Monday, June 18, 2007

TUKIAMUA KUWA WAZALENDO MTASTAHIMILI?

Ni rahisi sana kwa watawala wetu kama hawa wakisisitiza uzalendo kwa wananchi, kuna maswali kidogo nataka kuhoji hapa!

HIVI TUKIAMUA KUWA WAZALENDO, WANASIASA NA WATAWALA WETU WATASTAHIMILI?

.Je wanajua gharama ya uzalendo? Au wanasema tu?

Hala..hala wanasiasa mnapokuwa majukwaani. Jichungeni na kauli zenu. Muwe mnasema mnayomaanisha na kumaanisha haswa yale mnayoyasema!

Ndugu msomaji nimeamua nimejikuta nakuwa mkali tu leo, na si ajabu nikaitwa mbwatukaji, eti nabwatuka! Nambwatukia nani wakati mimi natoa elimu hapa? Nimeamua kuwa mkali kwa sababu sio siri kuna kauli na matamshi ya wanasiasa yanakera sana. Yanakera hasa unapozilinganisha kauli hizo na utendaji wake (wao?)

Hivi umewahi kuhudhuria mikutano, warsha, semina au nini zile…..? ‘Workshop’ za hasa wasemaji wakuu wanapokuwa wanasiasa? Hebu fikiria wito kama huu unaotolewa na huyu mheshimiwa nanihii…anasema “kwa hiyo nawaomba sana ndugu wananchi, muwe na moyo wa uzalendo kwa Taifa lenu” Mwingine najionyesha kuwa makini zaidi kwa kusema “unajua wakati umefika wa kuwa wazalendo” Msikilize na huyu anasema “eeeh!..uzalendo ni kitu muhimu sana kwa raia yeyote na wa taifa lolote kwa nchi yake”

Ni mahodari kweli wa kutoa matamko, kasheshe ni pale unapowadai watekeleze kauli zao kivitendo. Waambie waanzishe mitaala ya kufundisha uzalendo mashuleni, angau shule za chekechea tu, utapewa kila jina watakalojisikia kukupa au lile lililo rahisi kutamkwa na vinywa vyao.

Wengi wanato wito kwa wananchi kuwa wazalendo wakiwa hawajui gharama ya uzalendo pale wananchi wanapoamua kuwa wazalendo. Wanatunga mamba kwa hiari yao, lakini huwa wanakikimbia kile kinachozaliwa. Siwezi kuzungumza hapa leo ikiwa watanzania ni wazalendo au sivyo, isipokuwa, ukitaka kujua ukeli wa jambo hili angalia viongozi wa Tanzania, ung’amue ikiwa wao ni wazalendo au la!

Kwa ninavoelewa mimi uzalendo kwa lugha rahisi inayoweza kueleweka na kila mmoja ni hali ya kuwa na mapenzi ya dhati kwa nchi yake, si vibaya nikaongeza kwa kusema kuwa mtu mzaleno huwa tayari kujitoa mhanga kwa ajili ya Taifa lake, hasa pale linapohujumiwa bila kujali anayelihujumu ni nani na anatoka wapi!

Wanasiasa na watawala wanataka tuwe wazalendo, je watakuwa tayari kulipia gharama hii? Gharama ya watu hawa kujitoa mhanga kuijenga nchi yao? Nauliza hivi kwa sababu kuna mazingira yanaonesha kwamba watawala wengi hawapendi sana wananchi wawe na ufahamu wa kuelewa mwendo wa jinsi nchi yao inavyokwenda. Mwenendo wa watawala wao walivyo, ni haki yao maana waliwaweka madarakani, na mishahara yao ni kodi za wananchi!

Ngoja nitoe mawazo yangu hapa kuhusu wazalendo tunachoweza kukifanya tukishakuwa wazalendo. Mnatuambia tuwe wazalendo haya yafuatayo mtayaweza au ndio kule tunakodhani sisi watawaliwa ni janja ya maneno? Hata hivyo ikumbukwe kuwa kama wananchi hudhaniwa kuwa vikaragosi, wasiolewa mambo, mambumbu hawatabaki kuwa hivyo walivyo daima, kuna siku wataamka.

Uzalendo ambao wanasiasa wanatuhimiza sisi wenye nchi hii kuwa nao ni pamoja na kudai ahadi walizotuahidi wakati wa uchaguzi. Je watastahimili? Siku ambapo watakuwa wanapita na misafara ya utitiri wa magari yao kwenye majimbo yetu, watakubali tuwasimamishe, tuwaulize ahadi yao ya kutuletea maji jimboni iliyeyukia wapi na vipi? Watakubali tuwahimize kuwa muda unakwenda na hakuna lolote linalofanyika? Kusimamisha msafara jimboni tukiamua kuwa wazalendo haitakuwa na maana ya kuwakosea wakuu wetu adabu, itakuwa ni kujitoa mhanga wa kuwaonyesha kuwa tumeamua kuwa wazalendo na sio kuwa vikaragosi vya kuchezewa na kila mwanasiasa anayetaka ubunge jimboni kwetu.

Uzalendo ni pamoja na kuuliza inakuwaje mashirika yetu yanauzwa kwa bei ya kutupa? Ni pamoja na kuhoji kwa wanini viongozi wanakaa kimya wakati viwanda vyetu vinakufa nchini? Nani asiyejuwa kuwa vitu vingi vinaagizwa toka nje ili hali tunavyo hapa nchini? Kwa ninisamani ziagizwe nje ya nchi wakati tuna mininga, mikaratusi na aina zingine za miti inayoweza kutengeneza bidhaa hizo? Tukisema kuwa suala ni utandawazi, tutawahoji kuna ulazima gani wa kushikiria sera za mataifa ya magharibi huku tukijua kabisa kuwa zinapeperusha ndoto za maisha bora kwa kila mtanzania? Ni kweli hakuna la kufanya kulinda viwanda vyetu na wazalishaji wa ndani? Haya ni amswali ambayo watanzania wakiwa wazalendo watawauliza viongozi. Wanatuhimiza kuwa wazalendo, je haya watayastahimili? Je watatupa majibu yetu ya wazi na kweli? Je hawatatupachika majina na kutuita wenye wivu wa kike, wachochezi na kimbelembele? Maana huo ndio uzalendo!

Uzalendo ni pamoja na kuhoji juu ya uhalali wa viongozi kukingiana vifua hasa wanapokuwa na kashfa ikiwamo rushwa ambayo sasa hivi inaitwa uzembe kwa mujibu wa mwandishi Fulani hapa nchini. Tutawauliza kwa nini Fulani alifanya madudu haya halafu wewe unasema tumuache apumzike? Wasije juu na kutukunjia ndita, wasitukasirikie, wasitutishie maisha yetu na usalama wetu, maana huu ndio uzalendo! Hakuna maana ya kujiita wazalendo huku tukiiacha nchi ipelekwe na watu wachache kwa jinsi wanavyojisikia!

Uzalendo ni pamoja na kuhoji na kukemea ubadhirifu wa fedha za umma na baadhi ya viongozi wa ngazi tofauti tofauti. Na inapotokea hivyo wasituite majina wanayojisikia kutita, kama wana haja ya kutuita kwa majina yetu basi watuite yale majina halisi tuliyopewa na wazazi utotoni. Maana hii ndio gharama ya uzalendo!


Uzalendo una mengi, na mengi hayo hayapendwi na watawala, huu ndio ukweli! Wanapotuhimize uzalendo kwa wananchi, ikiwa si wanafiki waanze wao kuwa wazalendo, kwa kuacha kuhujumu taifa hili kwa wale wanaofanya hivyo, maana hata serikali inakiri kuwa kuna wahujumu, kwa mfano wale watendaji wanaotumia fedha za serikali (zetu) vibaya! Ikiwezekana pia wapunguze bei za katiba ya nchi yetu ili kila mtu amudu kununua, kasha maduka ya serikali yafunguliwe kila mahali ili hata watanzania wa vijijini wanunue wasome wawe na vigezo (grounds) za kuwakosoa na kuwakosoa au kuwapongeza na kuwakumbusha inapobidi!

Kuuliza hivi ikiwa watamudu gharama za uzalendo au la haina maana kuwa wakikataa gaharama hizo hatutakuwa wazalendo, hata wakikataa na kuacha kuhimiza uzalendo, bado tutaamshana ili tuwe wazalendo!

Mungu ibariki Tanzania, Mungu bariki watanzania!



Friday, June 15, 2007

Hali ni mbaya, nimeona leo tushirikishane juu ya uzalendo! Uzalendo! Unajua uzalendo wewe? Hali ya kujitoa kuipenda nchi yako, unaithamini, unailinda kimaadili, kisiasa, kiitikadi na kadhalika. Nasema unaipenda nchi yako, huu unaitwa uzalendo, naam kuipenda nchi yako.

Utashangaa nikikwambia kwamba binadamu wengi (sio wote) waishio katika nchi ya Tanzania, hawaipendi Tanzania. Nimesema binadamu, nimeogopa kutumia neno ‘watanzania’ Unaweza usinielewe. Labda niseme hivi, Watanzania (kama ulivyozoea kuita) wengi hawana mapenzi na nchi yao. Wako tayari kufanya lolote baya na kuidhuru nchi yao.

Hii ni kuanzia viongozi wa nchi mpaka raia wa kawaida. Hawaitaki Tanzania wala vilivyomo humu. Namaanisha kwamba, hawapendi lugha yao ya Kiswahili, wananchi wenzao, viongozi wao, mavazi yao( vazi la Tanzania ni lipi?) Unaweza kunizodoa kwa hoja hiyo. Nitakuuliza swali, ule mpango wa kubuni vazi la taifa umeishia wapi? Liko wapi hilo vazi? Juhudi zipi zimefanywa na wizara yenye dhamana ya utamaduni wa nchi hii kuhamasisha matumizi ya vazi hilo? Umewahi kumuona waziri wa utamaduni wa nchi hii amevaa vazi la kitanzania? Uliona waziri wa utamaduni siku alipokuwa akiapishwa alivaa vazi la wapi? Hiyo kazi nakupa katafute jibu, kama ukijisikia nitumie jibu hilo.

Tuhamie kwa wabunge wetu, wanapokuwa na vikao vyao kule Dodoma, si umewahi kusikia, huwa wanageuka na kuwa waingereza? Hawataki kutumia lugha yao ya Taifa, wanasahau kabisa kwamba wao ni wawakilishi wa mamilioni ya Watanzania ambao hawajui lugha hiyo ya kiingereza. Tatizo lao ni nini? Kwa nini wasitumie lugha yao asili ambayo pamoja na kuzungumza pia ni kuikuza ili iwe ya kimataifa kama ilivyo kwa lugha ya kiingereza? Huu ni uzalendo?

Waangalie nao wasomi wetu, wanaandaa mada zao wakiwalenga watanzania, bado wanatumia kizungu kuwasilisha mada hizo, sijui kama watakupa sababu za kueleweka zinazowafanya wakwepe kutumia Kiswahili utakapowataka wafanye hivyo. Je huu ni uzalendo?

Tusafiri pamoja na kufika kwenye asasi mbalimbali, kule kwa wanaotumia kiingereza wanaita NGO’s, asasi hizi ni zile zenye waasisi wa kitanzania. Ziwe za kuhusu elimu ya UKIMWI, elimu, afya na kadhalika. Wanapoweka matangazo yao, angalia kwa makini, mengi yako kwa lugha ya kiingereza kana kwamba wanawasiliana na watu wa mataifa mengine ambayo si Tanzania, kazi tunayo!

Tusiache kuwatembelea vijana vijiweni, hawa ndio kabisa, siku hizi ili waonekane bora watakwambia wanazungumza kizungu, wanacheka kizungu, wanavaa kizungu (vitovu vikiwa nje kwa upande wa mabinti) n.k hawataki kuonekana kuwa ni watanzania.

Unajua nini namaanisha katika makala hii? Chochote unachofanya ili kuihujumu nchi yako kwa namna yoyote ile, tunasema huo si uzalendo. Nimetoa mfano mdogo tu wa kuidharau lugha yetu.

Je nimetoka nje ya mada? Hivi nazungumzia nini hapa? nazungunzia nini vile? Aah!..nimekumbuka, nilikuwa nahoji sababu ya wasomi kusota mitaani wakiwa taabani kiuchumi. Nikasema tatizo ni uzalendo.

Maana yangu ni hii, viongozi wa nchi hii wamekuwa si wazalendo, utendaji wao unathibitisha hilo. Kama kiongozi ni mbovu na anashutimiwa wazi wazi kwa rushwa na hataki kujiuzulu, tumwiteje kama si mtu wa kuihujumu nchi yetu?

Mtu anayeingia mikataba ya siri ambayo baadaye inasababisha mahangaiko kwa wananchi wake tumpe jina gani? Au mtu anayeiuza nchi kwa kisingizio cha ubinafsishaji (usio na mpangilio) tumbatize jina lipi? Nisaidieni tafdhali!

Mtu anayeuza mashirika ya umma na kuwapa wazungu kwa kigezo cha kuboresha uzalishaji na kukuza uchumi wa nchi hii apewe jina gani? Ni wahujumu hawa!

Naomba niongeze swali hapa, nitafutieni jina la kumpa mtu anayewanyima mikopo wanafunzi kwa kisingizio cha alama za kufaulu, huku akijua wazi kuwa anarudisha nyuma maendeleo ya elimu yetu nchini. Mimi namwita mhujumu wa elimu ya nchi hii, hivyo si mzalendo!

Viongozi wengi wa nchi, huwa wanajisahau wanapoyakwaa madaraka, ndani Yao huzaliwa kitu kinaitwa ubinafsi, hawataki tena kujishughulisha kitaifa, pengine hujishughulisha zaidi na familia zao na jamaa zao. Kama ndivyo napata swali, kwa nini waliyakubali madaraka, kwani hawakujua kuwa wanakwenda kuwatumikia wananchi na si familia zao?

Wajibu wa kuandaa mazingira ya ajira na kujiajiri ni wa serikali. Serikali ndio inayoweka kanuni na taratibu za ajira na kujiajiri. Wananchi hata kama wangekuwa na uwezo wa kujiajiri, bado watalazimika kufuata taratibu na kanuni zilizowekwa na serikali yao. Sera na mipango.

Uzalendo…uzalendo uzalendo, naimba wimbo huu uzalendo, nasisitiza uzalendo. Hata hivyo ni muhimu kufahamu kuwa kuamua kua mzalendo kwataka moyo, kuna gharama za kuwa mzalendo na ndio maana huwa naamini kuwa uzalendo sio tabia, na kama ni tabia basi ni ile tabia sugu, imebadilika inakuwa ‘spirit'

Umeelewa hoja yangu ya leo, basi amka twende!
0713 550 778


Monday, June 11, 2007

SINZA INATIA AIBU KWA UCHAFU!

Huu ni moja tu kati ya mitaa michafu ya kule kunakoitwa Sinza kwa wajanja! Huu ni mtaa maarufu wa Sinza Msikitini au, wakazi wanapita kwenda maofisini, sidhani hata kama kuna mtu mmoja anawaza cha kufanya!


Huwezi amini kuwa hii ni Sinza, hawa ni watoto niliwafunmania asubuhi na mapema wakicheza kwenye uchafu uliolundikwa njiani na watu wenye akili timamu, si hivyo tu, lakini wanachezea pia maji machafu. Watu wanaodhaniwa kuwa ni wazazi wao walikuwepo nikipiga picha!

WAKAZI WA SINZA WANASEMA WAO SI DAWASCO WALA SERIKALI, NI KAMA VILE WANA 'ENJOY' SANA KUISHI NA UCHAFU


Huu ni mtaa anaoishi Mwenyekiti wa Serikali za mitaa Sinza, nyumba iliyojaa nyasi hapo kushoto ni nyumba ya kidosi mmoja, na kulia ni nyumba ya kidosi mwingine, wanatoka na magari yao na kuacha midimbwi hiyo kila siku kana kwamba hawaoni, Ili mradi wana masofa ya kutoka Ulaya ndani na vitu vingine vya thamani yakiwemo magari haoni haja ya kuweka mtaa safi!
Niliwahi kumfuata Mwenyekiti na kumuuliza kulikoni, akasema yeye hana la kufanya, eti hana la kufanya kiongozi, mbona kama ni viongozi Tanzania tumepata!


Friday, June 8, 2007

USIOGOPE!


Ni mchana huu wa leo, tunajiandaa na mitihani ya kumaliza mwaka na wakati huo huo kampeni za kuwania urais hapa chuoni kwetu zimeanza, kwa hiyo pia tumetoka kuwasikiliza wagombea, hawana tofauti sana na wanasiasa wa vyama vya siasa. Maneno meeengi. Tunasubiri utekelezaji, ndipo tutakapoweza kuhukumu ikiwa walitaka umaarufu au kututumikia wanafunzi!
Ni hatari sana kama wanataka kujifunzia siasa hapa chuoni, ni sawa ikiwa tui watakuwa hawajifunzi kudanganya kama walivyowaongo wanasiasa wengi Tanzania (na duniani?? au?)
Nyota njema huonekana asubuhi, msemo huu haujachuja maana yake bado, bado unafanya kazi. Chuoni ni mahali pa kujifunza uadili na ubadhirifu ukitaka. Kinachonisikitisha ni kwamba hata wasomi nao huwa bado hawana macho ya kung'amua waongo wanaodanganya mchana kweupee! Hivi mtu na akili zako unachagua kiongozi chuoni eti kwa sababu kakuahidi atahakikisha tunapata mikopo bila kutueleza njia atakazozitumia.
Atatupatiaje na kwa njia zipi? Mashaka zaidi tunayapata kwa sababu mtoa ahadi hizo hachukui mkpo, analipiwa na wazazi aua anajilipia mwenyewe. Huo ni mtihani mdogo sana wa wasomi kuwapima wanaotaka uongozi. Ndio maana wale wale wanaisasa wakija na sera zao kuwa watatujaza mapesa tunashangilia kana kwamba ana ghala za pesa sehemu fulani. oooh! samahani, naomba niishie hapa kwa leo! Nawahi kujiandaa na mitihani!


Nazungumzia hapa Chuo Kikuu cha Tumaini-Dar es salaam. Huyu anaitwa Anisa Juma, baada ya kujisomea, sasa ni mapumziko ikiwa ni pamoja na kupiga picha.

Wednesday, June 6, 2007

MAMBO YA TUMAINI UNIVERSITY

Hapa nipo na rafiki zangu wa chuo kikuu cha Tumaini tawi la Dar es salaam, kutoka kushoto ni Lusohoka Zakeyo, Anisa Juma, mimi mwenyewe, Balikudembe Joseph, Zamaradi, Neema Mrema na aliyeinama ni caroline Candus, hapa tulikuwa chuo cha Tumaini Iringa.