Wednesday, May 16, 2007

UZINZI HAUGOPI SIASA WALA DINI YAKO!




Huyu anaitwa mheshimiwa Amina Chifupa, mmoja wa vyanzo vya habari vya makala hii! Hapa alikuwa akila kiapo cha kuwa muadilifu (bungeni)



Nimechukua hatua kuandika makala hii kufuatia matukio mawili yaliyotokea hivi karibuni. Tukio la kwanza ni la Mbunge wa viti maalumu wa UVCC Amina Chifupa wa Mpakanjia, mitaani amepewa majina mengi sana, mengine siwezi hata kuthubutu kuandika hapa. Huyu ametengana na mumewe Mohamed Mpakanjia au Med.

Tukio la pili ni lile la Padri mmoja huko Arusha kutuhumiwa kuhusika na utoaji mamba, halafu walio andika wanasema eti katoa mimba katika mazingira yasiyo safi na salama, kwa maneno mengine mauji ya kiumbe aliyekuwa tumboni yamefanyika katika mazingira yasiyo safi na salama, kwa hiyo kuna dalili kwamba kama mauaji hayo yasingefanyika katika mazingira hayo basi yangekuwa halali.

Hilo sio hoja yetu ya leo, suala ni kwamba Padri Staphene Uhuru alikuwa anashiriki ngono na mwanafunzi wa kidato cha pili wilayani Mbulu, huyu dada sasa ni marehemu. Padri kakiuka maadili ya kikatoliki yanayomtaka kwamba sio kufanya ngono tu bali hata kuoa. Wengi wameshangazwa na tukio hili, tukio hili lina mlolongo. Kwanza jamaa kutembea na kibinti cha kidato cha pili, pili kutoa mimba, tatu mauaji.

Mimi sikushangazwa na lolote kati ya hayo, kwa sababu yako, ni ya kawaida. Waulize wanafunzi watakuambia. Kuna madai kuwa walimu nao hufundisha kwa nadharia na vitendo masomo ya kibaiolojia. Yaani uhusiano wa mwalimu na mwanafunzi haushii katika taaluma tu, bali mpaka kwenye mahaba. Taarifa hizi zipo! Ni unafiki kukataa! Kwa hiyo sio la ajabu mwanafunzi kufanya mapenzi, maana ni kama tabia mashuleni. Kutoa mimba nalo sio la ajabu, tembelea shule za bweni, naambiwa mimba hutolewa mabwenini.

Tujadili kitendo cha Padri kushiriki ngono, wengi niliwasikia wakijadili kama vile ni tukio la ajabu. Walichokuwa wanashangaa sio ngono, walikuwa wanashangaa kwamba Padri kafanya ngono.

Ili mada yetu inoge, turudi kidogo kwa Amina Chifupa, kilichomtenga na mumewe? Amina anadaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Zito Kabwe mbunge wa CHADEMA, Zito mwenyewe amekanusha tuhuma hizo. Vyovyote iwavyo, kilichomfanya Amina apewe talaka ni uhusiano wake usiofaa na Mheshimiwa Kabwe tena huku akiwa na ndoa yake. Tusirefushe mambo, kwenye ndoa ni rahisi kusema amina kaachwa kwa tuhuma za uzinzi, Kwa hiyo Amina anatuhumiwa kwa uzinzi!kwani uhusiano usiofaa wanaouzungumzia ni upi?

Kwamba watu wanashangaa matukio kama ya Amina na yule Padri ni ukweli kwamba binadamu huwa tunasahau kuwa watu kama wanasiasa na viongozi wa dini ni binadamu kama tulivyo, hilo huwa tunalisahau! Kama mchungaji mmoja kule Korogwe alivyo wahi kusema kwamba zamani alikuwa anaamini kuwa Wazungu huwa hawaendi haja kubwa, alisahau kuwa nao ni binadamu kama sisi Wanyakyusa na Wangoni.








Ndivyo ilivyo, tunawachukulia wanasiasa na watu wa dini kama vimiungu kama sio miungu. Eti tunashangaa Padri kuzini, cha ajabu kipi wakati yeye naye ni mwanaume lijali? Tunachoshangaa ni nini kusikia Amina kaachika kwa tuhuma za uzinzi? Mbona Amina kaanza kutuhumiwa toka akiwa Makongo Sekondari, tangu akiwa mtangazaji wa Clouds FM?

Napenda nikukumbushe kwamba suala la ngono (sio mapenzi, mapenzi ni ya wanandoa) haliko kama wengi wanavyodhani, kama ni mchzo, basi ngono ni wa aina yake! Ngono(uzinzi) si tabia kama unavyoweza kufikiri! Ni muhimu kuelewa kwamba mtu mzinzi ni mzinzi hataka kabla hajalala na mwanaume au mwanamke ambaye si mkewe/mumewe. Kama alivyo mwizi, hawi mwizi baada ya kuiba, huwa mwizi hata kabla hajaiba na muongo vivyo vivyo! Ndio maana naamini kwamba mzinzi hafugiki hataka kama ni mkeo au mumeo, uzinzi ni ugonjwa, ni kichaa cha kiwango cha juu sana.

Asipozini kwa kulala na mwanaume/mwanamke, basi atazini katika akili au moyo wake, ndio maana Yesu alitangaza

“Mmesikia kwamba imenenwa Usizini. Lakini mimi nawaambia, kila mtu amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amkwisha kuzininaye moyoni mwake”

Mathayo 5:27-28 Upo mpaka hapoo?? Kuzini ni kitendo kinachoanzia moyoni, moyo ambao kila mwanasiasa anao, kila shehe na kila mchungaji anao.

Ninachotaka kusema hapa ni kwamba, uzinzi ni roho au roho chafu (evil spirits) inayotenda kazi ndani ya mtu. Roho ninayoizungumzia hapa si ule uhai wa mtu. Kwa imani yangu mimi (Mkristo) kuna kiumbe kinaitwa Ibilisi, yeye huwa na idara katika utendaji wake. Kwa maneno mengine, zile idara ni mawakala wa Ibilisi duniani. Kazi ya mawakala hawa ni kuhakikisha kwamba mwanadamu anakwenda kinyume na kila kilichoagizwa na Mungu. Mawakala hawa pia huitwa pepo wachafu (demons) hutmia nguvu za kishetani (demonic power) kufanya kazi ndani ya mtu bila kujali hadhi au cheo chake ndani ya jamii. Ndio maana sio ajabu Stephen Uhuru kuzini japo ni Padri ambaye akiwa madhabahuni husimamisha mishipa kuwataka watu waache uzinzi. Sio ajabu kumkuta Shehe akifanya zinaa na mke wa jirani yake japo hukauka koo akiwataka watu kuacha maovu, na sio ajabu tena kumkuta mwanasiasa bila haya usoni akituma dereva wake kwenda shule moja wapo ya sekondari ili akamtafutie binti wa kuvinjari nae! Sio ajabu, maana kuna roho inatenda kazi ndani yake.

Nimekwambia Ibilisi ana mawakala, hawa hufanya kazi tofauti tofauti, kuna wale wanohakikisha binadamu anakuwa mdhulumaji au wezi, ndio maana sio ajabu kukuta wanasiasa wezi, wanaowaibia wananchi wao, ni roho! Kuna mawakala wa ibilisi wanaohakikisha kuwa watu wanakuwa wanafiki, wafitini, wagomvi na wazinzi! Mawakala hawa ni kuhakikisha kuwa mwanadamu anakwenda kinyume na kila jema aliloagiza Muumbaji wa Mbingu na nchi.

Ndio maana kwenye Warumi 8:6-7 inasema

“Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani. Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kutii”

Mwanadamu ana roho na mwili, mwili una nia ya mauti, na ndio maana tunauzika ardhini, na tunaamini pia kuwa roho inapaa na kwenda kwa Mungu aliyeiumba.

Soma na hapa tena Wagalatia 5:17

“Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka”

Bila shaka unaanza kupata picha ya kile ninachotaka ujue. Kwamba mara nyingine watu hufanya uzinzi si kwa sababu wanapenda, ni kama kitu Fulani huwapekesha ndani. Na mujibu wa Biblia, Mungu alijua kuwa hii miili ina matatizo yake, hata hivyo hakuhalalisha dhambi kwa kigezo kwamba miili ina matatizo, bali amesema

“Kila mmoja wenu (nikiwemo mimi) ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima, si katika hali ya tama mbaya kama mataifa wasiomjua Mungu” 1Wathesalonike 4:4-5
“Basi nasema enendeni kwa roho, wala hamtazitimiza kamwe tama za mwili” Galatia 5:16

Wengine hufikiri kwamba watu hufikia hatua ya kufanya uzinzi ili kujipatia kipato, hii ina maana kwamba wale wenye kiapato kizuri hawafanyi uzinzi. Hapana! Ukitaka kuamini, mchukue binti yako, mpe kila kitu nyumbani kwako, mpe gari ya kutembelea, mwekee viyoyozi kuanzia sebuleni, chumbani, stoo, jikoni mpaka chooni! Chukua pesa ndio ziwe zuria la nyumba nzima, au mpe pesa ziwe mataulo ya kujifutia baada ya kuoga.

Mpe pesa zingine ziwe vitambaa vya kushonea nguo zake za kuvaa, au ziwe leso za kuvutia jasho baada ya mazoezi ya viungo. Kwa kufupisha, muulize mahita ambayo anadhani akipata ataridhika kuwapo duniani, kasha mpatie, mi nakwambia kama na ile roho, hatachukua hata siku mbili, kwanza ataona pesa ulizo mpa ni utumwa!

Hii ni kukuonesha kwamba, uzinzi si tabia kama tabia zingine, ni roho inayofanya kazi kuupelekesha mwili, ndio maana nikasema, mtu huweza kuwa mzinzi hata kama hakutaka kuwa hivyo!

Tukirudi kwa upande wa Amina na yule padri sasa utaanza kuelewa kwa nini nilikuambia uzinzi haujali hadhi ya mtu katika jamii yake. Yalimpata Bill Clinton wa Marekani, mtu aliyeheshimika dunia nzima. Kama utakuwa unafahamu siri hutashngaa kwamba kwa nini na wao hufanya uzinzi.

Kuna watu walifikiri kuwa kuoa ni suluhisho, kwamba wataacha tabia hii chafu watakapopata waume au wake zao. Ndugu zangu waislamu, sheria zao zinaruhusu kuoa mke zaidi ya mmoja, lakini wataniunga mkono nikisema kwamba bado kuna wanaotoka nje ya ndoa, wapo wanaobadili wanawake kama mashati. Wanawake nao hawako nyumba katika mchezo huo, bila haya mtu huweza kuchukua mume wa mtu na kuishi naye, na mwanaume kuacha mke na kutembea na mwanamke mwingine. Hili lipo katika jamii, watu wanafikiri ni tabia ya kawaida kama ilivyo tabia ya watanzania kuwakarimu wageni au wachaga kupenda mtori!

Ni idara maalumu ya Ibilisi inayotenda kazi ndani ya watu, ni kampeni ya Ibilisi kwa kila mtu ili tuache kuyafanya ya mwenyezi Mungu. Hata hivyo hatuwezi kuendelea kuwa wazinzi kwa kisingizio kwamba sio sisi bali ni Ibilisi. Wakati wa kushiriki tendo hilo hakuna ambaye anakuwa hajui kuwa anafanya nini, kila mtu anajua, au kama ni mawazo ni wazi kwamba kila mtu anakuwa anajua anawaza nini. Kumbuka tulivyosoma hapo juu, haya ni mashindano ya mwili na roho, ni vita kali roho inasema sitaki, mwili unasema nataka, Biblia imetuapa jibu kwamba tusienende kwa mwili bali kwa roho, tena tumeambiwa kwamba kila mtu ajue kuuweza mwili wake!

Nina ujasiri wa kutumia Biblia hapa kwa sababu huwa naamini kuwa Biblia sio ya wakristo peke yao, ni ya waislamu pia, ndio maana hutumika kuwazodoa Wakristo kwenye mihadhara ya Kiislamu, na mara nyingine nimesikia ikisomwa misikitini! Si sahihi kwa Wakristo kusema Biblia ni mali yao! Tunapaswa kushinda!

Hebu soma kipengele hiki ambacho Mungu alikuwa akizungumza na mtoto wa mwanadamu wa kwanza, yaani Adam, mtoto huyu aliitwa Kaini.

“Kama ukitenda vyema, je hutapata kibali? Usipo tenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde” Mwanzo 4:7

Unaona hapo? Kumbe dhambi ipo, inaweza kumuotea mtu (kummendea, kumvizia ili imshinde) pia dhambi inaweza kumtamani mtu kwa lengo la kumfanya ashindwe kufanya yaliyo ya MUNGU, kama inaweza kutamani maana yake ina tambuzi wa namna Fulani, ndio maana nikakwambia, dhambi ni roho inayotenda kazi. Pamoja na hayo, bado Kain anaambiwa inampasa kuishinda. Kwa nini? Alikuwa anajua anachofanya tangu alipokuwa anawaza.

Kaini alikuwa anapanga kumuua ndugu yake aliyeitwa Habili, tayari Mungu aliliona hilo, akamtahadharisha Kaini juu ya kile alichotaka kukifanya, kwamba kilikuwa ndani yake ndio, kiliingia pengine bila Kaini kupenda, hilo halina ubishi, lakini alipaswa kushinda! Tukijaaliwa siku moja tutaangalia namna tunavyoweza kuushinda uzinzi!

0713 550 778

ilovejesustz@yahoo.com

NITAWAAMBIA NINI WANANGU?

Hawa ni wanasiasa, Freeman Mbowe wa CHADEMA na Jakaya Kikwete wa CCM


Hawa ni wanasiasa, kutoka kushoto ni mzee Mkapa, anayefuata ni Mzee mwinyi na kulia ni Kikwete, wale wengine kule nyuma, sio siri siwajui! nasema sio lazima wote tuwe wanasiasa ndipo tuijenge nchi yetu, kila mmoja anayo nafasi yake kuijenga nchi hii. Zaidi ya hapo ni kukwepa majukumu!




Wiki iliyopita sikuonekana kwenye ukurasa huu, pamoja na sababu za kiufundi, hofu, mashaka na wasiwasi pia vilichangia mimi kutokuonekana. Hii ilitokana na makala niliyo andika wiki mbili zilizopita, iliyokuwa na kichwa “NIMEMUHUTUBIA RAIS KIKWETE” Makala nyingi nilizoandika watu walinitumia ujumbe kunipongeza na kutoa maoni yao, wengine waliniponda, haya ni ya kawaida.

Makala ya wiki ile hakuna aliyenipongeza wala kuniponda, waliosoma na kunitmuia ujumbe wote walinipa ujumbe wa masikitiko, wengi walinitahadharisha kwamba ninakoelekea ni kufungwa au kuuwawa. Mmoja alifika mbali na kusema tuombe wiki ipite salama bila kufanywa chochote.

Yuko mwananchi mwingine yeye alinitahadharisha kuwa naweza kufanyiwa hujuma na kusababisha nikakosa masomo, kwamba makachero wa serikali watafanya kila wawezalo ili kuniharibia masomo, kisa! Eti nimemwandikia rais.

Nimeirudia ile makala tena na tena kujaribu kuona lugha ya dharau ua matusi niliyomwandikia mheshimiwa rais sikuiona, nimetafuta maneno makali yaliyowafanya wasomaji wangu wanionee huruma. Mwandishi mmoja wa habari wa siku nyingi nchini aliniambia baada ya kusoma makala ile alisema, nina umri mdogo sana kiasi cha kushindana na rais, sijui alipata wapi taarifa kwamba nashindana na rais. Anasema hivi huku nikiwa sioni wapi niliposhindana na rais katika makala ile.

Kwa ufupi vitisho vile vilidhoofisha hali yangu ya kuandika makala. Hata hivyo leo nataka nizungumzie kwa nini naandika makala. Wengi pengine hawajui akiwemo rais na serikali yake kama huwa anasoma makala zangu. Wakiwemo pia wananchi wa Tanzania.

Kuna dhana kwamba kila anayeandika makala ya kuikosoa au kupinga maamuzi mabovu na ya kidhalimu ya serikali basi ni mpinzani, wengine hufika mbali na kuniona kama mwanachama wa chama kimojawapo cha upinzani nchini. Wapinzani nao kuna kipindi walidhani mimi ni CCM baada ya kutoa makala yangu ya januari 22 mwaka huu.

Niliandika makala ile kuwataka viongozi wa vyama vya upinzani kuacha kuwa ving’ang’anizi badala yake wawachie damu changa vyama, maana baadhi ya viongozi hao waliopo sasa, kuna kila dalili ya wao kushindwa kuviongoza vyama hivyo na hivyo kuvipeleka vyama hivyo mrama.

Huwezi amini, nashukuru kuwa makala ile imefanya kazi, juzi Mbatia anatangaza kuwa yeye hakuzaliwa kuwa mwenyekiti wa NCCR-MAGEUZI, kwamba yuko tayari kuwaachia watu wengine kuongoza. Katika makala ile niliwataja watu kama Ibrahim Lipumba, Seif Sharif Hamad na Agustine Mrema.

Ndugu zangu watanzania, napenda ifahamike kuwa mimi nimewahi kuwa CCM, nab ado niko CCM kinadharia tu, maana sijarudisha kadi, nilizaliwa CCM, babu yangu alikuwa Mbunge wa Mbeya mjini kwa CCM, na siku za mwisho za uhai wake aliwahi kuniambia kuwa angefurahi kama ningekuwa mrithi wake kisiasa katika kizazi chake. Huyu ni Mzee Benson Obed Mwamfupe.

Hata kama ningekuwa mwanachama hai wa CCM bado si haki kukaa kimya pale inapoboronga na kuwatendea ndivyo sivyo watanzania. Maana hii nchi si mali yetu wana CCM, ni mali ya Watanzania, na nirudie kusema kwamba, sio ajabu siku moja wembe ule uliowanyoa KANU kule Kenya utakuja kutunyoa wana CCM.

Siandiki makala kuchekesha watu, siandiki kuwafurahisha wapinzani wala CCM. Dhamira yangu itanisuta nikifanya hivyo, nafsi itanishitaki. Naandika makala kuwahabnarisha watanzania na kuwaelimisha pia. Rejea makala yangu ya rushwa ambayo nililenga kuwaelimisha watanzania kuhusu mapambano ya rushwa, kama ni kutetea niliitea CCM katika makala ile. Ilikuwa na kichwa cha “Mapambano ya rushwa na unafiki wa watanzanzania” Kamwe siangalii upande mmoja, sikuzaliwa kumsema Kikwete wala kumkosoa, kwanza sikujua kama Kikwete angekuja kuwa rais wan chi hii, na wala Kikwete hakuzaliwa ili awe rais wan chi hii, lakini maadam ameingia Ikulu hawezi kukwepa vitu ambavyo mtu wa kawaida anaweza kuvikwepa.

Ngoja nikwambie tena kwa nini naandika makala. Kama wewe ni msomaji wa safu hii utakumbuka kuwa niliwahi kuwaambia watanzania kuwa sio lazima wote tuwe wanasia ndipo tulete maendeleo nchini, kama ingekuwa hivyo basi ilitupasa wote tuwe marais wan chi hii, wabunge wa majimbo yetu au madiwani wa kata zetu. Ingekuwa vurugu, pasingekalika.

Kukawa na rais mmoja, huyu tumempa dhamana ya kutuongoza na kutufikisha kule tunakotaka. Lazima ifahamike kwamba kapewa tu dhamana! Pamoja na kwamba tayari anatembelea magari ambayo ni ukweli usiopingika kwamba kuna watanzania watakaokufa sio tu bila kuyapanda, pengine bila hata kuyaona. Anavaa mavazi ambayo yako tofauti na watanzania wengi vijijini, anakwenda nchi ambazo kuna watanzania wamenyimwa kwenda na tofauti nyingi alizo nazo na watanzania wengine bado lazima tukubaliane kwamba hii nchi Kikwete haiwezi peke yake, si Kikwete tu, bali rais yeyote atakayekuja, hata angekuja kuwa rais baba yangu mzazi, ukweli huu alipaswa kuufahamu.

Rais ni mwanadamu, hili wengi tunalisahau mara nyingine. Rais kuna siku atakaufa kama nitakavyokufa mimi Daniel na kuzikwa kama walivyozikwa wengi duniani. Mazishi ya kupigiwa mizinga na mbwembwe zingine hazitamfanya arudi duniani, wakati wake utakuwa umekwisha, sababu ni moja, yeye ni mwanadamu kama mimi na wewe.

Ubinadamu huo ndio unaomfanya ahitaji msaada wa wengine kumsaidia katika kutekeleza majukumu yake. Ndio maana akahitaji makamu wa rais, akahitji kinja mkuu wa mawaziri wake, akahitaji wakuu wa wilaya na mikoa. Hii inadhirisha kwamba yeye peke yake hawezi.








Ni vizuri pia kufahamu kwamba hata hao wasaidizi wake wanahitaji wasaidizi, ndio maana kuna waandishi wa habari ambao watawapa taarifa zitakazowafanya watekeleze majukumu yao kiufanisi. Pengine wawe na kiburi cha kujifanya wanaweza kila jambo, kuwaona waandishi kama wachochezi na wambea. Tabia hii inafanya nchi hii kubaki nyuma daima. Taarifa za kuvitisha vyombo vya habari kwa sababu tu wao ndio walioshika dola haitaijenga kamwe nchi hii. Ndio maana naomba sana, vyombo vya habari vitangazwe rasmi kuwa mhimili wa nne wa serikali.

Ukweli kwamba Kikwete hawezi nchi hii peke yake ndio inayonifanya niandike makala, siandiki kumdhalilisha, naandika kumsaidia, hata kama kumkosoa, kwani ni uhalifu kumkosoa mtu, je ni dhambi kukosolewa? Kwa lugha ingine, kukosoa kuna maana ya kurekebisha na kuonyesha njia sahihi. Wanaokosoa sio lazima wawe wanasiasa, naweza nikawa mwananchi wa kawaida kama mimi, ili mradi tu ninajua kile ninachofanya.

Kuwa rais au waziri hakumaanishi kwamba tayari unajua kila kitu, una wezo wa kila jambo duniani, ndio maana kuna haja ya kuwaweaka washauri. Naamini kuna watanzania ambao hawatakaa waje kuwa marai wa nchi hii, lakini wenye mawazo ya kujenga nchi, ikiwa tu wanaoshauriwa wasiwe na wivu, kwamba kufanyia kazi ushauri wa wengine ni kuonyesha udhaifu. Huu ni upotofu.

Nilipozungumza na katibu mkuu wa NCCR-MAGEUZI aliniambia kuwa Mwenyekiti wa chama hicho bwana James Mbatia ndie aliyetoa wazo la kuanzishwa kwa mfuko wa elimu Tanzania, na mfuko huo ukaanzishwa na serikali. Kimeharibika nini kwa hao waliotekeleza wazo hilo? Je si maendeleo kwa taifa letu?

Ni muhimu kufahamu kwamba binafsi hatuandiki makala kwa sababu tunapenda sana kuandika, au tunanogewa kufanya hivyo, asikudanganye mtu, kuandika si kitu rahisi kama unavyoweza kudhani, ni ngumu sana, Mheshimiwa Mkapa atakuwa anaelewa vizuri jambo hili!

Kuandika kunakufanya wakati mwingine uishi maisha ya hofu, maana hujui nani ni nani, hujui nani anakuja kwa jema. Tunaogopa mpaka wageni nyumbani wakati mwingine. Maana zinakuja sura ambazo hujawahi kuziona, halafu unaulizwa, wewe ndie Daniel? kujibu uongo siwezi inabidi niseme mimi ndie! Kisha anasema samahani, ninashida na wewe, nataka tuongee pembeni! Naanza kupata wasiwasi, anasema nimetumwa na kaka nanihii anasema muazime shilingi 5000/= Aah! Mimi nilidhani tayari wametumwa kuja kuni…………

Jamani naandika makala kwa lengo la kuelimisha wananchi, kukosoa ni haki yangu kama mwananchi. Kwa nini niache nchi yangu iende mrama wakati uwezekano wa kuokoa jahazi? Nitawaambia nini watoto na wajukuu wangu watakaponiuliza sababu za sisi (kizazi hiki) kushindwa kuijenga nchi? Si bora mimi nitakuwa na la kujitetea kwamba niliandika gazetini, lakini walilalia masikio, walibeza makala zetu, walitutisha na kutaka tufunge midomo.

Naandika makala kuenzi wana harakati wa zamani wakina Martin Luther King Jr. Sio vizuri kwa watawala kudhani kila anayeandika kukikosoa ni wapinzani au wanasiasa. Badala ya kuwatishia waandishi wakae nao na kwarekebisha au kukanusha kilichoandikwa. Hata kama itatokea watawahujumu waandishi kwa siri na umma usijue, ipo siku gharana hiyo italipwa, kuna siku watazaliwa upya wale waliouwawa.











Nguvu ya kalamu ni kubwa kuliko mitutu ya bunduki, kuliko sumu kali kama ya pakanga. Kalamu huchukiwa na wengi, nami naitumia kwa kadri Mungu anavyonipa fursa ya kufanya hivyo. Naandika makala hii si kwa lengo la kushindana, naandika kwa lengo la kuelimisha, kwamba wajibu wa kujenga nchi ni wetu wote, na sio watawala peke yao. Sio kina Lipumba, Mrema, Mbowe, Sharif, Duni, Mtikila, Makamba, Kikwete peke yao.

Nchi hii inajengwa pia na mkulima wa karafuu na miogo kule Pemba, inajengwa na mkulima wa chai kule Amani- Tanga na Rungwe Mbeya, inajengwa na mkulima wa korosho kule Mtwara na waandishi kama mimi hapa. Nipewe nafasi tu hasa ile ya kukosoa kila inapobidi na kupongeza kila inapostahili.

Kwa nini? Ukiwa kiongozi ni vigumu kuona madudu unayofanya, hii inatokana na ukweli kwamba madaraka yanalevya, yanapofusha macho, huoni, unahitaji wenzako walioko nje wakupe japo ushauri kuwa pengine unaelekea shimoni, uwe mwepese kusikiliza na kukubali kuutafiti ukweli wa mambo. Usifanye tu vile akili inakutuma, akili ishirikiane na macho, macho tunaweza tukawa ni sisi tunaondika makala japo hatuna taaluma hiyo, lakini tuna maoni na ushauri unaoweza kufaa.

Nafanya hivi si kwa ajili yangu tu, naangalia pia vizazi vijavyo, naangalia watoto wangu, nisipoijenga mimi wataathirika wao, hata kama sitafanikiwa mimi, nitawaambia nao wajenge kwa ajili ya wajukuu zangu (watoto wao) na siku moja itafika mambo yatabadilika.

Naandika, kwa sababu naogopa nisije nikakosa cha kujibu watakaponiuliza siku moja, nawaza watauliza hivi “baba nani aliiharibu nchi hyetu” Kama ni wewe unaulizwa, utamtupia nani lawama? Utasema ni Mkapa alitumia vibaya pesa zetu kwa kununua ndege na rada (si ndivyo tunavyomlaumu mzee wa watu) au nitasema ni Kikwete? Kwa kusema watendaji wake walitumia vibaya pesa za walipa kodi? Au ni Mwinyi aliyeiuza Loliondo, kwamba kama aliweza kuuuza Loliondo basi hakushindwa kuuza migodi na mashirika?

Watauliza ninyi mlikuwa wapi? Je, nitasema sikuwa kiongozi? Aah wapi! Bora nije niwaambie kuwa niliandika sana kwenye gazeti la Fahamu, na kwenye blogu yangu uzuri wenyewe wataiona, maana blogu inatunza kumbukumbu zote, naamini watanisamehe na kunitakia safari njema ya kurudi nyumbani, Mbinguni. Wewe utawajibu nini wanao na wajukuu zako? Kwa jinsi tulivyozoea kujitetea kwa uongo, si ajabu utawaongopea watoto wako!

Lakini kwa nini usiwaambie tu ukweli kwamba ulipokuwa askari wa usalama barabarani ulishiriki rushwa, ulipokuwa usalama wa raia ulibambikizia watu makosa kusudi wakuhonge? Kwa nini usiwaambie tu ukweli kwamba ulipokuwa ofisini ulikuwa unafanya kazi kwa masaa mawili, kupiga soga (tena za umbea) masaa sita na kuzurura masaa yaliyo baki. Kwa nini usiwaambie tu kwamba serikali ilipopiga marufuku taka zisitupwe hovyo mitaani wewe ulikaidi?

Mbona usiwaambie kwamba ulipokuwa nesi au daktari ulisababisha vifo vingi vya watu ambao wangejenga nchi hii baadae? Je utawaambia ukweli kwamba ulishiriki kuuwa raia wasio na hatia kwa sababu tu waliandamana kudai haki zao? Je utathubutu kuwaambia ukweli kuwa ushindi wa chama chenu ulikuwa si wa halali, kwamba mulikiibia kura chama kingine? Je utasema hayo?
Utawaambia kwamba muliiba mafuta kwenye magari ya Wizara na au shirika na kwenda kuyauza kwa sababu ya ubinafsi ulionao, kwamba hukujua kuiba kwako kumeleta madhara mpaka kwa watoto wako hao?

Utawaambia nini watoto wako? Usipowaambia ukweli kuna hatari kwamba nao watakuwa wezi na wahujumu kama wewe. Ninachotaka nikwambie hapa ni kwamba kila mtanzania kuanzia viongozi wa serikali mpaka raia wa kawaida wameshiriki kwa njia moja au ingine kuharibu kwa kuihujumu nchini hii hasa wanasiasa na matapeli wachahe kwenye idara za serikali.

Mwenzako naandika leo, kukusadia wewe na mimi, labda ushupaze shingo. Naongea na wewe Elizabeth David, una wajibu wa kuijenga nchi hii! Nisipo fanya hivyo nitakuwa sina cha kujitetea kwa watoto wangu na vizazi vijavyo. Wewe nawe cheza katika nafasi yako, acha kuhujumu nchi hii, sio mali yako peke yako, uwe na haya, uone aibu! Naongea na wasomi na wasio wasomi, naongea na Rais mpaka raia wa kawaida.

Mungu ibariki Tanzania, bariki vizazi vijavyo!

0713 550 778
ilovejesustz@yahoo.com