Hawa ni wanasiasa, Freeman Mbowe wa CHADEMA na Jakaya Kikwete wa CCM

Hawa ni wanasiasa, kutoka kushoto ni mzee Mkapa, anayefuata ni Mzee mwinyi na kulia ni Kikwete, wale wengine kule nyuma, sio siri siwajui! nasema sio lazima wote tuwe wanasiasa ndipo tuijenge nchi yetu, kila mmoja anayo nafasi yake kuijenga nchi hii. Zaidi ya hapo ni kukwepa majukumu!
Wiki iliyopita sikuonekana kwenye ukurasa huu, pamoja na sababu za kiufundi, hofu, mashaka na wasiwasi pia vilichangia mimi kutokuonekana. Hii ilitokana na makala niliyo andika wiki mbili zilizopita, iliyokuwa na kichwa “NIMEMUHUTUBIA RAIS KIKWETE” Makala nyingi nilizoandika watu walinitumia ujumbe kunipongeza na kutoa maoni yao, wengine waliniponda, haya ni ya kawaida.
Makala ya wiki ile hakuna aliyenipongeza wala kuniponda, waliosoma na kunitmuia ujumbe wote walinipa ujumbe wa masikitiko, wengi walinitahadharisha kwamba ninakoelekea ni kufungwa au kuuwawa. Mmoja alifika mbali na kusema tuombe wiki ipite salama bila kufanywa chochote.
Yuko mwananchi mwingine yeye alinitahadharisha kuwa naweza kufanyiwa hujuma na kusababisha nikakosa masomo, kwamba makachero wa serikali watafanya kila wawezalo ili kuniharibia masomo, kisa! Eti nimemwandikia rais.
Nimeirudia ile makala tena na tena kujaribu kuona lugha ya dharau ua matusi niliyomwandikia mheshimiwa rais sikuiona, nimetafuta maneno makali yaliyowafanya wasomaji wangu wanionee huruma. Mwandishi mmoja wa habari wa siku nyingi nchini aliniambia baada ya kusoma makala ile alisema, nina umri mdogo sana kiasi cha kushindana na rais, sijui alipata wapi taarifa kwamba nashindana na rais. Anasema hivi huku nikiwa sioni wapi niliposhindana na rais katika makala ile.
Kwa ufupi vitisho vile vilidhoofisha hali yangu ya kuandika makala. Hata hivyo leo nataka nizungumzie kwa nini naandika makala. Wengi pengine hawajui akiwemo rais na serikali yake kama huwa anasoma makala zangu. Wakiwemo pia wananchi wa Tanzania.
Kuna dhana kwamba kila anayeandika makala ya kuikosoa au kupinga maamuzi mabovu na ya kidhalimu ya serikali basi ni mpinzani, wengine hufika mbali na kuniona kama mwanachama wa chama kimojawapo cha upinzani nchini. Wapinzani nao kuna kipindi walidhani mimi ni CCM baada ya kutoa makala yangu ya januari 22 mwaka huu.
Niliandika makala ile kuwataka viongozi wa vyama vya upinzani kuacha kuwa ving’ang’anizi badala yake wawachie damu changa vyama, maana baadhi ya viongozi hao waliopo sasa, kuna kila dalili ya wao kushindwa kuviongoza vyama hivyo na hivyo kuvipeleka vyama hivyo mrama.
Huwezi amini, nashukuru kuwa makala ile imefanya kazi, juzi Mbatia anatangaza kuwa yeye hakuzaliwa kuwa mwenyekiti wa NCCR-MAGEUZI, kwamba yuko tayari kuwaachia watu wengine kuongoza. Katika makala ile niliwataja watu kama Ibrahim Lipumba, Seif Sharif Hamad na Agustine Mrema.
Ndugu zangu watanzania, napenda ifahamike kuwa mimi nimewahi kuwa CCM, nab ado niko CCM kinadharia tu, maana sijarudisha kadi, nilizaliwa CCM, babu yangu alikuwa Mbunge wa Mbeya mjini kwa CCM, na siku za mwisho za uhai wake aliwahi kuniambia kuwa angefurahi kama ningekuwa mrithi wake kisiasa katika kizazi chake. Huyu ni Mzee Benson Obed Mwamfupe.
Hata kama ningekuwa mwanachama hai wa CCM bado si haki kukaa kimya pale inapoboronga na kuwatendea ndivyo sivyo watanzania. Maana hii nchi si mali yetu wana CCM, ni mali ya Watanzania, na nirudie kusema kwamba, sio ajabu siku moja wembe ule uliowanyoa KANU kule Kenya utakuja kutunyoa wana CCM.
Siandiki makala kuchekesha watu, siandiki kuwafurahisha wapinzani wala CCM. Dhamira yangu itanisuta nikifanya hivyo, nafsi itanishitaki. Naandika makala kuwahabnarisha watanzania na kuwaelimisha pia. Rejea makala yangu ya rushwa ambayo nililenga kuwaelimisha watanzania kuhusu mapambano ya rushwa, kama ni kutetea niliitea CCM katika makala ile. Ilikuwa na kichwa cha “Mapambano ya rushwa na unafiki wa watanzanzania” Kamwe siangalii upande mmoja, sikuzaliwa kumsema Kikwete wala kumkosoa, kwanza sikujua kama Kikwete angekuja kuwa rais wan chi hii, na wala Kikwete hakuzaliwa ili awe rais wan chi hii, lakini maadam ameingia Ikulu hawezi kukwepa vitu ambavyo mtu wa kawaida anaweza kuvikwepa.
Ngoja nikwambie tena kwa nini naandika makala. Kama wewe ni msomaji wa safu hii utakumbuka kuwa niliwahi kuwaambia watanzania kuwa sio lazima wote tuwe wanasia ndipo tulete maendeleo nchini, kama ingekuwa hivyo basi ilitupasa wote tuwe marais wan chi hii, wabunge wa majimbo yetu au madiwani wa kata zetu. Ingekuwa vurugu, pasingekalika.
Kukawa na rais mmoja, huyu tumempa dhamana ya kutuongoza na kutufikisha kule tunakotaka. Lazima ifahamike kwamba kapewa tu dhamana! Pamoja na kwamba tayari anatembelea magari ambayo ni ukweli usiopingika kwamba kuna watanzania watakaokufa sio tu bila kuyapanda, pengine bila hata kuyaona. Anavaa mavazi ambayo yako tofauti na watanzania wengi vijijini, anakwenda nchi ambazo kuna watanzania wamenyimwa kwenda na tofauti nyingi alizo nazo na watanzania wengine bado lazima tukubaliane kwamba hii nchi Kikwete haiwezi peke yake, si Kikwete tu, bali rais yeyote atakayekuja, hata angekuja kuwa rais baba yangu mzazi, ukweli huu alipaswa kuufahamu.
Rais ni mwanadamu, hili wengi tunalisahau mara nyingine. Rais kuna siku atakaufa kama nitakavyokufa mimi Daniel na kuzikwa kama walivyozikwa wengi duniani. Mazishi ya kupigiwa mizinga na mbwembwe zingine hazitamfanya arudi duniani, wakati wake utakuwa umekwisha, sababu ni moja, yeye ni mwanadamu kama mimi na wewe.
Ubinadamu huo ndio unaomfanya ahitaji msaada wa wengine kumsaidia katika kutekeleza majukumu yake. Ndio maana akahitaji makamu wa rais, akahitji kinja mkuu wa mawaziri wake, akahitaji wakuu wa wilaya na mikoa. Hii inadhirisha kwamba yeye peke yake hawezi.
Ni vizuri pia kufahamu kwamba hata hao wasaidizi wake wanahitaji wasaidizi, ndio maana kuna waandishi wa habari ambao watawapa taarifa zitakazowafanya watekeleze majukumu yao kiufanisi. Pengine wawe na kiburi cha kujifanya wanaweza kila jambo, kuwaona waandishi kama wachochezi na wambea. Tabia hii inafanya nchi hii kubaki nyuma daima. Taarifa za kuvitisha vyombo vya habari kwa sababu tu wao ndio walioshika dola haitaijenga kamwe nchi hii. Ndio maana naomba sana, vyombo vya habari vitangazwe rasmi kuwa mhimili wa nne wa serikali.
Ukweli kwamba Kikwete hawezi nchi hii peke yake ndio inayonifanya niandike makala, siandiki kumdhalilisha, naandika kumsaidia, hata kama kumkosoa, kwani ni uhalifu kumkosoa mtu, je ni dhambi kukosolewa? Kwa lugha ingine, kukosoa kuna maana ya kurekebisha na kuonyesha njia sahihi. Wanaokosoa sio lazima wawe wanasiasa, naweza nikawa mwananchi wa kawaida kama mimi, ili mradi tu ninajua kile ninachofanya.
Kuwa rais au waziri hakumaanishi kwamba tayari unajua kila kitu, una wezo wa kila jambo duniani, ndio maana kuna haja ya kuwaweaka washauri. Naamini kuna watanzania ambao hawatakaa waje kuwa marai wa nchi hii, lakini wenye mawazo ya kujenga nchi, ikiwa tu wanaoshauriwa wasiwe na wivu, kwamba kufanyia kazi ushauri wa wengine ni kuonyesha udhaifu. Huu ni upotofu.
Nilipozungumza na katibu mkuu wa NCCR-MAGEUZI aliniambia kuwa Mwenyekiti wa chama hicho bwana James Mbatia ndie aliyetoa wazo la kuanzishwa kwa mfuko wa elimu Tanzania, na mfuko huo ukaanzishwa na serikali. Kimeharibika nini kwa hao waliotekeleza wazo hilo? Je si maendeleo kwa taifa letu?
Ni muhimu kufahamu kwamba binafsi hatuandiki makala kwa sababu tunapenda sana kuandika, au tunanogewa kufanya hivyo, asikudanganye mtu, kuandika si kitu rahisi kama unavyoweza kudhani, ni ngumu sana, Mheshimiwa Mkapa atakuwa anaelewa vizuri jambo hili!
Kuandika kunakufanya wakati mwingine uishi maisha ya hofu, maana hujui nani ni nani, hujui nani anakuja kwa jema. Tunaogopa mpaka wageni nyumbani wakati mwingine. Maana zinakuja sura ambazo hujawahi kuziona, halafu unaulizwa, wewe ndie Daniel? kujibu uongo siwezi inabidi niseme mimi ndie! Kisha anasema samahani, ninashida na wewe, nataka tuongee pembeni! Naanza kupata wasiwasi, anasema nimetumwa na kaka nanihii anasema muazime shilingi 5000/= Aah! Mimi nilidhani tayari wametumwa kuja kuni…………
Jamani naandika makala kwa lengo la kuelimisha wananchi, kukosoa ni haki yangu kama mwananchi. Kwa nini niache nchi yangu iende mrama wakati uwezekano wa kuokoa jahazi? Nitawaambia nini watoto na wajukuu wangu watakaponiuliza sababu za sisi (kizazi hiki) kushindwa kuijenga nchi? Si bora mimi nitakuwa na la kujitetea kwamba niliandika gazetini, lakini walilalia masikio, walibeza makala zetu, walitutisha na kutaka tufunge midomo.
Naandika makala kuenzi wana harakati wa zamani wakina Martin Luther King Jr. Sio vizuri kwa watawala kudhani kila anayeandika kukikosoa ni wapinzani au wanasiasa. Badala ya kuwatishia waandishi wakae nao na kwarekebisha au kukanusha kilichoandikwa. Hata kama itatokea watawahujumu waandishi kwa siri na umma usijue, ipo siku gharana hiyo italipwa, kuna siku watazaliwa upya wale waliouwawa.
Nguvu ya kalamu ni kubwa kuliko mitutu ya bunduki, kuliko sumu kali kama ya pakanga. Kalamu huchukiwa na wengi, nami naitumia kwa kadri Mungu anavyonipa fursa ya kufanya hivyo. Naandika makala hii si kwa lengo la kushindana, naandika kwa lengo la kuelimisha, kwamba wajibu wa kujenga nchi ni wetu wote, na sio watawala peke yao. Sio kina Lipumba, Mrema, Mbowe, Sharif, Duni, Mtikila, Makamba, Kikwete peke yao.
Nchi hii inajengwa pia na mkulima wa karafuu na miogo kule Pemba, inajengwa na mkulima wa chai kule Amani- Tanga na Rungwe Mbeya, inajengwa na mkulima wa korosho kule Mtwara na waandishi kama mimi hapa. Nipewe nafasi tu hasa ile ya kukosoa kila inapobidi na kupongeza kila inapostahili.
Kwa nini? Ukiwa kiongozi ni vigumu kuona madudu unayofanya, hii inatokana na ukweli kwamba madaraka yanalevya, yanapofusha macho, huoni, unahitaji wenzako walioko nje wakupe japo ushauri kuwa pengine unaelekea shimoni, uwe mwepese kusikiliza na kukubali kuutafiti ukweli wa mambo. Usifanye tu vile akili inakutuma, akili ishirikiane na macho, macho tunaweza tukawa ni sisi tunaondika makala japo hatuna taaluma hiyo, lakini tuna maoni na ushauri unaoweza kufaa.
Nafanya hivi si kwa ajili yangu tu, naangalia pia vizazi vijavyo, naangalia watoto wangu, nisipoijenga mimi wataathirika wao, hata kama sitafanikiwa mimi, nitawaambia nao wajenge kwa ajili ya wajukuu zangu (watoto wao) na siku moja itafika mambo yatabadilika.
Naandika, kwa sababu naogopa nisije nikakosa cha kujibu watakaponiuliza siku moja, nawaza watauliza hivi “baba nani aliiharibu nchi hyetu” Kama ni wewe unaulizwa, utamtupia nani lawama? Utasema ni Mkapa alitumia vibaya pesa zetu kwa kununua ndege na rada (si ndivyo tunavyomlaumu mzee wa watu) au nitasema ni Kikwete? Kwa kusema watendaji wake walitumia vibaya pesa za walipa kodi? Au ni Mwinyi aliyeiuza Loliondo, kwamba kama aliweza kuuuza Loliondo basi hakushindwa kuuza migodi na mashirika?
Watauliza ninyi mlikuwa wapi? Je, nitasema sikuwa kiongozi? Aah wapi! Bora nije niwaambie kuwa niliandika sana kwenye gazeti la Fahamu, na kwenye blogu yangu uzuri wenyewe wataiona, maana blogu inatunza kumbukumbu zote, naamini watanisamehe na kunitakia safari njema ya kurudi nyumbani, Mbinguni. Wewe utawajibu nini wanao na wajukuu zako? Kwa jinsi tulivyozoea kujitetea kwa uongo, si ajabu utawaongopea watoto wako!
Lakini kwa nini usiwaambie tu ukweli kwamba ulipokuwa askari wa usalama barabarani ulishiriki rushwa, ulipokuwa usalama wa raia ulibambikizia watu makosa kusudi wakuhonge? Kwa nini usiwaambie tu ukweli kwamba ulipokuwa ofisini ulikuwa unafanya kazi kwa masaa mawili, kupiga soga (tena za umbea) masaa sita na kuzurura masaa yaliyo baki. Kwa nini usiwaambie tu kwamba serikali ilipopiga marufuku taka zisitupwe hovyo mitaani wewe ulikaidi?
Mbona usiwaambie kwamba ulipokuwa nesi au daktari ulisababisha vifo vingi vya watu ambao wangejenga nchi hii baadae? Je utawaambia ukweli kwamba ulishiriki kuuwa raia wasio na hatia kwa sababu tu waliandamana kudai haki zao? Je utathubutu kuwaambia ukweli kuwa ushindi wa chama chenu ulikuwa si wa halali, kwamba mulikiibia kura chama kingine? Je utasema hayo?
Utawaambia kwamba muliiba mafuta kwenye magari ya Wizara na au shirika na kwenda kuyauza kwa sababu ya ubinafsi ulionao, kwamba hukujua kuiba kwako kumeleta madhara mpaka kwa watoto wako hao?
Utawaambia nini watoto wako? Usipowaambia ukweli kuna hatari kwamba nao watakuwa wezi na wahujumu kama wewe. Ninachotaka nikwambie hapa ni kwamba kila mtanzania kuanzia viongozi wa serikali mpaka raia wa kawaida wameshiriki kwa njia moja au ingine kuharibu kwa kuihujumu nchini hii hasa wanasiasa na matapeli wachahe kwenye idara za serikali.
Mwenzako naandika leo, kukusadia wewe na mimi, labda ushupaze shingo. Naongea na wewe Elizabeth David, una wajibu wa kuijenga nchi hii! Nisipo fanya hivyo nitakuwa sina cha kujitetea kwa watoto wangu na vizazi vijavyo. Wewe nawe cheza katika nafasi yako, acha kuhujumu nchi hii, sio mali yako peke yako, uwe na haya, uone aibu! Naongea na wasomi na wasio wasomi, naongea na Rais mpaka raia wa kawaida.
Mungu ibariki Tanzania, bariki vizazi vijavyo!
0713 550 778
ilovejesustz@yahoo.com