Saturday, June 23, 2007

Waraka wangu kwa Rais Kikwete!


Rais Jakaya Kikwete akionekana mwenye kuumiza kichwa kutafakari jambo fulani, hapa ni kama vile anasema "ama kweli kazi ninayo'

Ninakusalimu kwa heshima zote unazostahili mheshimiwa Rais upendwaye na wengi. Uniwie radhi sana ikiwa ninakukera kwa kutumia muda mwingi kuiandikia serikali yako. Hii imesababisha watu kuniuliza kwa nini kila makala ninayotoa huwa ‘naishambulia’ serikali. Mimi siishambulii serikali, kwa mtazamo wangu mimi naisaidia serikali kwa nafasi yangu niliyonayo.

Hata hivyo ikiwa mtu ataniuliza kwa nini naishambulia serikali, na ikiwa ni kweli nafanya hivyo, basi nitamjibu kuwa sina sioni sababu ya kutosihambulia! Kirahisi tu, nitajibu hivyo!

Mheshimiwa rais, nimewahi kuandika kuwa nchi hii ina rais mmoja tu, na kuwa rais haimaanishi kuwa unajua na kuweza kila kitu, nikasema, ndio maana unahitaji mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na waandishi wa habari na wachambuzi kama sisi kukusaidia kutekeleza majukumu yako ya kila siku. Ka msingi ho usituchukie wala kutuwekea kinyongo eti kwa sababu tunakuandika kila mara!

Mara nyingi ninyi watu wa serikali mnapoandikwa kwa namna msivyopenda huwa mnalaumu vyombo vya habari na kushauri kuwa vitumie taaluma hiyo kuwaelimisha wananchi. Na mimi nitumie fursa hii kusema kwamba mnapoona kuwa waandishi wameandika ndivyo sivyo msiwatishie kuwafungia wala usalama wa maisha yao, ni vizuri mkawasahihisha kwamba walichoandika sio au ndio. Tuishi kwa amani!

Mheshimiwa rais wangu, ulipokuwa ukitimiza mwaka mmoja Ikulu nilikuandikia kuwa sidhani kama kuan mtu ambaye watanzania wa,ewahi kutokea kuwa na matumaini nae kama wewe. Sehemu ya makala hiyo ilikuwa hivi “
sina mengi ya kusema juu ya utawala wa Kikwete kwa siku 365, ninachoweza kusema ni kumtia moyo na kumpa ukweli kuwa akaze buti, hali bado ni rhumba kali. Safari bado ni ndefu! Nikiwa kama mzalendo wa nchi hii sina sababu ya kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa, nimeshuhudia watu wengi wanapoanza kuzungumzia utawala wa Kikwete mara hurejea kwenye hotupa zake na kwenye mikutano ya kampeni. Akiwa mgombea wa urais kupitia C.C.M Kikwete aliwakuna sana watanzania kwa ahadi zake kemkem. Ahadi hizo zilikua nzito na nzuri, akadiriki hata kusema wazi kuwa kama kuna ahadi ambazo atasahau basi ruksa kukumkumbusha.Aliwapa matumaini makubwa sana watanzania, mara nyingine ninaporudi nyuma kuangalia historia ya viongozi wa nchi hii najikuta namuonea huruma rais Kikwete. Namuonea huruma kutokana na ukweli kwamba je, asipotimiza ahadi hizo atawaeleza nini watanzania? Ni ahadi nzito na nyingi mno, huruma yangu inazidi nikiwaza ikiwa alitoa ahadi hizo ili apate kuingia Ikulu au kwamba kweli amedhamiria kuikwamua nchi hii.Unajua kwa nini nasema namuonea huruma? Watanzania ni miongoni mwa Waafrika wanaosota kimaisha kutokana na pengine sera mbovu za wanasiasa au ufisadi na ubinafsi wa viongozi wa nchi zao. Watanzania wamesubiri kwa hamu kubwa kiongozi kama Kikwete, ambaye anaweza akakiri tatizo hadharani bila kuficha wala kupamba kwa unafiki ili kuonekana kiongozi mzuri bila kujali kuwa anaua watu wake.

Watanzania hawajasahau dharau na ubabe wa viongozi wao kama ule wa Basil Mramba aliyekuwa waziri wa fedha katika serikali ya awamu ya tatu, chini ya Mzee Benjamin Mkapa, aliyeidhinisha ununuzi wa ndege ya rais kwa mabilioni ya shilingi huku nchi ikikabiliwa na janga la njaa.
Na mramba kwa jeuri kubwa akasema bora watanzania wale majani kuliko kuacha kununua ndege ya rais, eti watanzania wale majani? Kila ninapoikumbuka kauli hii, hushikwa na uchungu na machozi hunilenga. Hivi kweli Mramba alitudharau kiasi hiki watanzania? Sisi ambao nchi hii ni mali yetu na wala si wakimbizi au wavamizi. Anatusimanga katika nchi yetu wenyewe? Kwelii??Kidonda hiki cha wananchi hakijapona bado, kilitoneshwa zaidi pale waliposikia kuwa Mramba yuko tena ndani ya baraza la mawaziri, sio kila mtu alimwangalia vizuri Mramba ‘a.k.a’ ndege ya rais, tukadhani atajirekebisha.Baada ya muda tukasikia kuwa amemdanganya rais kuhusu ujenzi wa barabara ya shekilango na Sam Nujoma jijini Dar es salaam , kama hiyo haitoshi nasikia kule Mtwara au Lindi aliwahi kumkera hata waziri Mkuu, Mh. Lowassa”

Rais Kikwete nimeamua nikukumbushe tu kwamba nimeahi kuzungmza na wewe kupitia safu hii, kama wewe hujasoama basi kwa namna moja ama nyingine wasaidizi wako watakuwa walisoma.

Katika kukuambia nilichokusudia leo sina haja ya kuzunguka mbuyu au kufunika kombe mwanaharamu apite, ukweli ni kwamba watanzania walio wengi ukiondoa mawziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wamekata tamaa, wamechoka!

Na sioni sababu ya kwa nini nisikuambie tu kwamba wanasema mitaani kuwa utawala wako umeanza kuwachosha watanzania. Lengo langu hapa sio kukuumiza wala kukudhihaki, nia yangu ni kukufanya uwe na taarifa hiyo ili uweze kuchukua hatua zinazostahili kunusuru hali, ndio maana nikasema nakusaidia, maana naamini kwamba ili kumsaidia rais, hainihitaji kuwa waziri au sehemu ya familia ya rais.

Miongoni mwa vitu ambavyo watanzania wanakatishwa tamaa ni kauli zako zinazoonekana wazi kumtetea mtangulizi wake bwana Mkapa katika tuhuma zinazomkabili, unavyoonekana mbele ya macho ya baadhi ya watanzania ni kwamba umeona kitu alichofanya Mkapa kuanzisha kampuni akiwa bado rais ni kitu kizuri na chenye kufaa, hii inatufanya tubaki njia pamnda katika ahadi yako ya kutofanya biashara Ikulu kama alivyofanya Mkapa.

Si hivyo, kuna maneno yanasemwa mitaani kwamba unamkinga Mkapa ili kwamba kama itatokea utafanya maovu ukiwa Ikulu basi atakayekufuata naye akukingie kifua kwa kisingizio cha kukucha upumzike. Hivi kweli ulithubutu kuwaziba midomo wasimhoji mwajiriwa wao mstaafu? Kuna ubaya gani kumhoji alichofanya ikiwa ni halali au la? Kama watanzania hawatamuhoji Mkapa, unataka nani amuhoji?

Binafsi mimi kijana wako nilishangazwa na misimamo yako mheshimiwa Rais, eti unataka Mkapa apumzike, sawa hatuna tatizo na Mkapa kupumzika, lakini nani atamjibia tuhuma hizo mzee Mkapa? Je ni Sumaye? Sumaye mwenyewe kasema kuna hoja alishindwa kuzijibu kwa makusudi kabisa kwa sababu hazina maana. Kama kuna uwezekano, ningekusihi kwamba uwaache wenye nchi wamhoji Mkapa, apumzike kwa kazi ipi? Mbona hajamaliza kulitumikia Taifa? Ikiwa ni pamoja na kutueleza alipataje mali anazomiliki sasa hivi? Mbona alipoingia alitaja mali? Kimya chake kwa kushindwa kutaja mali alizotuma ndicho kinachotutia mashaka kwamba Mkapa ana walakini!

Joseph Mbatia, mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi aliwahi kusema kwamba, ni hatari sana kuufikisha umma mahali pa kukata tamaa, hatuna lugha ya kutosha kukiri kuwa sasa watanzania wanaanza kukata tamaa.

Nikutie moyo rais wangu, kaza buti, anza wewe kujifunga mkanda, hali ni ngumu, macho ya mamilioni ya watanzania yako kwako, utawajibu nini watanzania utakapoondoka bila kutimiza zile ajira milioni moja, bila kudhibiti mfumuko wa bei, uhakika wa masikini kuwasomesha watoto wao vyuo vikuu, nasema utawajibu nini Watanzania?
Hivi ni kweli kwa kusoma magazeti na vyombo vingine vya habari hujagundua tu kuwa watanzania wamekata tamaa? Hujashtuka tu, najua sio rahisi wewe kufika kila kijiji cha Tanzania, kila wilaya nakadhalika, waliofika wanakwambia hali ni mbaya, fanya kila uwezalo ili matumaini ya Watanzania kwako yardi. Hii ni pamoja na kuwawajibisha wasaidizi wako ambao hawana msaada uwao wote katika kuwatumikia wananchi.

Sio mbaya kama ungeuliza nani hafai, mimi harakaharaka bila hata kuhitaji kufikiri ningekushauri umpumzishe Peter Msolla na wala sio Mkapa na wengine wanaofanana naye akiwamo Basil Mramba.

Nimejitoa kwa lolote, najua hawatafurahia ukweli huu, hata kama watakasirika na kufikia hatua ya kutaka hata kuniua, basi wakae wakijua kuwa nikifa Danieli kuna kina Daniel wengine wengi watazaliwa tena, hata hivyo hata kama wao hawataniua bado kuna siku moja nitakufa!

Mheshimiwa Rais, nakupenda ndio maana nakwambia watu wamekata tamaa! Ninakuombea, kwa hakika tuko nyuma yakom lakini kaa ukielewa kuwa kuna wasaidizi wako wanakuponza!

Mung ibariki Tanzania, bariki viongozi wake, wawe watu wa kukubali ukweli, wafanye kuelewa kua kukosolea si dhambi ya kuwapeleka jehanam! Amen!