Hali ni mbaya, nimeona leo tushirikishane juu ya uzalendo! Uzalendo! Unajua uzalendo wewe? Hali ya kujitoa kuipenda nchi yako, unaithamini, unailinda kimaadili, kisiasa, kiitikadi na kadhalika. Nasema unaipenda nchi yako, huu unaitwa uzalendo, naam kuipenda nchi yako.
Utashangaa nikikwambia kwamba binadamu wengi (sio wote) waishio katika nchi ya Tanzania, hawaipendi Tanzania. Nimesema binadamu, nimeogopa kutumia neno ‘watanzania’ Unaweza usinielewe. Labda niseme hivi, Watanzania (kama ulivyozoea kuita) wengi hawana mapenzi na nchi yao. Wako tayari kufanya lolote baya na kuidhuru nchi yao.
Hii ni kuanzia viongozi wa nchi mpaka raia wa kawaida. Hawaitaki Tanzania wala vilivyomo humu. Namaanisha kwamba, hawapendi lugha yao ya Kiswahili, wananchi wenzao, viongozi wao, mavazi yao( vazi la Tanzania ni lipi?) Unaweza kunizodoa kwa hoja hiyo. Nitakuuliza swali, ule mpango wa kubuni vazi la taifa umeishia wapi? Liko wapi hilo vazi? Juhudi zipi zimefanywa na wizara yenye dhamana ya utamaduni wa nchi hii kuhamasisha matumizi ya vazi hilo? Umewahi kumuona waziri wa utamaduni wa nchi hii amevaa vazi la kitanzania? Uliona waziri wa utamaduni siku alipokuwa akiapishwa alivaa vazi la wapi? Hiyo kazi nakupa katafute jibu, kama ukijisikia nitumie jibu hilo.
Tuhamie kwa wabunge wetu, wanapokuwa na vikao vyao kule Dodoma, si umewahi kusikia, huwa wanageuka na kuwa waingereza? Hawataki kutumia lugha yao ya Taifa, wanasahau kabisa kwamba wao ni wawakilishi wa mamilioni ya Watanzania ambao hawajui lugha hiyo ya kiingereza. Tatizo lao ni nini? Kwa nini wasitumie lugha yao asili ambayo pamoja na kuzungumza pia ni kuikuza ili iwe ya kimataifa kama ilivyo kwa lugha ya kiingereza? Huu ni uzalendo?
Waangalie nao wasomi wetu, wanaandaa mada zao wakiwalenga watanzania, bado wanatumia kizungu kuwasilisha mada hizo, sijui kama watakupa sababu za kueleweka zinazowafanya wakwepe kutumia Kiswahili utakapowataka wafanye hivyo. Je huu ni uzalendo?
Tusafiri pamoja na kufika kwenye asasi mbalimbali, kule kwa wanaotumia kiingereza wanaita NGO’s, asasi hizi ni zile zenye waasisi wa kitanzania. Ziwe za kuhusu elimu ya UKIMWI, elimu, afya na kadhalika. Wanapoweka matangazo yao, angalia kwa makini, mengi yako kwa lugha ya kiingereza kana kwamba wanawasiliana na watu wa mataifa mengine ambayo si Tanzania, kazi tunayo!
Tusiache kuwatembelea vijana vijiweni, hawa ndio kabisa, siku hizi ili waonekane bora watakwambia wanazungumza kizungu, wanacheka kizungu, wanavaa kizungu (vitovu vikiwa nje kwa upande wa mabinti) n.k hawataki kuonekana kuwa ni watanzania.
Unajua nini namaanisha katika makala hii? Chochote unachofanya ili kuihujumu nchi yako kwa namna yoyote ile, tunasema huo si uzalendo. Nimetoa mfano mdogo tu wa kuidharau lugha yetu.
Je nimetoka nje ya mada? Hivi nazungumzia nini hapa? nazungunzia nini vile? Aah!..nimekumbuka, nilikuwa nahoji sababu ya wasomi kusota mitaani wakiwa taabani kiuchumi. Nikasema tatizo ni uzalendo.
Maana yangu ni hii, viongozi wa nchi hii wamekuwa si wazalendo, utendaji wao unathibitisha hilo. Kama kiongozi ni mbovu na anashutimiwa wazi wazi kwa rushwa na hataki kujiuzulu, tumwiteje kama si mtu wa kuihujumu nchi yetu?
Mtu anayeingia mikataba ya siri ambayo baadaye inasababisha mahangaiko kwa wananchi wake tumpe jina gani? Au mtu anayeiuza nchi kwa kisingizio cha ubinafsishaji (usio na mpangilio) tumbatize jina lipi? Nisaidieni tafdhali!
Mtu anayeuza mashirika ya umma na kuwapa wazungu kwa kigezo cha kuboresha uzalishaji na kukuza uchumi wa nchi hii apewe jina gani? Ni wahujumu hawa!
Naomba niongeze swali hapa, nitafutieni jina la kumpa mtu anayewanyima mikopo wanafunzi kwa kisingizio cha alama za kufaulu, huku akijua wazi kuwa anarudisha nyuma maendeleo ya elimu yetu nchini. Mimi namwita mhujumu wa elimu ya nchi hii, hivyo si mzalendo!
Viongozi wengi wa nchi, huwa wanajisahau wanapoyakwaa madaraka, ndani Yao huzaliwa kitu kinaitwa ubinafsi, hawataki tena kujishughulisha kitaifa, pengine hujishughulisha zaidi na familia zao na jamaa zao. Kama ndivyo napata swali, kwa nini waliyakubali madaraka, kwani hawakujua kuwa wanakwenda kuwatumikia wananchi na si familia zao?
Wajibu wa kuandaa mazingira ya ajira na kujiajiri ni wa serikali. Serikali ndio inayoweka kanuni na taratibu za ajira na kujiajiri. Wananchi hata kama wangekuwa na uwezo wa kujiajiri, bado watalazimika kufuata taratibu na kanuni zilizowekwa na serikali yao. Sera na mipango.
Uzalendo…uzalendo uzalendo, naimba wimbo huu uzalendo, nasisitiza uzalendo. Hata hivyo ni muhimu kufahamu kuwa kuamua kua mzalendo kwataka moyo, kuna gharama za kuwa mzalendo na ndio maana huwa naamini kuwa uzalendo sio tabia, na kama ni tabia basi ni ile tabia sugu, imebadilika inakuwa ‘spirit'
Friday, June 15, 2007
Umeelewa hoja yangu ya leo, basi amka twende!
0713 550 778
Subscribe to:
Posts (Atom)