye ni mtayarishaji wa muziki, si mtunzi wala muimbaji kwa anavyofahamika na wengi.
John Kitime, huyu ni mwanamuziki na meneja wa bendi ya Kilimanjaro, lakini ni jaji anayeonekana kutokua na sauti katiaka maamuzi ya shindano hili tofauti na wale wasio wanamuziki, yaani Slama, Rita na Master J.

Kwa hiyo tukiamua kuwa makini, katika shindano hilo kuna jaji mmoja tu ambaye ni kitine kwa maana ya taaluma yake.

Jambo lingine lililonisumbua ni kwamba, hata kama wangekuwa ni majaji, je, wanatumia vigezo gani kumpata mwanamuziki wanayemtafuta? Je ni unyororo wa sauti? Ujumbe katika nyimbo? Madoido ya kucheza? Au nyimbo tu wanazozipenda majaji ambazo zimewahi kuimbwa na wanamuziki wengine?

Katika suala la majaji, waandaaji wangeiga mfano wa Mamu pale kariakoo ambapo yye huwatumia wanamuziki waliokubalika zaidi kili kuzipitia na kuzijaribu kazi za wanamuziki wanaoinukia!

Hata hivyo, suala lingine ni kwamba waandaaji wa shindano hilo nao wanaumwa ule ugonjwa wa kuendekeza utamaduni wa nje hasa suala la lugha, wanajua fika kuwa wanamtafuta mwanauziki nguli wa Tanzania, na sio Marekani wala Hispania, lakini ajabu ni kwamba mpaka jina la shindano ni la kizungu, ndilo linalotumika kutangaza kwenye vyombo vya habari, kuna ubaya gani kuliita shindano hilo, SHINDANO LA KUMSAKA au KUMTAFUTA MWANAMUZIKI NYOTA WA TANZANIA? Hata kama ni refu, lakini si ndio lugha yenu? ukiangalia majaji wamekuwa mahodari kwenye kushangilia nyimbo za magharibi, za kizungu, kwa hiyo kama vizazi baadae vitakuja kusaka na kuhumu wahumu wa utamaduni wa Tanzania hususani kwenye lugha, BENCHMARK LTD hawawezi kukwepa hukumu hiyo!

Kwa taarifa tu ni kwamba huo ulikuwa ni utangulizi wa makala hii kuhusu Bongo Star Search! Shindano lisilo na vigezo!

Lakini binafsi nimejifunza kwa watanzania wenzangu hasa vijana, na nimegundua na kuendelea kujua kwamba dezo au vya bure vitaendelea kutumaliza tusipo kubali kugeuka. Maradhi ya kupenda dezo ni mardhi yaliyolikumba hata Taifa letu, kuendelea kutegemea hisaniza Wazungu katika kujenga uchumi wetu, wakati tuna mbuga, mito, bahari, milima na wataalamu mbalimbali.

Nina maana gain? Wengi walioenda kujipitsha mbele ya majaji ili kuchaguliwa wana uwezo mkubwa wa kufanya mazoezi yao ma kuja kuibuka kuwa waimbaji mahiri bila hata ya kupitia BenchMark, na hivyo kuepuka na kukwepa udhalilishaji wanaofanyiwa na majaji na ule wanaojifanyia wenyewe. Aliyekaa kwa makini na kufuatilia kipindi kile atagundua kuwa uamsikini au unyonge na dezo ndio iliyowapeleka wengi pale leaders club ili kubahatika kuchaguliwa! Masikini vijana watanzania, wanaenda pale na kukutana na watu kama Salama jabir ambaye haangalii kama wewe una wadogo zake kama yeye, au umemzidi kwa namna moja ama nyingine na kukujibu hovyo! Nimeona vijana wengi wakidhalilishwa bila wao kushituka, lakini siwalaumu ni kuna nadharia kadhaa hapa, kwanza umasikini au dezo na kutaka umaarufu wa haraka!

Wanachokimbilia wengi ni kupata mkataba wa kurekodi albamu zao bure, pesa (kama zipo) na gari la bure! Sielewi kwa nini wasikubali kuwa masikini jeuri, kwamba kama mtu ameamua kukusaidie hebu na afanye hivyo bila kukusimanga na kukudhalilisha, vinginevyo tafuta kutoka kivyako!

Ninayo mifano ya wanamuziki kama Ephraim Mwansasu, faustine Munishi, Neema Mushi, Bahati Bukuku, David Nyanda, Sipho Makabane, Jabu na wengineo wa ndani na nje ya nchi ambao walisota sana kaba ya kutoka! Matokeo ya kutegemea mashindano kama haya ambako utaambiwa hujui kuimba wakati unajua ni kujichelewesha mwenyewe na kwenda kuvunjika moyo na kuacha kuchochea kipawa chako! Si ajabu kwamba hata wale amabo wamepitishwa na watu wengine si waimbaji ka wewe uliyekatishwa tama kwa kuambiwa na Master J au Salama, au Rita kuwa hujui kuimba!

Nakumbuka wakati nilipokuwa nataka kufikisha makala zangu magazetini waliponiambia kuwa sijui kuandika, niliamua kuandika kwenye madaftari ya shuleni na kuyahifadhi, kasha nikiwa kidato cha sita nikaomba walimu waniruhusu nianzishe kagazeti kangu, humo nikawa naandika mawazo yangu na kufikisha kwa wanafunzi wenzangu, mara nyingine niliwahi kufika shule mapema na kuweka ujumbe wangu kwenye ubao wa darasani, ni mpaka mwalimu alipofika ubao ulifutwa! Sasa ninaweka maandishi yangu kwenye blogu, tembelea www.amkenitwende.blogspot.com , sisahau pia kwamba niliambiwa na wazazi wangu kuwa sina sauti nzuri ya kuimba, sikukubali, nikaacha kuimba mbele za watu, nikawa naingiza sauti kwenye kaseti, mpaka watu Fulani waliponiona na kutaka nikarekodi nao, hata hivyo mambo hayajakwenda sawa, masomo yamenibana, lakini nitarekodi, sasa naandika nyimbo na nawapa wengine wanazitumia! Sikukubali!

Kama moto wa kuimba unawaka ndani endelea kuimba, wakati unaoga au wakati unavaa suruali au sketi yako chumbani, imba usiogope, imba sio mpaka Salama Jabir au Master J akuone, sio mpaka BenchMark wakuone!

Usikubali watu watumie kukosa kwako pesa ya kurekodi wakudhalilishe, na usikubali kudhalilika, kuna njia nyingi za kutoka kimuziki, muweke Mungu mbele, enzi za kina Munishi, Mzungu Four, Patrick Balisidya, Msanii Kyande, Charles Jangalason hakukuwa na BenchMark LTD na bado walitoka!
Itaendelea wiki ijayo!

Sunday, November 18, 2007

Fumbo, kitendawili na hadithi pamoja?


Mheshimiwa Zitto Kabwe

Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kuunda tume ya kuchunguza suala zima la mikataba ya madini nchini, na napenda ifahamike kuwa pongezi hizi ni za dhati kwa maana ya kutoka moyoni, tena kule kilindini. Pongezi hizi ni kwa sababu mbili.

Kwanza ni kwa sababu ya rais kutimiza ahadi aliyoahidi hivi karibuni katika mkutano mkuu wa CCM pale Dodoma , aliahidi kufanya hivyo, naam amefanya tena kwa muda mfupi sana , ametimiza ahadi.

Lakini la pili lililokubwa zaidi ni kwa vile rais anaelekea kupona ule ugunjwa wa siku nyingi wa serikali ya CCM kufanya mambo kwa kuzingatia maslahi ya chama zaidi kuliko Taifa, uginjwa wa kudhani wapinzani hawawezi kutoa mchango wowote kwa serikali iliyoko madarakani zaidi ya kupiga kelele za majukwaani na kupoteza muda, hiyo ndio ilikuwa pengine ni dhana ya CCM na serikali kwa ujumla.

Lakini Kikwete ananishawishi nianze kuamini kuwa CCM ( kama si dhamira binafsi ya Kikwete) inaelekea kupona uginjwa huu, ni pale alipoamua kuunda tume inayojumuisha viongozi wa CCM na wale wa upinzani wakiwamo John Momose Cheyo wa UDP na Zito Zuberi Kabwe wa CHADEMA. Kwa moyo mkunjufu nasema hongera sana Mheshimiwa rais na asante !

Hata hivyo mwishoni mwa makala hii nitakutaka mpendwa msomaji wangu uamue/upembue uteuzi huu, ikiwa ni fumbo, kitendawili au hadithi kwa maana ya historia mpya ambayo vizazi vitasimuliwa hapo baadae?

Tume hii imekuwa gumzo mitaani na hasa kwa wafuatiliaji wa masuala mbalimbali hapa nchini, na aliyesababisha gumzo hilo si mwingine ni Zitto Kabwe, suala sio tume, suala ni Kabwe kuwa kwenye tume hiyo. Wakati gumzo hilo likiwa bado bichi, gazeti moja likaripoti kuwa baadhi ya wanachama wa CHADEMA wamanza kumjadili Kabwe, kwamba inakuwaje awe kwenye tume hiyo na mambo mengine mengi ambayo nimeyatafsiri kama ya kitoto kama sio propaganda za baadhi ya maadui wa Zitto Kabwe kupitia magazeti hayo. Suala la Zitto kabwe kuwa kwenye tume hiyo siyo suala la kiitikadi, ni swala la kitaifa.

Mimi sijui kwa upande wako unafikiriaje, wenzako wanasema Zitto Kabwe ana ajenda ya siri na CCM, kwamba ananunuliwa ili kuzibwa midomo, mimi nayakataa madai haya kwa nguvu zote, ni utoto wa kimawazo kuanza kufikiri hivi mapema, tusiache kujadili hoja ya msingi, tukianza kujadili uhalali wa Kabwe kuchaguliwa na rais anayetokea CCM tutawapa walfi nafasi ya kupumua kama wapo.

Na hapa leo nataka nikutafakarishe wewe mwenye mawazo hayo ya kitoto kuhusiana na uwepo wa Kabwe kwenye tume ya rais.

Unakumbuka kuwa Zitto Kabwe alifungiwa na Bunge (spika?) kuhudhuria vikao vya bunge kwa madai ya kulidanganya bunge, kwamba alitoa madai ya uongo, wengine wakafika mbali kwamba amemdhalilisha Waziri Karamagi? Unafikiri hii ina maana gain? Sikiliza wewe! tungeweza kumwita Kabwe ni mhalifu aliyeko kifungoni, lakini mpaka anatoka bungeni alisisitiza kuwa madai yake yalikuwa kweli, na akasema anawaachia wananchi wengine waamue, kwamba yeye alikuwa amemaliza zamu yake. Bunge likazodolewa na kushutumiwa na wanasiasa, wanaharakati na wananchi wengine wa kawaida. Ninakumbuka wakati ule nilikuwa Mbeya, nilipigiwa simu na mwanafunzi mmoja wa sekondari iliyoko Morogoro, huyu msichana alisema hivi, “niliiheshimu sana CCM, lakini sasa kwa hatua ya Bunge kumfungia Zito Kabwe, mh, mimi nahamia CHADEMA” Nilichomshauri ni kutulia ili afanye maamuzi sahihi, kuhama chama kusingemnusuru Zitto Kabwe wakati ule.

Zitto Kabwe aliitwa muongo, mzushi, wakasema anajitafutia umaarufu kwa kusema uongo, mjidala hiyo ikafika hata vyuoni na kuwagawa wanafunzi, wengine wakimtetea huku wengine wakimshutumu na kumwita kimbelembele, Zitto akasonga mbele, vyama vya upinzani vikachochea moto kwa kuamua kupanga ziara za kwenda kuishitaki serikali kwa umma, maana bunge lilishindwa kuidhiti serikali.

Mbele ya macho ya bunge Kabwe alikuwa ni mhalifu aliyeko kifungoni, kadhalika mbele ya Karamagi na Kikwete na baadhi ya wana CCM, sina shaka kwamba adhabu ya bunge kwa Zitto ilimfariji sana Karamagi aliyemwita Zitto Kabwe kuwa ni muongo na mdhalilishaji.

Wiki iliyopita limetokea jambo, sijui mpaka saa niliiteje, ninakupa nafasi ya kutoa jina. ‘Mhalifu’ yule yule, muongo, mzushi na mdhalilishaji aliyefungiwa kwa misimamo yake kwenye kulinda rasilimali za Taifa na hasa madini, leo amekuwa wa maana mbele ya rais hata kupewa ujumbe katika tume yenye kazi ya kuchunguza suala lile lile la madini. Unasemaje? Je, rais kapitiwa au anajua kwa hakika alichokifanya? Hajui kuwa Zito ni mfungwa? tena kwa sababu ya kutetea madini ya nchi yetu, madini ambayo yamefanya serikali ipoeze imani kwa wananchi wake? Rais amesahau kuwa waziri wake (Karamagi) anamchukulia kuwa Zito Kabwe ni muongo na mzushi? Kwa nini kaamua kumteua? Je, Zitto Kabwe ni msafi tofauti na anavyoonekana mbele za macho ya bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania ?

Je Zito Kabwe ni mkweli tofauti na fikra za Karamagi? Au kwa nini rais amemteua? Kwetu tunaamini kuwa mheshimiwa rais kazingatia na kuamini kuwa Zito Kabwe anafaa na anaiweza kazi aliyompa, kigezo cha uadilifu, uchapa kazi, ukweli na uwazi ndicho kilichompa kibali zito mbele za rais Kikwete.

Kama ndivyo basi, tuiteje uteuzi huo, ni fumbo la rais kwa Karamagi na bunge? Kwa maana kwamba bunge na Karamagi walivyomfikiria Zitto Kabwe sivyo alivyo? Au ni vipi? Kama ndivyo, je rais amemsuta Karamagi? Kwa hiyo kama ni hivyo, huo si ushindi wa kishindo kwa Zitto Kabwe kama mwanaharakati, kwamba sasa imethibitika kuwa alikuwa ni Nabii asiyeheshimika na kutiliwa mashaka bure tu!

Je hatuwezi kufikiri kuwa CCM na serikali yake imejizodoa? Mimi huko simo, ni katika kujaribu kuwaza na kuwazua, lakini pongezi zangu kwa rais zinabaki palepale!
Ni vipi pia? Uteuzi huo ni kitendawili? Nani atakitegua? Kinasemaje hicho kitendawili? Je ni hadithi mpya katika historia ya Tanzania ?

Suala la Zito kwenye tume hiyo limenikumbusha habari za RADA, wanaharakati walipotuhumu kuwa ina mazingira ya rushwa, baadhi ya wanunuzi wakapinga kwamba sivyo ilivyokuwa. Leo TAKUKURU imemtangaza mmoja wa watuhumiwa hao wa rushwa hadharani, hii ina maana kuwa mazingira ya rushwa yalikuwapo, je wanasemaje wanaposikia kuwa madai ya wale walioitwa wazushi yamethibitika kuwa na ukweli?

Naamini hili ni funzo hata kama rais amefanya bila kujua kuwa kuna watu wangekuja na tafsiri nyingi sana baada ya uteuzi huo.Kwa hiyo tunashawishika kuamini kwamba, kumbe kuna madai mengi ya wapinzani yakiwemo yale ya ufisadi tutakuja kuujua ukweli wake siku moja, tena watakaokuja kuuthibitisha ni hao hao wahusika, tuombe Mungu!

Kila la Heri tume ya rais!

Monday, October 29, 2007

KWA HERI SHUJAA LUCKY DUBE!


NITAMKUMBUKA LUCKY DUBE SIKU ZOTE ZA MAISHA YANGU!





KWA HERI SHUJAA LUCKY PHILIP DUBE



Natafuta namna ya kuanza kuandika makala hii, kwa sababu nataka iwe makala maalumu kabisa, na zaidi sana nataka iwe tuzo kwa kazi ya nzuri ya Lucky Philip Dube wakati wa uhai wake duniani. Mbali na serikali ya Afrika ya kusini kumzawadia kombe la dunia la Rugby ambalo nchi hiyo ilitwaa baada ya kuifunga Uingereza, nataka makala hii iwe pia zawadi ya rambirambi kwa familia ya mwanamuziki huyo na Afrika kwa ujumla.

Unaweza ukauliza pengine, kwamba kama makala hii inamhusu Lucky Dube kwa nini basi isiwe kwenye kurasa za michezo na burudani? Sikiliza ndugu yangu, kwa upande wangu mwenzako Lucky Dube hakuwa mwanamuziki na mleta burudani, kwangu dube alikuwa ni mwanaharakati kama wanaharakati wengine duniani. Ndio maana inawashangaza watu kuona Mwinjilisti kama mimi kuanza kuzungmzia habari za Lucky Dube, na uzuri sikumficha mtu, nilisema wazi nimefiwa, nimeumizwa na kifo cha ndugu huyu wa Afrika.

Nilishaacha kusikiliza nyimbo za Lucky dube, na badala yake mpaka mauti ina mkuta nilikuwa nikizisoma na kuzitafakari, zilikuwa kama hotuba za kiongozi Fulani kwangu, nilimchukulia sawa na kina Nelson Mandela na kina Martin Luthere King, Jr.

Kuna mambo mengi yanayonifanya nimtofautishe Dube na wanamuziki wengine na hasa wale wa rege, kwa mfano matumizi ya bangi, pombe na imani kwamba haile Selassie alikuwa au ni Mungu, haya na mengine yalinifanya nimheshimu Dube na kumtenga na baadhi ya wanamuziki wenzake wakiwemo wa Tanzania. Nimewahi kubishana sana na wenzangu kuhusu imani ya Dube, hasa nilipokuwa shule ya msingi pale Gilman Rutihinda pale Dar es salaam, wengi waliamini kwamba, eti kwa sababu tu alikuwa na rasta kichwani, basi yeye ni ‘rastafarian’ na pia kwamba kwa sababu aliimba rege, pengine ni kutokujua kwamba rege ni aiana ya mahadhi Fulani ya muziki na kwamba hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya rege na bangi, mimi niliamini kuwa Dube ni mkristo kwa dini, nah ii ilitokana na baadhi ya maneno ya baadhi ya nyimbo zake, kigezo kingine ni kwamba nyimbo nyingi za Lucky Dube zimeakisi ukweli kuhusu maisha yake mwenyewe aliyoyapitia.

Fuatilia nyimbo kama slave, remember me, think about the children na it’s not easy, katika mabishano hayo jamaa zangu waliendelea kushikilia misimamo yao ile, lakini Lucky Dube mwenyewe alipokuja Dar mwaka 1997 aliwahi kusema hivi “kama urastafarian ni kufuga rasta, kuvuta bangi na kunywa pombe na kuamini Haile Selassie ni Mungu basi mimi si Rastafarian, lakini kama ni itakuwa ni kuhusu siasa na maisha ya kila siku basi mimi ni Rastafarian”

Kwangu tofauti kubwa iliyoko kati ya Lucky Dube na wanaharakati na wanafalsafa wengine kama Mwalimu Nyerere wa Tanzania, Nelson Mandela, Martin Luther na wengine ni kwamba wao walikuwa hawaimbi lakini wote walitumia majukwaa kueneza ujumbe kwa hadhira yao na malengo yao yalifanana, wote ni wapambanaji, kama huamini sikiliza kauli aliyoitoa Dube mwaka 2000, hapa anasem,a hivi “A lots of people were thinking that once we had this black government everything would be fine, may be we were only fighting the past government because it was a white government. But that is not the case with me, I was just fighting the system, it is the same now, if there is injustice or any sort of nonsense towards people I will sing about that” akiwa na maana kwamba, watu wengi walifikiri kwamba baada ya kuwa na serikali ya watu weusi kila kitu kinge kuwa sawa, pengine tulikuwa tukipambana na tu na serikali ya zamani kwa sababu tu ilikuwa ni serikali ya weupe (Makaburu) lakini sivyo ilivyo kwangu, nilikuwa napambana na mfumo, na ndivyo ilivyo sasa, kama kuna namna yoyote ya uonevu na upuuzi wowote wanaofanyiwa watu (raia) nitaimba hilo nalo”

Hii si kauli ya mtu wa kawaida, ni kauli inayoweza kutolewa na wanaharakati jasiri tu kama Lucky Dube, na ukiwa makini utagundua kupitia kauli yake kwamba hakuwa mpigania haki wa Afrika tu bali pia wa Ulimwengu. Anasema ili mradi serikali hiyo inafanya ndivyo sivyo dhidi ya wananchi wake yeye ataimba. Na kupitia Dube ndipo pia unaweza kuona umuhimu wa kuwa na wagombea binafsi wa kizalendo, wao mara nyingi hawana muda wa kusiamam na kutetea maslahi ya vyama vyao au serikali za dhalimu, maana hata kama wangetaka kusiama upande wa wananchi katiba au kanuni za vyama vyao zingewabana. Hujawahi kusikia wanasiasa wanaolalamikia au kukosoa mwenendo mbaya wa vyama dhidi raia wao wanaambiwa apaleke hoja zake kwenye vikao? Wanafanya hivyo huku wakielewa fika kwamba wataminywa na kunyamazishwa. Sijaelewa hasa kwa upande wa Tanzania kwa nini bado kuna ugumu kuruhusu wagombea binafsi kama walivyo dai watu kama Faustine Munishi na Christopher Mtikila, wanahofu kitu gain?

Lucky Dube aliimba na kusema ukweli bila kuogopa Taifa, chama au serikali Fulani. Fuatilia wimbo kama Puppet masters, No truth in the World, Victims, na You stand alone utalewa nini nasema hapa.
Fuatilia wimbo wake wa 'Crazy World hapa uone
So far so good we still living today
But we don't know what tomorrow brings
In this crazy world
People dying like flies every day
You read about it in the news
But you don't believe it
You'll only know about it
When the man in the long black coat
Knocks on your door'Cause you're his next victim
As you are living in this
Chorus:Living in, living in this crazy world (x4)
Leaders starting wars every time they want
Some for their rights,
Some for fun and their own glory
letting people die for the wrong that they do
Oh it's painful
come on now little boy
Say your prayers before you sleep
Little boy went down on his knees
And he said:"Oh Lord Now I lay me down to sleep
I pray the Lord my soul to keep
And if I die before I wake
I pray the Lord my soul to take.
"'Cause he's living in this crazy worldOh Lord
Mpaka hapa sasa angalau tunaishi, lakini hatujui kesho italeta nini,
Katika ulimwengu huu uliochanganyikiwa,
Kila siku Watu wanakufa kama inzi,
Unayasoama haya kwenye taarifa za habari lakini huamini,
Unakuja kujua mpaka pale mtu mwenye koti jeusi anapokujia
Na kugonga mlangoni kwako, Kwa sababu wewe ndiwe mhanga wake
Unapoishi kwenye ulimwengu huu ulio changanyikiwa
Viongozi huanzisha vita kila wakati wanapojisikia,
wengine wa kutetea haki zao na wengine kwa ajili ya mambo ya ajabu na kujitafutia tu utkufu
Wanaaacha watu wanakufa kwa amakosa wanayofanya wao, Ooh inaumiza
Ee mvulana mdogo, fanya sala kabla hujalala, Yule kijana akapiga magoti na kusema,
Ee Bwana Sasa nalala, Namuomba Bwana roho yangu ailinde, Na kama nitakufa kabla sijaamka
Namumba Bwana roho yangu aichukue, Kwa sababu anaishi kwenye ulimwengu huu uliochanganyikiwa!

Lucky Dube aliwashinda hata baadhi ya wanasiasa kwa moyo wa upendo kwa watu wake, na kwa moyo huo ndio maana mmoja wa mawaziri nchi Rwanda katika salamu zake za rambirambi amesema wamempoteza rafiki yao . Ni nadra sana kwa viongozi wa kitaifa kutoa kauli zao kwenye vifo vya wana muziki wengie wa kawaida, ndio maana nakwambia kwa watu wanaofuatialia masuala ya kiutawala, haki na usawa watakubaliana na mimi kuwa Dube hakuwa tu mwanamuziki bali mwanaharakati hasa, hilo linaweza lisisemwe wazi au hadharani na wanasiasa lakini wanaelewa mishale yake, nah ii ni hasa kwa wanasiasa wakorofu, waonevu na wadhalimu dhidi ya wananchi wan chi zao. Dube alikuwa makini kwa maana ya kuijua historia ya Afrika na jamii yake.

Alitembelea Rwanda mara tu baada ya mauaji ya halaiki mwaka 1994, mauaji ambayo hayatasahaulika kwa vizazi hivi vya karibuni, huko alifanya maonesho kwenye jiji la Kigali kwenye uwanja wa mpira wa Amahoro (Amani) na moja kati ya nyimbo zilizowatoa Wanyarwanda machozi ni ule wa ‘together as one’ sehemu ya wimbo huo inasema hivi


In my whole life,My whole life I've got a dream (x2)

Too many peopleHate apartheid Why do you like it? (x2)

Chorus: (x3)Hey you rasta manHey European,Indian man, We've got to come together as one

Not forgetting the Japanese


The cats and the dogsHave forgiven each otherWhat is wrong with us (x2)All those yearsFighting each otherBut no solution (x2)


Kwa kiswahili anasema. Katika Maisha yangu yote nimekuwa na ndoto, watu wengi hawapendi ubaguzi wa rangi, kwa nini wewe unapenda, enyi marastafariani, wazungu na wahindi tunatakiwa kuwa kitu kimoja

Paka na mbwa walisameheana, tatizo ni nini kwetu? Miaka yote hii tumepigana wenyewe kwa wenyewe bila suluhisho,


unaonaje wewe ujumbe huu, je haukuwa mahususi kwa Wanyarwanda kwa wakati ule? Bila shaka aliimba pia ule wimbo wake wa “we cray for peace’ (tunalilia Amani)
Katika wimbo huo anasema “tunalilia Amani kamili, Ee Mungu tunalilia upendo katika ujrani huu, nakwambia hakuna maji yanayoweza kuzima moto huu (vita) Ni Mungu peke yake anaweza kutuokoa”
Kuanzia wiki ijayo nitakuletea maelezo na tafsiri ya baadhi ya nyimbo zake kwa wiki mbili ikiwa ni ishara ya watoto wawili wa Dube walioshuhudia mauja ya baba yao.

Dube pia atakumbukwa na watu masikini duniani kwa sababu ya kuwatetea, aliwashukia matajiri wa ulimwengu kwa kusema utajiri wao hakuwa na maana yoyote duniani kama watakuwa hawawajali masikini na wale watu wasio na matumaini katika wimbo wake wa ‘hand that giveth’
Sasa LUCKY PHILIP DUBE hayupo tena, wamekatisha uhai wake kwa risasi, mtu ambaye pamoja na kwamba hakunifahamu nilimuombea ampe Yesu maisha yake, niliwahi panga siku moja kwamba siku za usoni ningemtembelea Afrika ya kusini ili kumshirikisha neno la Mungu, sasa katoweka na ndoto zangu zimezimika. Naanza kurudi nyuma kukumbuka jinsi alivyonifanya nitoroke shule kwenda kumpokea uwanja wa ndege Dar es salaam na alipokuwa anaorudi kwao nilitega shule kuhakikisha kuwa naenda kumuaga, nakumbuka nilipokuwa nagombana na mama nyumbani kwa sababu ya kupiga kanda zake mfululizo na kuziimba pia kwa sauti, nakumbuka nilipogombana na walimu kama vile mwalimu Sadala na mwalimu Assey pale Rutihinda kwa kutembe kila wakati huku nikiimba nyimbo za Dube, nilipotumia nyimbo zake kama mifano katika mazungumzo na rafiki zangu na katika baadhi ya makala zangu, Bila shaka wakina Simba Ramadhani, George Madanga, Hafidh Ismail, Juma, Humphrey Mutabirwa na Ukasha Mrami wanakumbuka nilivyokuwa kituka kwa kuwehuka na mwanaharakati huyo, ndio maana pamoja na kuelewa kwamba hivi sasa mimi ni mchungaji bado hawajaacha kunitumia salamu za pole! Hayupo tena! Tuonane wiki ijayo kuendelea na maombolezo na kumbukumbu hii muhimu katika maisha yangu!

Sunday, July 29, 2007

YANAJIELEZA YENYEWE!

YANAJIELEZA YENYEWE!

Kabla sijaanza kuandika makala hii naomba nitoe utabiri japo si mtabiri, labda nianze leo. Makala hii inaweza ikazaa maswali kama “una uhakika gani?” “takwimu imezitoea wapi?” “tupe vielelezo” na mengineyo mengi, yasipotokea maswali hayo msije kunisuta, tayari nilikwisha sema kuwa mimi si mtabiri ila natabiri tu! Ni kichekesho eeh??


Ingekuwa barua ningeanza makala hii kwa kusema, kicha cha somo hapo juu chajieleza! Na kweli hivi ndivyo ninavyoweza kusema, na sababu kubwa ya kusema hayo ni yale tunayoyaona mitaani tangu bajeti ya serikali ilipopitishwa!

Malalamiko ya watanzania ni mengi, yale yanayoandikwa kwenye magazeti kwa upande wa habari na makala za wachambuzi mbalimbali si yote ya uzushi, yale yanayosemwa kwamba watanzania wameanza kukata tama, si ya kutunga ili kuuza magazeti, na itakuwa dhambi kubwa magazeti hayohayo kuacha kuripoti habari kama hizo kwa sababu tu ya kuogopa na kujipendekeza kwa wakubwa.

Ni ukweli unaoandikwa humo, lugha rahisi tunayoweza kutumia hapa ni kusema watanzania wamechoka, kwa hivi sasa lolote ni sawa! Maisha yao ni duni nay a kuvunja moyo! Lugha hii ni ngumu kueleweka kwa baadhi ya wakubwa serikalini, na hasa wale ambao kwao huamini kuwa kukosolewa au kuambiwa ukweli ni kudhalilishwa, wanaogopa na kuukwepa ukweli huku watanzania wao wakiendelea kukandamizwa na ugumu wa maisha. Maisha ni magumu kwa wengi wa watanzania! Ni ajabu sana serikali inapojaribu kupingana na watanzania binafsi wananochambua mambo magazetini badala ya kufanyia kazi uchambuzi uliotolewa!

Gharama ya maisha ya mtanzania inapanda bila sababu za msingi za kua hivyo. Tutafakari suala ambalo kwa serikali linaonekana dogo sana lakini linaloumiza watanzania. Suala la kupanda kwa bei ya mafuta na hatimaye kusababisha kupanda kwa nauli. Kwa mawazo yangu kidgo, naanza kuamini kuwa pengine serikali haiwajui vyema watu wake, haijui matatizo yanyowakabili wananchi wake, na ni hatari sana kama imani yangu iko sawa basi hali ni mbaya!

Nimetafakari sana kuhusu mkazi mtanzania wa Bunju ambako kutoka huko mpaka mwenge nauli ni shilingi 400 (kama ni sawa) na kutoka Mwenge mpaka kariakoo anakofanya kazi hotelini na kupata mshahara wa shilingi 30000/= kwa mwezi ni shilingi 250, nauli imepanda huku mshahara wake ukiwa umebaki pale pale, hii ina maana kwamba nauli yake kwa mahesabu ya harakaharaka inazidi mshahara wake kwa mwezi, hapo hajala, hajalipa kodi na ni bachela! Na si kwamba amependa kuishi huko ni mazingira yalimfanya alazimike kuwa huko. Watanzania wa jinsi hii wako wengi sana , wanaendelea kuteseka!

Watanzania kwa njia tofautitofauti waliililia serikali kwamba chonde ifanye linalowezekana kupunguza makali haya, lakini wapi! Wapinzania wakaja na bajeti yao mbadala amabyo mpaka wasomi wameisifu kuwa ni nzuri na yenye kufaa! Swali linakuja, kwa nini serikali inashindwa kuchukua bajeti hii na kuitumia? Je sio utaratibu? Ni kiburi au dharau kwa wapinzania hao? Je tunaendesha serikali kwa manufaa na maslahi ya nani kama si wananchi? Kwa nini tusichukue yale mawazo yanayofaa kwa ajili ya wananchi wetu bila kujali ni chama gani kimetoa mawazo hayo?

Je serikali inaogopa kwamba ikitumia mawazo ya wapinzani itachekwa na kudharauliwa? Kama ndivyo japo hawawezi kukiri hadharani, watazuiaje hisia zetu kwamba wako madarakani kwa maslahi yao na si wananchi?

Mambo mengi yameandikwa, tumeandika hata sisi tusio waandishi wa habari, kwamba watanzania wamechoka na kukata tamaa, kwamba serikali isikilize maoni ya watanzania, hii nchi si ya mtu mmoja, nchi hii ni ya kidemokrasia, serikali ya kidemokrasia ni serikali ya watu, iliyoundwa na watu na kwa ajili ya watu, hili ni muhimu kulikumbuka kila siku, wala tusilewe madaraka na kusahau, kwamba serikali hii ni ya watu, tena kwa ajili ya hao hao watu, wanapolia wasikilizwe, wanapoomba msaada wapewe, maana serikali hiyo haipo kwa ajili ya chama au taasisi Fulani, ni serikali ya watu!

Wanapopiga mayoe ya machungu ya maisha wasikilizwe, si vyema kudhani wananchi wote ni mambumbu, wa kuwaambia ndege inapaa wakati wao situ kwamba haipai, bali pia haionekani machoni mwao. Tukisema hivi tunaweza kuonekana wachochezi na kuanza kutafutwa, kuuliziwa, badala ya kuchukua maoni tunayotoa. Tunaamini kwamba pengine rais au waziri mkuu hajui au haoni kuwa watanzania wana hali ngumu, tunaamini pia kuwa kwa njia hii tunamsaidia!

Narudia kusema kwamba watanzania wote si vipofu, wanaona, si viziwi, maana wanasikia, tatizo si kwamba ni mabubu isipokuwa wamezibwa tu midomo yao wasiseme, wamezibwa kwa kutishiwa hata usalama wao! Hili litaendelea kudidimiza maendeleo ya nchi hii. Tukubali kuambiwa ukweli, na ndio maana tunasema kwamba tunaomba ikibidi sasa itafutwe njia mbadala ya kupunguza makali haya ya maisha kwa watanzania!

Tunapoizungumzia Tanzania hatuizungumzii Dar es salaam, Arusha au Mwanza pekee, tuaihusisha pia Singida, Kigoma, Mtwara, Pemba, na maeneo yote ambayo wengine wanaishi kama vile si watanzania!

Watanzania walioko vijijini ambako hakuna barabara nzuri wanaathirika sana na kupanda kwa bei ya mafuta, bei ambayo kuna uwezekano mkubwa wa kuishisha ilo watanzania wapumue kidogo!

Tafadhali, naandika kwa uchungu, na wala nisiitwe kimbelembele, kwamba najipendekeza kwa watanzania, hapana! Mimi ni mmoja wa watu wanaoathrika na hali hiyo, wazee wangu kule vijijini wanaathirika. Mtu mmoja aalizungumza maneno mazito na ya uchungu sana , alisema hivi “sasa hivi tutakuwa tukizikana kwa simu” alikuwa akiongea hayo baada ya kupata habari za msiba wa ndugu yake, alikuwa akimwambia mdogo wake! Akiwa na maana kwamba hawawezi tena kumudu nauli za mikoani kwenda kuzika ndugu zao!

Serikali isilalie masikio, ahadi zake kwa watanzania ni nyingi mno! Tunaiombea kila la heri isikilize vilio vya watanzania!

Saturday, July 21, 2007

Happy Birthday Madiba

Nelson Rolihlahla Madiba Mandela

Naandika makala hii kwa heshima kubwa ya mwanaharakati chipukizi kabisa, mwanafunzi wa sekondari, Elizabeth David wa Arusha. Ni moja ya hazina zinazochipuka kwa taifa hili wakiwa na moyo wa uzalendo kwa Taifa hili, nikipata nafasi nitaeleza kirefu kuhusu yeye.

Leo namzungumzia Nelson Rolihlahla Madiba Mandela, kwangu huyu ni mmoja kati ya zawadi ambazo Mungu aliamua kuutunuku ulimwengu, namwita shujaa na hilo halihitaji ufafanuzi wala wakati wa mjadala. Maisha yake yanajieleza.

Alizaliwa kitongoji cha Transkei nchini Afrika ya Kusini tarehe 18, julai 1918, hii ina maana kwamba wiki iliyopita tarehe 18, jumatano mwana huyu wa Afrika alitimiza miaka 89. Kwa faida ya wasomaji wa safu hii, shujaa huyu alizaliwa na baba ambaye alikuwa chifu wa kabila la Watembu, aliitwa Henry mandela.

Miongoni mwa mambo mengi ambayo pengine wengi wetu hatuji labda kwa sababu hayajaripotiwa sana, ni kwamba kwa taaluma Mandela ni mwanasheria aliyehitimu shahada yake katika chuo kikuu cha Witwatersrand mwaka 1942 kabla hajawa mwanasiasa kwa kujiunga na ANC mwaka 1944

Kuishi maisha ya miaka 89 katika ulimwengu huu uliochanganyikwa si kitu kidogo hasa kwa mtu kama mandela aliyepitia karibu robo ya maisha yake. Kati ya misukosuko ikiwemo kuwekwa gerezani kwa miaka ipatayo 27.

Unaweza kumwita Mandela shujaa, jasiri, mapambanaji au mwanamapinduzi. Alipinga uonevu wa kila namna, alikataa ukandamizaji na aina ya maisha ya watu waliotaka kujifanya miungu wa dunia hii. Kwa nini nasema haya yote! Sikiliza mandela alivyosema mwenyewe:

Anasema “Nimepinga utawala wa watu weupe, nimepinga utawa wa watu weusi. Nimeheshimu mpango wa kidemokrasia na jamii iliyo huru ambapo watu wote wataishi pamoja kwa amani pamoja na fursa sawa. Ni mpango ambao nitaishi kwa ajili hiyo na kuufanikisha. Lakini ikibidi, basi ni mpango ambao nimejiandaa kufa kwa ajili yake”

Maneno haya ni mazito sana, Mandela aliyasema haya alipohukumiwa kifungo cha miaka mitano katika kesi fulani hivi, eti kwa kosa la uhaini, lakini uhaini uliodiwa na maadui zake ni kile kitendo cha yeye kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika ya Kusini. Hiyo ni mwaka

Kwa wale amabo wamefuatilia maisha ya harakati ya Madiba wanaweza kukubaliana na mawazo yangu kwamba Mandela hakuwa tu msemaji bali pia mtu wa vitendo, na si hivyo tu bali pia alianza kutenda kabla ya kusema, upo hapoo? Baada ya kutafakari hayo, nikajikuta nakumbuka aya fulani ya Biblia inayosema “kitabu kile cha kwanza nalikiandika, Theofilo, katika habari ya mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha” Matendo 1:1 Unaona hapo, watu wanaanza kutenda na kisha kusema au kufundisha.


Je wakoje wanasiasa wetu wa leo, unaweza kuwafananisha na Mandela? Je wanamfikia hata kwa mbali? Wangapi angalau wanatenda wanachokisema? Mandela alianza kutenda kabla hajasema, alianza kupigania uhuru wa waafrika hata kabla Afrika haijajua dhamiri yake, kabla waafrika hawajajua, kabla hatamka hadharani kuwa amejitolea maisha yake kuipigania Afrika!

Kwa nini nasema kuwa alianza kutenda kabla hajasema? Tuirejee kwanza sehemu ya kauli yake “Ni mpango ambao nitaishi kwa ajili hiyo na kuufanikisha. Lakini ikibidi, basi ni mpango ambao nimejiandaa kufa kwa ajili yake”

Angalia maisha yake kabla ya kuwekwa gerezani, alipigania uhuru wa weusi, kitu ambacho wazungu walikitafsiri kama uhaini na hivyo kumtupa lupango.

Je, alipigana kabla ya kutoa kauli hiyo gerezani?
Ndiyo, hii ni bada ya chama chake cha ANC kupigwa marufuku kuendelea kuwapo nchini Afrika ya Kusini mwaka 1960. Je Mandela akaishia hapa? Hapana, kitendo cha ANC kufungiwa kilichochea moto wa harakati za mandela kwani kwa ushawishi wake baadhi ya maodfisa wa ANC walikubali kuunda kikundi kingine cha harakati za ukombozi kilichojulikana kwa jina la Umkhonto we Sizwe kikiwa na malengo yale yale ya ANC, wao walikitafsiri kikundi hiki kama ubawa (wing) wa ANC. Kwa kitendo hicho, ilipofika mwaka 1962, Mandela alikamatwa na kuhukumiwa kifungo miaka mitano pamoja na kazi ngumu akiwa gerezani, hatia kubwa kwa mujibu wa wazungu ni kwamba, eti Mandela alikuwa akitaka kuipundua serikali yao nchini humo. Ndio maana nasema alianza kupambana kwa ajili ya ndugu zake waafrika, hata kabla hajawaambia kuwa atapambana kwa ajili yao! Tuko pamoja?

Mwaka 1964, July, 14, Mandela na wenzake walihukumiwa kifungo cha maisha. Kitendo hicho kilikuwa kama kinauamsha ulimwengu kuanza kujua hasa Mandela alikuwa nani kwa Waafrika.

Nelson Mandela aliachiwa huru februal 11, 1990 . Je aliacha kutekeleza ahadi yake kwa waafrika? Hapana kwani kwa moyo wake wote akajikita zaidi katika mapamano kama alivyokuwa ameahidi, alipigfania kutimiza ndoto zake. Ndoto gani? Alisema hivi “Nimepinga utawala wa watu weupe, nimepinga utawa wa watu weusi. Nimeheshimu mpango wa kidemokrasia na jamii iliyo huru ambapo watu wote wataishi pamoja kwa amani pamoja na fursa sawa. Ni mpango ambao nitaishi kwa ajili hiyo na kuufanikisha. Lakini ikibidi, basi ni mpango ambao nimejiandaa kufa kwa ajili yake”
Ndio maana mwaka 1991, katika kongamano la kwanza la ANC, Mandela alichaguliwa kuwa rais wa ANC huku swahiba wake Oliver Tambo akiwa Mwenyekiti.

Tangu wakati huo, Mandela hajaacha kupambana, wiki iliyopita huku akiadhimisha miaka 89 ya kuzaliwa kwake, alizindua kikundi cha viongozi mashuhuri, wazee wenye hekima duniani kikiwa na lengo la kutatua matatizo yanayoikabili dunia kwa sasa.n Kikundi hiki kikiongozwa na Mandela mwenyewe kwa kusaidiana na mkewe Graca Machel na mwenyekiti wake, Askofu mkuu mstaafu, Desmond Tutu watatumia hekima walizojaaliwa na mwenyezi Mungu kuikwamua dunia kutoka mahali pabaya ilipofika. Unaweza kuona sasa, kwamba Mandela bado anapambana.

Swali langu ni hili, je viongozi wetu wa leo watakuaje watakapofika umri huu wa Mandela? Je watakumbukwa na kuenziwa kama tunavyomuenzi mzee huyu? Mbona baadhi yao wameanza kuchokwa na watu wao, majimboni, wilayani, na kwinginekeo wakati hata miaka 60 bado? Hii ni changamoto, Mandela hajatumia uchawi, uchawi wake mkubwa ni moyo wake wa kujitoa kwa ajili ya watu wake, na wala sio kujaza matumbo tu kwa kula vya wananchi.

Nilikwambia naandika makala hii kwa heshima kubwa kabisa ya wanaharakati akiwemo binti mdogo Elizabeth David, je wao watakuwaje? Kwa mfano, Elizabeth anampend sana Mandela, basi ni vizuri akatamani pia moyo wa Mandela, ili afanikiwe na kisha kuenziwa baadae!

Nimalizie kwa kumtakia kila la heri, mzee Nelson Rolihlahla Madiba Mandela, heri yake ya siku ya kuzaliwa!

Wednesday, July 4, 2007

WARAKA WANGU KWA WATANZANIA!

Nianze kwanza kwa kukusalimu popote ulipo ee Mtanzania, poleni kwa yote ambayo mnakutana nayo katika kila iitwayo siku kwenu. Baada ya salamu napenda kuwauliza swali, je ninyi ni wazalendo? Tafadhali lifanyie kazi swali hili.

Baada ya swali hili naomba nitoe ombi langu kwako wewe uliyebahatika kusoma waraka huu. Chonde chonde, jitahidi, fanya kila uwezalo uhakikishe waraka huu unasomwa na watanzania wengi kama si wote. Jitahidi kuwa mbunifu ili kufanikisha hilo.

Unaweza ukanunua nakala nyingi kadri uwezavyo na kuwagawia watanzania wengine, (hakikisha unayempa ni mtanzania) Pia unaweza ukasoma na kuanza kuzungumza na wenzako kuhusu waraka huu, nenda kawaelimisha, usijali kama wataukubali au watakataa ujumbe huu! Omba tu wakupe nafasi wakusikilize.

Pia unaweza ukatuma anuani ya tovuti ilipo hapo juu kwa wote walioko mikoani na nje ya nchi, waambie wasome kupitia mtandao wa ‘Internet’ anuani yenyewe ni hii www.amkenitwende.blogspot.com, tafadhali nisaidie kuufikisha ujumbe huu kwa watanzania wa rika, hadhi, jinsia na hali zote, nisaidie tafadhali!

Kwa nini nimeamua kuandika waraka huu? Nimekuwa nikisisitiza kila siku kwamba hii nchi ni ya kwetu. Ni sisi ndio tutakaojenga au kubomoa nchi hii. Nchi hii si mali ya CHADEMA, CUF, CCM, UDP, NCCR-Mageuzi au vinginevyo. Hakuna waziri au Mbunge mwenye hati miliki ya nchi hii. Hata Mwl. Nyerere alikuja, akaitumikia nchi hii, kwa kutambua kuwa hii nchi si mali yake, ulipofika wakati akawaachia watanzania wengine kuongoza nchi hii.

Ninachosisitiza hapa ni kwamba hii nchi ni watanzania walioko kule Magila kule Gonja, ni wale walioko Mlalo, Lushoto, walioko Kizorogoto kule Morogoro na kila paitwapo Tanzania. Kuna haja ya kuondoa dhana ndani ya fikra zetu kwamba Tanzania inamilikiwa na SERIKALI, kwa hivyo wananchi wa kawaida hawana la kufanya katika kujenga nchi hii.

Nakumbuka siku moja nikiwa eneo mojawapo hapa Dar es salaam, katika mitaa ya eneo hilo ilijaa uchafu na madimbwi ambayo ulikuwepo uwezekano mkubwa na wa kutosha kabisa kuondosha ile hali. Ilinibidi kuzungumza na baadhi ya wakazi kuhusu suala la uchafu ule. Mmoja wapo alijibu na kusema kwamba sisi sio jiji, kuhusu kupasuka kwa mabomba yanayotoa maji na kumwaga barabarani walisema wao si DAWASCO hata waamue kushughulikia tatizo hilo.

Kwa watanzania wengi kila kitu kinafanywa na serikali, pengine enzi za ni athari za ujamaa ndizo zinazotusumbua kwa sasa, lakini je hii nchi bado ni ya kijamaa kwa kweli? Hata kama Katiba inaeleza hivyo katika kifungu cha………

Kila mwanadamu anayezaliwa katika ardhi hii huzaliwa kwa makusudi, na ndio maana ni vizuri kujihoji kila mara, UNAIFANYIA NINI TANZANIA? Naamini kwamba ni watanzania wengi sana hawajawahi na hawana mpango wa kujiuliza swali hili, kama imani yangu ni potofu naomba nisamehewe. Yote haya ni kwa sababu tunadhani hatuhusiki kwa namna yoyote katika kuijenga nchi hii, na ndio maana kila kinachotokea na kutudhuru hutupa lawama kwa serikali, lakini tunashindwa kukumbuka kuwa pengine tunahusika kuifanya serikali ifanye yale inayoyafanya.

Sikatai kuilaumu serikali, serikali ni mzazi, anabeba lawama pale anaposhindwa kuwafanyia watoto wake stahili yao. Lakini hatuwezi kumlaumu mzazi eti kwa sababu mtoto wake mwenye umri wa miaka 24. mwenye akili timamu, mwanafunzi wa chuo kikuu mwaka wa kwanza haogi kwa sababu ya uvivu tu! Hatuwezi, tutaonekana wehu!

Kama wananchi tuna wajibu wetu kuhakikisha nchi hii inakwenda kuliko inakotakiwa kwenda. Naomba nitoe mfano kidogo hapa.

Hivi karibuni kumetokea ajali za kutosha zilizo poeteza watanzania wenzetu, sasa hawapo, wamelala mauti! Hatukuchelewa baadhi yetu kuilaumu serikali kwa sababu ya ajali hizo. Moja ya sababu zilizotolewa na baadhi ya wahanga wa ajali hizo ni mwendo kasi! Hili nalo tumeilaumu serikali.

Kuna wakati tuliilaumu serikali kwa sababu ya magari kujaza abiria kwenye mabasi yaenadyo mikoani! Ngoja nkiupe kisa hiki halafu niendelee!

Tarehe 19/05/2007 nilisafiri kimasomo kwenda mkoani Tanga, kama kawaida nilipanda gari pele stendi kuu. Safari ilianza vizuri sana, lakini tulipofika kituo cha Kibaha, lile basi lilipakia abirai zaidi kiasi cha kufanya wengine kusimama, kumbuka hiyo ni safari ya kwenda Tanga.

Kitendo kile kilishuhudiwa na askari mmoja wa usalama barabarani ambaye alipanda lile gari na kuwataka abiria wengine wapungue. Ndugu yangu abiria waliokuwamo kwenye gari walikuja juu kwa kitendo cha yule askari kutaka kupunguza abiria. Hoja yao ilikuwa ni kwamba wanacheleweshwa. Sio siri nilishindwa kuvumilia kile kitendo cha abiria wenzangu.

Nilisimama na kumtetea yule askari, si kwamba nilikosa siti ya kukaa, nilikuwa nayo! nikawa kama nimewasha moto ndani ya basi, kwani abiria wote walikuja juu na kuniita mnafiki, nilikuwa katika wakati mgumu sana. Katika lile gari kulikuwamo mwanafunzi mwenzangu yeye anachukua masomo ya sheria. Akageuka na kuwa mwiba kwangu, yeye alivuka mipaka na kutaka kunivamia ili kunipiga mbele ya askari wapatao watatu pale Kibaha, huyu ndiye mwanasheria wan chi hii baadae! Hoja yake ni kwamba mimi ni kimbelembele na kwamba nachelewesha safari za watu!

Amini usiamini askari wote pale walizidiwa nguvu na abiria, gari ikaachwa iende ikiwa na abiria waliosimama kama mizigo kwenye basi. Na abiria wale waliapa kwamba nikipanda lile gari nitakiona cha moto, nakwambia nilishushwa na kutafutiwa gari ingine. Hii ndio nchi yetu, na wale ndio watanzania wenyewe. Ajali ingetokea pale, lawama ni serikali.

Hiyo ni moja, pili nakumbuka nilikupa kisa kimoja nilipokuwa natokea Nairobi kurudi nchini, kwamba gari ilikwenda mwendo wa kasi mno, lilikuwa ni basi la kampuni ya SABCO, wakati tunalalamika mwendo huo, kuna abiria wakatupinga vikali na kumtaka dereva aongeze mwendo zaidi. Mungu bariki tulipofika maeneo ya michungwani mkoani Tanga, askari mmoja alisimamisha liele basin a kumuonya yule dereva, kasha akatoa namba yake ya simu ikiwa yule dereva ataendesha kwa mwendo mbaya, si hivyo tu alituachia jina lake kuwa anaitwa YOHANA, Ee Mungu tupe askari wengine wengi kama Afande YOHANA!

Ndugu zangu sijasahu nilipokuwa mkoani Singida mwaka 2004 ambako nilikwenda kwa shughuli za kuhubiri ujumbe wa neno la Mungu, niligombana na baadhi ya wasafiri wenzangu kwa sababu ya kuzidisha abirai kwenye basi la kampuni ya TASHRIF, ambayo baadae ilipata ajali muda mfupi baada ya kuondoka Stendi kuu ya Singida.

Hivi una habari kuwa kuna watanzania huwa wanachanga pesa ili kuwalipa askari wa usalama barabarani pindi madereva wanapofanya makosa? Tunailamu serikali kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kama yale ya kulinda usalama wa raia wake, je sisi tumetekeleza yapi ili kulinda usalama wetu? Pengine ni maneno magumu na machungu sana naongea hapa, mniwie radhi, nivumilieni, huu ndio ukweli!

Hii ninayoitoa hapa ni mifano kidogo tu! Watanzania tumekuwa pia na nidham ya uoga isiyo kifani, tuna chembe Fulani ya unafiki.

Siku moja tukiwa darasani chuoni, kulianza mjadala kuhusu tatizo la rushwa Tanzania, katika hali ya kustaajabisha kuna baadhi wakawa wanakiri na kusimamia kwamba rushwa haiwezi kuondoka, ungesikiliza kwa makini ungegundua kuwa si kwamba haiwezi kuisha kwa sababu ya ugumu wake, bali ni kwa sababu ya maslahi ya watu Fulani, kuna wajumbe wakafikia hatua ya kusema bila haya kwamba ihalalishwe! Hawa ni watanzania! Ninyi mnapigana na adui upande wa kusini, upande wa kasikazini kuna wapiganaji wenzetu wanamtia moyo adui na kumpa mbinu za kutushinda!

Makala hii itaendelea wiki ijayo!