Wednesday, July 4, 2007

WARAKA WANGU KWA WATANZANIA!

Nianze kwanza kwa kukusalimu popote ulipo ee Mtanzania, poleni kwa yote ambayo mnakutana nayo katika kila iitwayo siku kwenu. Baada ya salamu napenda kuwauliza swali, je ninyi ni wazalendo? Tafadhali lifanyie kazi swali hili.

Baada ya swali hili naomba nitoe ombi langu kwako wewe uliyebahatika kusoma waraka huu. Chonde chonde, jitahidi, fanya kila uwezalo uhakikishe waraka huu unasomwa na watanzania wengi kama si wote. Jitahidi kuwa mbunifu ili kufanikisha hilo.

Unaweza ukanunua nakala nyingi kadri uwezavyo na kuwagawia watanzania wengine, (hakikisha unayempa ni mtanzania) Pia unaweza ukasoma na kuanza kuzungumza na wenzako kuhusu waraka huu, nenda kawaelimisha, usijali kama wataukubali au watakataa ujumbe huu! Omba tu wakupe nafasi wakusikilize.

Pia unaweza ukatuma anuani ya tovuti ilipo hapo juu kwa wote walioko mikoani na nje ya nchi, waambie wasome kupitia mtandao wa ‘Internet’ anuani yenyewe ni hii www.amkenitwende.blogspot.com, tafadhali nisaidie kuufikisha ujumbe huu kwa watanzania wa rika, hadhi, jinsia na hali zote, nisaidie tafadhali!

Kwa nini nimeamua kuandika waraka huu? Nimekuwa nikisisitiza kila siku kwamba hii nchi ni ya kwetu. Ni sisi ndio tutakaojenga au kubomoa nchi hii. Nchi hii si mali ya CHADEMA, CUF, CCM, UDP, NCCR-Mageuzi au vinginevyo. Hakuna waziri au Mbunge mwenye hati miliki ya nchi hii. Hata Mwl. Nyerere alikuja, akaitumikia nchi hii, kwa kutambua kuwa hii nchi si mali yake, ulipofika wakati akawaachia watanzania wengine kuongoza nchi hii.

Ninachosisitiza hapa ni kwamba hii nchi ni watanzania walioko kule Magila kule Gonja, ni wale walioko Mlalo, Lushoto, walioko Kizorogoto kule Morogoro na kila paitwapo Tanzania. Kuna haja ya kuondoa dhana ndani ya fikra zetu kwamba Tanzania inamilikiwa na SERIKALI, kwa hivyo wananchi wa kawaida hawana la kufanya katika kujenga nchi hii.

Nakumbuka siku moja nikiwa eneo mojawapo hapa Dar es salaam, katika mitaa ya eneo hilo ilijaa uchafu na madimbwi ambayo ulikuwepo uwezekano mkubwa na wa kutosha kabisa kuondosha ile hali. Ilinibidi kuzungumza na baadhi ya wakazi kuhusu suala la uchafu ule. Mmoja wapo alijibu na kusema kwamba sisi sio jiji, kuhusu kupasuka kwa mabomba yanayotoa maji na kumwaga barabarani walisema wao si DAWASCO hata waamue kushughulikia tatizo hilo.

Kwa watanzania wengi kila kitu kinafanywa na serikali, pengine enzi za ni athari za ujamaa ndizo zinazotusumbua kwa sasa, lakini je hii nchi bado ni ya kijamaa kwa kweli? Hata kama Katiba inaeleza hivyo katika kifungu cha………

Kila mwanadamu anayezaliwa katika ardhi hii huzaliwa kwa makusudi, na ndio maana ni vizuri kujihoji kila mara, UNAIFANYIA NINI TANZANIA? Naamini kwamba ni watanzania wengi sana hawajawahi na hawana mpango wa kujiuliza swali hili, kama imani yangu ni potofu naomba nisamehewe. Yote haya ni kwa sababu tunadhani hatuhusiki kwa namna yoyote katika kuijenga nchi hii, na ndio maana kila kinachotokea na kutudhuru hutupa lawama kwa serikali, lakini tunashindwa kukumbuka kuwa pengine tunahusika kuifanya serikali ifanye yale inayoyafanya.

Sikatai kuilaumu serikali, serikali ni mzazi, anabeba lawama pale anaposhindwa kuwafanyia watoto wake stahili yao. Lakini hatuwezi kumlaumu mzazi eti kwa sababu mtoto wake mwenye umri wa miaka 24. mwenye akili timamu, mwanafunzi wa chuo kikuu mwaka wa kwanza haogi kwa sababu ya uvivu tu! Hatuwezi, tutaonekana wehu!

Kama wananchi tuna wajibu wetu kuhakikisha nchi hii inakwenda kuliko inakotakiwa kwenda. Naomba nitoe mfano kidogo hapa.

Hivi karibuni kumetokea ajali za kutosha zilizo poeteza watanzania wenzetu, sasa hawapo, wamelala mauti! Hatukuchelewa baadhi yetu kuilaumu serikali kwa sababu ya ajali hizo. Moja ya sababu zilizotolewa na baadhi ya wahanga wa ajali hizo ni mwendo kasi! Hili nalo tumeilaumu serikali.

Kuna wakati tuliilaumu serikali kwa sababu ya magari kujaza abiria kwenye mabasi yaenadyo mikoani! Ngoja nkiupe kisa hiki halafu niendelee!

Tarehe 19/05/2007 nilisafiri kimasomo kwenda mkoani Tanga, kama kawaida nilipanda gari pele stendi kuu. Safari ilianza vizuri sana, lakini tulipofika kituo cha Kibaha, lile basi lilipakia abirai zaidi kiasi cha kufanya wengine kusimama, kumbuka hiyo ni safari ya kwenda Tanga.

Kitendo kile kilishuhudiwa na askari mmoja wa usalama barabarani ambaye alipanda lile gari na kuwataka abiria wengine wapungue. Ndugu yangu abiria waliokuwamo kwenye gari walikuja juu kwa kitendo cha yule askari kutaka kupunguza abiria. Hoja yao ilikuwa ni kwamba wanacheleweshwa. Sio siri nilishindwa kuvumilia kile kitendo cha abiria wenzangu.

Nilisimama na kumtetea yule askari, si kwamba nilikosa siti ya kukaa, nilikuwa nayo! nikawa kama nimewasha moto ndani ya basi, kwani abiria wote walikuja juu na kuniita mnafiki, nilikuwa katika wakati mgumu sana. Katika lile gari kulikuwamo mwanafunzi mwenzangu yeye anachukua masomo ya sheria. Akageuka na kuwa mwiba kwangu, yeye alivuka mipaka na kutaka kunivamia ili kunipiga mbele ya askari wapatao watatu pale Kibaha, huyu ndiye mwanasheria wan chi hii baadae! Hoja yake ni kwamba mimi ni kimbelembele na kwamba nachelewesha safari za watu!

Amini usiamini askari wote pale walizidiwa nguvu na abiria, gari ikaachwa iende ikiwa na abiria waliosimama kama mizigo kwenye basi. Na abiria wale waliapa kwamba nikipanda lile gari nitakiona cha moto, nakwambia nilishushwa na kutafutiwa gari ingine. Hii ndio nchi yetu, na wale ndio watanzania wenyewe. Ajali ingetokea pale, lawama ni serikali.

Hiyo ni moja, pili nakumbuka nilikupa kisa kimoja nilipokuwa natokea Nairobi kurudi nchini, kwamba gari ilikwenda mwendo wa kasi mno, lilikuwa ni basi la kampuni ya SABCO, wakati tunalalamika mwendo huo, kuna abiria wakatupinga vikali na kumtaka dereva aongeze mwendo zaidi. Mungu bariki tulipofika maeneo ya michungwani mkoani Tanga, askari mmoja alisimamisha liele basin a kumuonya yule dereva, kasha akatoa namba yake ya simu ikiwa yule dereva ataendesha kwa mwendo mbaya, si hivyo tu alituachia jina lake kuwa anaitwa YOHANA, Ee Mungu tupe askari wengine wengi kama Afande YOHANA!

Ndugu zangu sijasahu nilipokuwa mkoani Singida mwaka 2004 ambako nilikwenda kwa shughuli za kuhubiri ujumbe wa neno la Mungu, niligombana na baadhi ya wasafiri wenzangu kwa sababu ya kuzidisha abirai kwenye basi la kampuni ya TASHRIF, ambayo baadae ilipata ajali muda mfupi baada ya kuondoka Stendi kuu ya Singida.

Hivi una habari kuwa kuna watanzania huwa wanachanga pesa ili kuwalipa askari wa usalama barabarani pindi madereva wanapofanya makosa? Tunailamu serikali kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kama yale ya kulinda usalama wa raia wake, je sisi tumetekeleza yapi ili kulinda usalama wetu? Pengine ni maneno magumu na machungu sana naongea hapa, mniwie radhi, nivumilieni, huu ndio ukweli!

Hii ninayoitoa hapa ni mifano kidogo tu! Watanzania tumekuwa pia na nidham ya uoga isiyo kifani, tuna chembe Fulani ya unafiki.

Siku moja tukiwa darasani chuoni, kulianza mjadala kuhusu tatizo la rushwa Tanzania, katika hali ya kustaajabisha kuna baadhi wakawa wanakiri na kusimamia kwamba rushwa haiwezi kuondoka, ungesikiliza kwa makini ungegundua kuwa si kwamba haiwezi kuisha kwa sababu ya ugumu wake, bali ni kwa sababu ya maslahi ya watu Fulani, kuna wajumbe wakafikia hatua ya kusema bila haya kwamba ihalalishwe! Hawa ni watanzania! Ninyi mnapigana na adui upande wa kusini, upande wa kasikazini kuna wapiganaji wenzetu wanamtia moyo adui na kumpa mbinu za kutushinda!

Makala hii itaendelea wiki ijayo!