Saturday, April 28, 2007

MAPAMBANO YA RUSHWA NA UNAFIKI WA WATANZANIA!

Nianzeje kuandika makala hii? Ninahitaji ujasiri wa hali ya juu, vinginevyo nitashindwa, na kuna msemo unasema kwamba “ukitaka kumuua nyani usimwangalie usoni” Msemo huu ulitokana na dhana kwamba nyani anapolemewa huwa na uso uliojaa huruma,n i rahisi sana kwa adui wa nyani kumuonea huruma na kuacha kumdhuru au kumuadhibu kama alikusudia.

Kuandika makala sio kitu rahisi sana kama wengi wanavyodhani, inahitaji tafakuri ya hali ya juu sana, inahitaji kujipima wewe kwanza katika kile unachotaka kuwaandikia wengine. Wataalamu wanaita ‘pre-writing’ Unapotaka kuandika jambo inabidi ulipime katika ufahamu wako kwanza, kwa mfano unapoandika juu ya watu wanaoambukiza watu wengine virusi kwa makusudi, ni busara ukajipima kwanza wewe ikiwa hufanyi hivyo. Vinginevyo huo unaitwa unafiki, na adhabu ya unafiki ni kubwa kuliko wengi wanavyodhani. Ni bora uwe mwizi kuliko mnafiki.

Leo nataka kuandika kuhusu RUSHWA, wengine wamemuita mdudu, wengine adui, wanasiasa Fulani wakambatiza jina zuri na tamu kama nini, wakamuita TAKRIMA, nakuruhusu mpe jina lolote unalojisikia kumpa, lakini anabaki kuwa RUSHWA. Kwa wanasiasa wengi ni moja kati ya beti za nyimbo wanazoimba majukwaani wakiimba sauti ya kwanza, vyombo vya habari vimekuwa vikinogesha beti hizo kwa kuimba sauti zote zinazofuata, nikiwa na maana sauti ya pili, ya tatu na ya nne. Waitikiaji wamekuwa ni wananchi wa kawaida, kuunogesha wimbo huo, wao wameimba kwa hisia kali kuliko zile za Bob Marley wa Jamaika, Lucky Dube wa Afrika ya Kusini na Epharaimu Mwansasu wa Tanzania, wameimba huku wakitoa machozi kuonyesha hisia zao katika ujumbe walioukusudia kwa wasikilizaji wao. Ili mradi kuna kitu kinaitwa rushwa kinachotajwa na kusikika masikioni mwa watu!

Wanachi wengi wanalalamika kuwa rushwa imekithiri, miswada inatungwa, naambiwa kuna sheria mpya inaandaliwa ili kuwalinda watoa taarifa za rushwa, hekoo, safiii sanaaa! Pamoja na jitihada hizo zoote, bado kuna walakini katika vita hii, na mimi kama mwananchi naomba nitoe mawazo yangu.

Nataka kwanza tujihoji kidogo, kwa nini rushwa haikomi? Nani anatoa rushwa na nani anapokea? Nauliza hivi kwa sababu tumekuwa mahodari kweli wa kuwanyooshea vidole wanasiasa kuwa ni wala rushwa, watumishi wa idara za serikali kuwa ni wala rushwa, kwa lugha ingine ni kwamba tumekuwa tukiwatuhumu kuwa wanapokea rushwa. Kwamba watumishi wa idara mbalimbali za serikali, hasa zile nyeti wamekuwa wakiuza huduma ambazo wananchi walistahili kupewa bure! Tumekuwa tukiandika hata magazetini kuwa wanajihusisha na rushwa, lakini kwa nini tunasahau kuwa hawa watu wanapokea? Wanapokea kutoka wapi kama sio kwa watoaji? Nani anatoa kama sio anayehudumiwa ambaye ni mwananchi?

Nasema hivi, tumesahau kuwa hawa wapokea rushwa hawawezi kupokea wasipopewa, mtu analalamika kuwa hakimu alimuomba rushwa, kisha na yeye kwa hiari yake anatoa rushwa, ukiuliza anakwambia kuwa aliombwa! Siamini kuwa kuna mla rushwa anayemlazimisha mtu kutoa rushwa, hiyo hakunaa! Kwa hiyo hapa unaanza kupata picha kuwa wapo wahalifu wawili hapa, tufanye HAKIMU na MWANANCHI. Hakimu anadai apewe rushwa na mwananchi ili wafute kesi yake, kesi ambayo mwananchi na uhakika kabisa kwamba hana hatia, mwananchi naye anaingiza mkono mfukoni na kutoa hiyo rushwa, unaona hapa? Wote wameshiriki kutoa rushwa ila kwa staili tofauti, mmoja ni ametoa (kwa mtazamo wangu huyu ndiye mbaya zaidi) na mwingine amepokea ( ulikuwepo uwezekano wa huyu hakimu kukosa pesa hizo kwa vile hazikuwa kwenye himaya yake na wala hazikuwa mali zake)

Kitu ninachojaribu kufanya hapa ni kukuonyesha UNAFIKI tulionao baadhi ya wananchi ambao tumekuwa tukilalama kuwa rushwa imekithiri wakati sisi ndio watoaji. Ngoja nikupe mfano ulio hai, wiki iliyopita nilisafairi kikazi kwenda NAIROBI nchini Kenya, wakati narudi, basi (jina nalihifadhi) nililokuwa nikisafiria lilisimamishwa pale SEGERA mkoani Tanga.

Baada ya dakika chache mara utingo(jina lake ninalo) wa lile basi aliingia ndani ya basin a kuanza kuwataka abiria kuchanga pesa ili wampatie (sijui nani?) ili gari iachiwe iendelee na safari, kuna abiria walichanga pesa, yule konda akazikusanya na kushuka nazo kuelekea kwenye sheli na hoteli iliyo mkono wa kushoto kama unakuja Chalinze, hapo alipelekewa mtu Fulani zile pesa, baadae niliambiwa kuwa alikuwa ni askari wa usalama barabarani.

Hapo ni rahisi kujua, huhitaji Kuwa na elimu ya chuo kikuu kufahamu, unaelewa tu kuwa ilikuwa ni rushwa, (a)nani alidai rushwa, (b)kwa nini alidai, (c)nani alitoa na (d)kwa nini alitoa ndio maswali ya kujiuliza hapa? Kuna vitu nataka ujifunze hapo, kuwa makini, usije nihukumu kwa madai kuwa nimewadhalilisha wananchi! Hapa hatupokudhalilishana, tupo kuelimishana!

Rushwa iliombwa na askari wa usalama barabarani hilo ndilo jibu la swali la kwanza, swali la pili jibu lake ni rahisi sana, kumbuka nimekwambia kuwa hakuna mla rushwa anayemlazimisha mtu kutoa/kuhonga, kwa vyovyote aliona uvunjwaji Fulani wa sheria uliofanywa na wananchi, na watu hawa ni wajanja kweli, wanawajua watanzania ni waoga kwedna kwenye vyombo vya dola/sheria, sasa ili wasiende huko wanawadai rushwa, na hapo kuna kuwa hakuna kipingamizi, wanatoa kiulainiii! Hata kama kweli wananchi wanakuwa hawana kosa, ni ukweli kwamba wananchi wengi hawazijui haki zao katika nchi yao, Niumekutana na mambo hayo sehemu nyingi sana katika nchi hii. Kwa hiyo wanapotishwa kidogo hukubali kutoa rushwa ili wasikamatwe hata kama hawana kosa la kuwafanya wakamatwe. Jambolingine ni kwamba watanzania wengi tunapenda vitu vya dezo, na dezo zimetugharimu hasa wafanya biasha wanaovuka mipaka kwenda nchi mbalimbali, biashara nyingi ziazopita mipakani ni hazipiti kihalali, utashangaa utakapofanikiwa kukutana nazo siku moja, wasaidizi wakubwa ni madereva wa mabasi makubwa, nina wasiwasi pia na bandarini.

Bidhaa zilizokatazwa kama vile mirungi, madereva husaidia kwa kiasi kikubwa kuzipitisha mpakani kwa sataili wanazozijua wao, zingine huwekwa kwenye mifuko ya suruali, zingine kwenye magazeti na kuwekwa sehemu ya kioo kwa dereva, zingine hufungwa kwenye nguo, zinapokamatwa ndipo mkamataji anataka ahongwe ili kumwacha huru mvushaji, akishahonga anarudi kulalamika kuwa rushwa nchi hii imezidi, mnafiki huyu!! Mnafiki huyu anatoa hongo kwa sababu anajua kuwa amevunja sheria, watoa rushwa wengi na wavunjaji wa sheria, hutoa rushwa ili wanunue haki ya kutokamatwa! Hapo nimejibu swali la C na D

Ni muhimu kufahamu kuwa kuna namna nyingi za kutoa rushwa, kuna wale wanaotaka vya dezo (vya bei rahisi) kwa mfano wafanya biashara wanaokwepa gharama za ushuru.

Wanaovunja sheria na taratibu za nchi; hawa wako wengi sana, waangalie madereva, sheria inawataka kufunga mkanda, tena ni kwa ajili ya usalama wao wenyewe, lakini wanataka kufunga mkanda pindi wanapomuona trafiki barabarani, tariki akimkamata kwa sababu ya kukosa uazlendo na kuhujumu Taifa anamdai dereva hongo, dereva anatoa kasha anaanza kulalamika akisaidiwa na abiria kwenye basi, hakuna anayedadisi kwa nini trafiki alidai hongo! Kazi kupayuka na kulalama kuwa askari ni wala rushwa, kitu gain kilimpelekea kudai rushwa kama asingeona kosa la dereva? Kama kweli hana hatia kwa nini atoe rushwa?
Madereva na makondakta wameamuriwa kuvaa sare, bila haya, wanavaa sare wanapomuona askari wa barabarani, mara nyingine husimamisha gari na kupoteza muda wa abiria ili wavue au kuvaa sare, wakikamatwa (wao huita kupigwa bao) askari huwataka watoe hongo, na wanazichota kweli kweli!! Wakitoka hapa wanalalamika kuwa rushwa haitaisha nchi hii, wanaziba masikio na macho yao wasione kuwa wao wanashiriki kuipalilia rushwa katika Taifa hili. ADUI WA MTU NI MTU MWENYEWE, adui wa TANZANIA ni WATANZANIA WENYEWE! Watanzania wengi ni wakiwamo wanasiasa, viongozi wa dini, wafanya bishara ni wanafiki katika vita ya rushwa, kama Shigongo alivyosema, na mimi siwezi kuwa adui yenu kwa kusema ukweli!!


www.amkenitwende.blogspot.com
www.gingo.sulekha.com
Simu: 0713 550 778
E-mail: ilovejesustz@yahoo.com