Monday, June 18, 2007

TUKIAMUA KUWA WAZALENDO MTASTAHIMILI?

Ni rahisi sana kwa watawala wetu kama hawa wakisisitiza uzalendo kwa wananchi, kuna maswali kidogo nataka kuhoji hapa!

HIVI TUKIAMUA KUWA WAZALENDO, WANASIASA NA WATAWALA WETU WATASTAHIMILI?

.Je wanajua gharama ya uzalendo? Au wanasema tu?

Hala..hala wanasiasa mnapokuwa majukwaani. Jichungeni na kauli zenu. Muwe mnasema mnayomaanisha na kumaanisha haswa yale mnayoyasema!

Ndugu msomaji nimeamua nimejikuta nakuwa mkali tu leo, na si ajabu nikaitwa mbwatukaji, eti nabwatuka! Nambwatukia nani wakati mimi natoa elimu hapa? Nimeamua kuwa mkali kwa sababu sio siri kuna kauli na matamshi ya wanasiasa yanakera sana. Yanakera hasa unapozilinganisha kauli hizo na utendaji wake (wao?)

Hivi umewahi kuhudhuria mikutano, warsha, semina au nini zile…..? ‘Workshop’ za hasa wasemaji wakuu wanapokuwa wanasiasa? Hebu fikiria wito kama huu unaotolewa na huyu mheshimiwa nanihii…anasema “kwa hiyo nawaomba sana ndugu wananchi, muwe na moyo wa uzalendo kwa Taifa lenu” Mwingine najionyesha kuwa makini zaidi kwa kusema “unajua wakati umefika wa kuwa wazalendo” Msikilize na huyu anasema “eeeh!..uzalendo ni kitu muhimu sana kwa raia yeyote na wa taifa lolote kwa nchi yake”

Ni mahodari kweli wa kutoa matamko, kasheshe ni pale unapowadai watekeleze kauli zao kivitendo. Waambie waanzishe mitaala ya kufundisha uzalendo mashuleni, angau shule za chekechea tu, utapewa kila jina watakalojisikia kukupa au lile lililo rahisi kutamkwa na vinywa vyao.

Wengi wanato wito kwa wananchi kuwa wazalendo wakiwa hawajui gharama ya uzalendo pale wananchi wanapoamua kuwa wazalendo. Wanatunga mamba kwa hiari yao, lakini huwa wanakikimbia kile kinachozaliwa. Siwezi kuzungumza hapa leo ikiwa watanzania ni wazalendo au sivyo, isipokuwa, ukitaka kujua ukeli wa jambo hili angalia viongozi wa Tanzania, ung’amue ikiwa wao ni wazalendo au la!

Kwa ninavoelewa mimi uzalendo kwa lugha rahisi inayoweza kueleweka na kila mmoja ni hali ya kuwa na mapenzi ya dhati kwa nchi yake, si vibaya nikaongeza kwa kusema kuwa mtu mzaleno huwa tayari kujitoa mhanga kwa ajili ya Taifa lake, hasa pale linapohujumiwa bila kujali anayelihujumu ni nani na anatoka wapi!

Wanasiasa na watawala wanataka tuwe wazalendo, je watakuwa tayari kulipia gharama hii? Gharama ya watu hawa kujitoa mhanga kuijenga nchi yao? Nauliza hivi kwa sababu kuna mazingira yanaonesha kwamba watawala wengi hawapendi sana wananchi wawe na ufahamu wa kuelewa mwendo wa jinsi nchi yao inavyokwenda. Mwenendo wa watawala wao walivyo, ni haki yao maana waliwaweka madarakani, na mishahara yao ni kodi za wananchi!

Ngoja nitoe mawazo yangu hapa kuhusu wazalendo tunachoweza kukifanya tukishakuwa wazalendo. Mnatuambia tuwe wazalendo haya yafuatayo mtayaweza au ndio kule tunakodhani sisi watawaliwa ni janja ya maneno? Hata hivyo ikumbukwe kuwa kama wananchi hudhaniwa kuwa vikaragosi, wasiolewa mambo, mambumbu hawatabaki kuwa hivyo walivyo daima, kuna siku wataamka.

Uzalendo ambao wanasiasa wanatuhimiza sisi wenye nchi hii kuwa nao ni pamoja na kudai ahadi walizotuahidi wakati wa uchaguzi. Je watastahimili? Siku ambapo watakuwa wanapita na misafara ya utitiri wa magari yao kwenye majimbo yetu, watakubali tuwasimamishe, tuwaulize ahadi yao ya kutuletea maji jimboni iliyeyukia wapi na vipi? Watakubali tuwahimize kuwa muda unakwenda na hakuna lolote linalofanyika? Kusimamisha msafara jimboni tukiamua kuwa wazalendo haitakuwa na maana ya kuwakosea wakuu wetu adabu, itakuwa ni kujitoa mhanga wa kuwaonyesha kuwa tumeamua kuwa wazalendo na sio kuwa vikaragosi vya kuchezewa na kila mwanasiasa anayetaka ubunge jimboni kwetu.

Uzalendo ni pamoja na kuuliza inakuwaje mashirika yetu yanauzwa kwa bei ya kutupa? Ni pamoja na kuhoji kwa wanini viongozi wanakaa kimya wakati viwanda vyetu vinakufa nchini? Nani asiyejuwa kuwa vitu vingi vinaagizwa toka nje ili hali tunavyo hapa nchini? Kwa ninisamani ziagizwe nje ya nchi wakati tuna mininga, mikaratusi na aina zingine za miti inayoweza kutengeneza bidhaa hizo? Tukisema kuwa suala ni utandawazi, tutawahoji kuna ulazima gani wa kushikiria sera za mataifa ya magharibi huku tukijua kabisa kuwa zinapeperusha ndoto za maisha bora kwa kila mtanzania? Ni kweli hakuna la kufanya kulinda viwanda vyetu na wazalishaji wa ndani? Haya ni amswali ambayo watanzania wakiwa wazalendo watawauliza viongozi. Wanatuhimiza kuwa wazalendo, je haya watayastahimili? Je watatupa majibu yetu ya wazi na kweli? Je hawatatupachika majina na kutuita wenye wivu wa kike, wachochezi na kimbelembele? Maana huo ndio uzalendo!

Uzalendo ni pamoja na kuhoji juu ya uhalali wa viongozi kukingiana vifua hasa wanapokuwa na kashfa ikiwamo rushwa ambayo sasa hivi inaitwa uzembe kwa mujibu wa mwandishi Fulani hapa nchini. Tutawauliza kwa nini Fulani alifanya madudu haya halafu wewe unasema tumuache apumzike? Wasije juu na kutukunjia ndita, wasitukasirikie, wasitutishie maisha yetu na usalama wetu, maana huu ndio uzalendo! Hakuna maana ya kujiita wazalendo huku tukiiacha nchi ipelekwe na watu wachache kwa jinsi wanavyojisikia!

Uzalendo ni pamoja na kuhoji na kukemea ubadhirifu wa fedha za umma na baadhi ya viongozi wa ngazi tofauti tofauti. Na inapotokea hivyo wasituite majina wanayojisikia kutita, kama wana haja ya kutuita kwa majina yetu basi watuite yale majina halisi tuliyopewa na wazazi utotoni. Maana hii ndio gharama ya uzalendo!


Uzalendo una mengi, na mengi hayo hayapendwi na watawala, huu ndio ukweli! Wanapotuhimize uzalendo kwa wananchi, ikiwa si wanafiki waanze wao kuwa wazalendo, kwa kuacha kuhujumu taifa hili kwa wale wanaofanya hivyo, maana hata serikali inakiri kuwa kuna wahujumu, kwa mfano wale watendaji wanaotumia fedha za serikali (zetu) vibaya! Ikiwezekana pia wapunguze bei za katiba ya nchi yetu ili kila mtu amudu kununua, kasha maduka ya serikali yafunguliwe kila mahali ili hata watanzania wa vijijini wanunue wasome wawe na vigezo (grounds) za kuwakosoa na kuwakosoa au kuwapongeza na kuwakumbusha inapobidi!

Kuuliza hivi ikiwa watamudu gharama za uzalendo au la haina maana kuwa wakikataa gaharama hizo hatutakuwa wazalendo, hata wakikataa na kuacha kuhimiza uzalendo, bado tutaamshana ili tuwe wazalendo!

Mungu ibariki Tanzania, Mungu bariki watanzania!