Sunday, July 29, 2007

YANAJIELEZA YENYEWE!

YANAJIELEZA YENYEWE!

Kabla sijaanza kuandika makala hii naomba nitoe utabiri japo si mtabiri, labda nianze leo. Makala hii inaweza ikazaa maswali kama “una uhakika gani?” “takwimu imezitoea wapi?” “tupe vielelezo” na mengineyo mengi, yasipotokea maswali hayo msije kunisuta, tayari nilikwisha sema kuwa mimi si mtabiri ila natabiri tu! Ni kichekesho eeh??


Ingekuwa barua ningeanza makala hii kwa kusema, kicha cha somo hapo juu chajieleza! Na kweli hivi ndivyo ninavyoweza kusema, na sababu kubwa ya kusema hayo ni yale tunayoyaona mitaani tangu bajeti ya serikali ilipopitishwa!

Malalamiko ya watanzania ni mengi, yale yanayoandikwa kwenye magazeti kwa upande wa habari na makala za wachambuzi mbalimbali si yote ya uzushi, yale yanayosemwa kwamba watanzania wameanza kukata tama, si ya kutunga ili kuuza magazeti, na itakuwa dhambi kubwa magazeti hayohayo kuacha kuripoti habari kama hizo kwa sababu tu ya kuogopa na kujipendekeza kwa wakubwa.

Ni ukweli unaoandikwa humo, lugha rahisi tunayoweza kutumia hapa ni kusema watanzania wamechoka, kwa hivi sasa lolote ni sawa! Maisha yao ni duni nay a kuvunja moyo! Lugha hii ni ngumu kueleweka kwa baadhi ya wakubwa serikalini, na hasa wale ambao kwao huamini kuwa kukosolewa au kuambiwa ukweli ni kudhalilishwa, wanaogopa na kuukwepa ukweli huku watanzania wao wakiendelea kukandamizwa na ugumu wa maisha. Maisha ni magumu kwa wengi wa watanzania! Ni ajabu sana serikali inapojaribu kupingana na watanzania binafsi wananochambua mambo magazetini badala ya kufanyia kazi uchambuzi uliotolewa!

Gharama ya maisha ya mtanzania inapanda bila sababu za msingi za kua hivyo. Tutafakari suala ambalo kwa serikali linaonekana dogo sana lakini linaloumiza watanzania. Suala la kupanda kwa bei ya mafuta na hatimaye kusababisha kupanda kwa nauli. Kwa mawazo yangu kidgo, naanza kuamini kuwa pengine serikali haiwajui vyema watu wake, haijui matatizo yanyowakabili wananchi wake, na ni hatari sana kama imani yangu iko sawa basi hali ni mbaya!

Nimetafakari sana kuhusu mkazi mtanzania wa Bunju ambako kutoka huko mpaka mwenge nauli ni shilingi 400 (kama ni sawa) na kutoka Mwenge mpaka kariakoo anakofanya kazi hotelini na kupata mshahara wa shilingi 30000/= kwa mwezi ni shilingi 250, nauli imepanda huku mshahara wake ukiwa umebaki pale pale, hii ina maana kwamba nauli yake kwa mahesabu ya harakaharaka inazidi mshahara wake kwa mwezi, hapo hajala, hajalipa kodi na ni bachela! Na si kwamba amependa kuishi huko ni mazingira yalimfanya alazimike kuwa huko. Watanzania wa jinsi hii wako wengi sana , wanaendelea kuteseka!

Watanzania kwa njia tofautitofauti waliililia serikali kwamba chonde ifanye linalowezekana kupunguza makali haya, lakini wapi! Wapinzania wakaja na bajeti yao mbadala amabyo mpaka wasomi wameisifu kuwa ni nzuri na yenye kufaa! Swali linakuja, kwa nini serikali inashindwa kuchukua bajeti hii na kuitumia? Je sio utaratibu? Ni kiburi au dharau kwa wapinzania hao? Je tunaendesha serikali kwa manufaa na maslahi ya nani kama si wananchi? Kwa nini tusichukue yale mawazo yanayofaa kwa ajili ya wananchi wetu bila kujali ni chama gani kimetoa mawazo hayo?

Je serikali inaogopa kwamba ikitumia mawazo ya wapinzani itachekwa na kudharauliwa? Kama ndivyo japo hawawezi kukiri hadharani, watazuiaje hisia zetu kwamba wako madarakani kwa maslahi yao na si wananchi?

Mambo mengi yameandikwa, tumeandika hata sisi tusio waandishi wa habari, kwamba watanzania wamechoka na kukata tamaa, kwamba serikali isikilize maoni ya watanzania, hii nchi si ya mtu mmoja, nchi hii ni ya kidemokrasia, serikali ya kidemokrasia ni serikali ya watu, iliyoundwa na watu na kwa ajili ya watu, hili ni muhimu kulikumbuka kila siku, wala tusilewe madaraka na kusahau, kwamba serikali hii ni ya watu, tena kwa ajili ya hao hao watu, wanapolia wasikilizwe, wanapoomba msaada wapewe, maana serikali hiyo haipo kwa ajili ya chama au taasisi Fulani, ni serikali ya watu!

Wanapopiga mayoe ya machungu ya maisha wasikilizwe, si vyema kudhani wananchi wote ni mambumbu, wa kuwaambia ndege inapaa wakati wao situ kwamba haipai, bali pia haionekani machoni mwao. Tukisema hivi tunaweza kuonekana wachochezi na kuanza kutafutwa, kuuliziwa, badala ya kuchukua maoni tunayotoa. Tunaamini kwamba pengine rais au waziri mkuu hajui au haoni kuwa watanzania wana hali ngumu, tunaamini pia kuwa kwa njia hii tunamsaidia!

Narudia kusema kwamba watanzania wote si vipofu, wanaona, si viziwi, maana wanasikia, tatizo si kwamba ni mabubu isipokuwa wamezibwa tu midomo yao wasiseme, wamezibwa kwa kutishiwa hata usalama wao! Hili litaendelea kudidimiza maendeleo ya nchi hii. Tukubali kuambiwa ukweli, na ndio maana tunasema kwamba tunaomba ikibidi sasa itafutwe njia mbadala ya kupunguza makali haya ya maisha kwa watanzania!

Tunapoizungumzia Tanzania hatuizungumzii Dar es salaam, Arusha au Mwanza pekee, tuaihusisha pia Singida, Kigoma, Mtwara, Pemba, na maeneo yote ambayo wengine wanaishi kama vile si watanzania!

Watanzania walioko vijijini ambako hakuna barabara nzuri wanaathirika sana na kupanda kwa bei ya mafuta, bei ambayo kuna uwezekano mkubwa wa kuishisha ilo watanzania wapumue kidogo!

Tafadhali, naandika kwa uchungu, na wala nisiitwe kimbelembele, kwamba najipendekeza kwa watanzania, hapana! Mimi ni mmoja wa watu wanaoathrika na hali hiyo, wazee wangu kule vijijini wanaathirika. Mtu mmoja aalizungumza maneno mazito na ya uchungu sana , alisema hivi “sasa hivi tutakuwa tukizikana kwa simu” alikuwa akiongea hayo baada ya kupata habari za msiba wa ndugu yake, alikuwa akimwambia mdogo wake! Akiwa na maana kwamba hawawezi tena kumudu nauli za mikoani kwenda kuzika ndugu zao!

Serikali isilalie masikio, ahadi zake kwa watanzania ni nyingi mno! Tunaiombea kila la heri isikilize vilio vya watanzania!