Tanzania ilipata uhuru lini na kutoka kwa nani?
“Mnamo tarehe 30/06/07 kamati kuu ya utendaji ya Tanzania Association ilikuwa na kikao katika ofisi zake za muda zilizopo huko Tottenham London.Kati ya mengi yaliyojadiliwa ilikuwa ni kuadhimishwa kwa siku ya uhuru wa Tanzania na watanzania waishio hapa UK”
Hiki ni kipande cha taarifa ya Jumuiya ya Watanzania waishio nchini Uingereza kwenye mtandao. Angali kwa makini lile neno nililolikoleza kwa wino mweusi. Nilishtuka, nikajua kwa vyovyote kuna watanzania wengi wanaweza kuwa wanafikiri hivyo, kwamba Tanzania inasheherekea uhuru wake. Na hapa napenda ifahamike tu natoa maoni yangu ikiwa ni moja kati ya kusheherekea siku hiyo ya uhuru!
Siko hapa kuwabeza wala kuwadharau wale wenye mawazo kwamba Tanzania inasheherekea siku ya kupata uhuru! Kukaa kimya kunaweza kuchangia kuendelea kupotoshwa kwa historia, kwa hivyo kwa kutumia hekima, uungwana na busara ni vizuri tukakumbushana yale yaliyo ya muhimu kwa ajili ya historia ya nchi yetu.
Swali linaanza hivi, Je, ni kweli tunasheherekea uhuru wa Tanzania? Kuna ukweli hapo kihistoria? Ili kulijibu swali hili hebu tuanagalie maana ya Tanzania.
Tanzania ni muunganiko wa majina mawili ya zilizokuwa nchi mbili, yaani Tanganyika na Zanzibar. Nchi hizi mbili ziliungana mwaka 1964 na kuunda Jamhuri ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo baadae ikaitwa Tanzania. Ikumbukwe pia kwamba, kabla nchi hizo hazijawa nchi moja Tayari Tanganyika iliyokuwa koloni la Mwingereza ilikuwa tayari imepata uhuru wake mwaka 1961, miaka miatatu kabla ya muungano huo.
Kwa hiyo wakati Tanganyika inapata Uhuru, nchi au kitu kinachitwa Tanzania hakikuwepo/haikuwepo. Zanzibar yenyewe ilikuja kupata uhuru wake kutoka kwa Sultani mwaka 1964 kwa njia ya mapinduzi. Kwa hiyo siku za uhuru wa Tanganyika kama nchi, na Zanzibar kama nchi pia ni tofauti. Kwa kusheherekea, Tanganyika ina siku yake ya uhuru na Zanzibar vivyo hivyo.
Kwa huoni kuwa kuna walakini kusheherekea uhuru wa Tanzania ambayo haijawahi kutawaliwa? Unapozungmzia Tanzania unazungumzia Tanganyika na Zanzibar, kwa nini tusheherekee uhuru wa nchi mbili tofauti, zilizopata uhuru kwa miaka na tarehe tofauti kabisa.
Sisemi haya kwa nia mbaya, ni kwa ajili ya wale wanaodhani tunasheherekea uhuru wa Tanzania. Hebu soma hii nayo hapa;
“Kuelekea maadhimisho ya miaka 47 ya Uhuru wa Tanzania Bara na 46 ya Jamhuri nimepata wazo. Angalia yale maneno yaliyokolezwa. Ni wakati wa kuiinua bendera yetu juu kama ishara ya umoja wetu na kama ishara ya utaifa wetu”
Huyu ni mchambuzi mahiri wa masuala ya kijamii hapa nchini, yeye anaishi nchini Marekani kwa sasa, anaitwa M. M. Mwanakijiji. Yeye kasema wazi kuwa ni uhuru wa Tanzania Bara, ni bora. Lakini hata hivyo kuna nchi inaitwa Tanzania Bara? Hili tuliache, tutalijadili wakati mwingine tukijaaliwa.
Kuna wakati niliwahi kusoma uachambuzi wa mwandishi fulani akihoji kwa nini historia ya Zanzibari inapotoshwa kuhusu mapinduzi, nadhani pia naanza kuona kuwa kuna mambo tukikaa kimya bila kuruhusu mijadala yenye kujenga tutaipoteza historia halisi na maana ya uhuru tulioupata.
Mwaka jana niliwahi kuhoji kwa habari hii ya Tanzania kuwa na sherehe za uhuru, lakini sikuzama kwa undani hivi, lengolisema hivi “Hivi ni uhuru wa Tanganyika au Tanzania ? Kwani Tanzania iliwahi kutawaliwa na nchi gain. Eti kwa mujibu wa walimu wang wa historian a kumbukumbu zangu, Tanganyika (si Tanzania ) ndio iliyopata uhuru mwaka 1961. Ni haki yangu kuhoji swali hili, ni muhimu, historia isipotoshwe. Naomba mhariri aruhusu mjadala katika hili. Kwa nini tusheherekee uhuru wa Tanzania badala ya Tanganyika ?” kama nilivyokwisha kusema kabla ni kuibua mjadala ili tuone kama tuko mahali sahihi au tumejisahau.
Bado swali langu liko pale pale, Tanzania kwa maana ya nchi, ilipata lini uhuru? Ilitawaliwa na nani? Kwa nini navyofahamu mwaka 1961, Tanzania ilikuwa haijazaliwa bado, kwa wale wanaotumia neno Uhuru wa Tanzania waache kufanya hivyo, kwani ni kupotosha historia, Tanzania haijawahi kuwa Koloni, Yaani tangu Tanganyika na Zanzibar ziungane na kuwa nchi moja, nchi hiyo (Tanzania) baada ya mwaka 1964 haijawahi kuwa chini ya Ukoloni.
Pengine kama tuna maana ya ukoloni wa kimawazo (kifkra) na kiuchumi, kwamba bado tunatawaliwa kiuchumi na kifikra na mataifa ya Magharibi. Ndio maana tunaendekeza hadi lugha yao na kuona kiswahili ni takataka na laana kwetu. Ndio maana asilimia 40% ya bajeti yetu tunategemea kutoka kwao. Hata kama ndivyo, kwamba tunatawaliwa kiuchumi na kifikra je uhuru tumeupata? Lini, tarehe ngapi?
Lakini pia hivi hamfikirii kwamba kuendelea kusheherekea uhuru wa Tanganyika ni kuendelea kuitambua Tanganyika? Wana makosa gani sasa wakina Mtikila wanapojinadi kuwa wao si watanzania, bali watanganyika? Kwa nini tusisheherekee tu uhuru wa Tanzania kama upo au tubakie tu na sherehe za Muungano ambao nao una mkanganyiko?
Chonde ndugu zanguni, popote mlipo,lengo langu ni kuwakumbusha wale wanaopenda kutumia neno uhuru wa Tanzania badala ya Tanganyika, na tena nimesema kwamba kama tunasheherekea uhuru wa Tanganyika ina maana kwamba tunakiri na kuungana na kina Mtikila kwamba bado kuna nchi inaitwa Tanganyika, je Katiba inasemaje? Je tuna katiba ya Tanganyika bado? Siku moja nitaleta uchambuzi kuhusu suala la Muungano, ili ujue kwamba kuna mambo mengi bado tunayafanya lakini huku tukiwa hatuelewi bado maana yake au yakiendelea kutuchanganya! Lazima tufanye haraka kurekebisha ili vizazi vijavyo visije vikatuhukumu.