Monday, June 11, 2007


Huwezi amini kuwa hii ni Sinza, hawa ni watoto niliwafunmania asubuhi na mapema wakicheza kwenye uchafu uliolundikwa njiani na watu wenye akili timamu, si hivyo tu, lakini wanachezea pia maji machafu. Watu wanaodhaniwa kuwa ni wazazi wao walikuwepo nikipiga picha!

WAKAZI WA SINZA WANASEMA WAO SI DAWASCO WALA SERIKALI, NI KAMA VILE WANA 'ENJOY' SANA KUISHI NA UCHAFU


Huu ni mtaa anaoishi Mwenyekiti wa Serikali za mitaa Sinza, nyumba iliyojaa nyasi hapo kushoto ni nyumba ya kidosi mmoja, na kulia ni nyumba ya kidosi mwingine, wanatoka na magari yao na kuacha midimbwi hiyo kila siku kana kwamba hawaoni, Ili mradi wana masofa ya kutoka Ulaya ndani na vitu vingine vya thamani yakiwemo magari haoni haja ya kuweka mtaa safi!
Niliwahi kumfuata Mwenyekiti na kumuuliza kulikoni, akasema yeye hana la kufanya, eti hana la kufanya kiongozi, mbona kama ni viongozi Tanzania tumepata!


Friday, June 8, 2007

USIOGOPE!


Ni mchana huu wa leo, tunajiandaa na mitihani ya kumaliza mwaka na wakati huo huo kampeni za kuwania urais hapa chuoni kwetu zimeanza, kwa hiyo pia tumetoka kuwasikiliza wagombea, hawana tofauti sana na wanasiasa wa vyama vya siasa. Maneno meeengi. Tunasubiri utekelezaji, ndipo tutakapoweza kuhukumu ikiwa walitaka umaarufu au kututumikia wanafunzi!
Ni hatari sana kama wanataka kujifunzia siasa hapa chuoni, ni sawa ikiwa tui watakuwa hawajifunzi kudanganya kama walivyowaongo wanasiasa wengi Tanzania (na duniani?? au?)
Nyota njema huonekana asubuhi, msemo huu haujachuja maana yake bado, bado unafanya kazi. Chuoni ni mahali pa kujifunza uadili na ubadhirifu ukitaka. Kinachonisikitisha ni kwamba hata wasomi nao huwa bado hawana macho ya kung'amua waongo wanaodanganya mchana kweupee! Hivi mtu na akili zako unachagua kiongozi chuoni eti kwa sababu kakuahidi atahakikisha tunapata mikopo bila kutueleza njia atakazozitumia.
Atatupatiaje na kwa njia zipi? Mashaka zaidi tunayapata kwa sababu mtoa ahadi hizo hachukui mkpo, analipiwa na wazazi aua anajilipia mwenyewe. Huo ni mtihani mdogo sana wa wasomi kuwapima wanaotaka uongozi. Ndio maana wale wale wanaisasa wakija na sera zao kuwa watatujaza mapesa tunashangilia kana kwamba ana ghala za pesa sehemu fulani. oooh! samahani, naomba niishie hapa kwa leo! Nawahi kujiandaa na mitihani!


Nazungumzia hapa Chuo Kikuu cha Tumaini-Dar es salaam. Huyu anaitwa Anisa Juma, baada ya kujisomea, sasa ni mapumziko ikiwa ni pamoja na kupiga picha.

Wednesday, June 6, 2007

MAMBO YA TUMAINI UNIVERSITY

Hapa nipo na rafiki zangu wa chuo kikuu cha Tumaini tawi la Dar es salaam, kutoka kushoto ni Lusohoka Zakeyo, Anisa Juma, mimi mwenyewe, Balikudembe Joseph, Zamaradi, Neema Mrema na aliyeinama ni caroline Candus, hapa tulikuwa chuo cha Tumaini Iringa.

Saturday, June 2, 2007

MASUALA YA HABARI TANZANIA!

Hamjambooo? Salamu zenu wana Blogu, wana harakati wote! Hujambo Elizabeth David, nakuheshimu sana!

Niko kwenye chumba fulani cha habari, lakini sikuambi ni wapi, sababu soma chini hapa!





Hapa nipo katika studio za redio ya chuo kikuu cha Tumaini tawi la Iringa, hapa ninahojiwa na mtangazaji Janet.... kuhusu uhuru wa vyombo vya habari nchini. Nilimwambia kuwa siamini kama kuna uhuru wa vyombo vya habari nchini unaotakiwa. Nitakupa sababu siku moja!






Thursday, May 31, 2007

JE CCM, NI MASHETANI?


Mwasisi wa TANU na CCM, hayati Julius Kambarage Nyerere, akiwa na mkewe huko mahali fulani hivi!
JE CCM NI MASHETANI?

Nimekutana na mheshimiwa Fulani hivi karibuni, huyu nilipata fursa ya kujadili naye mambo yanayoihusu nchi hii na hasa siasa. Kumbuka niliwahi kukuambia kuwa napenda sana kila ninapopata fursa ninaijadili nchi hii.

Simuiti mheshimiwa kwa kumdhihaki, kwangu huyu ni mheshimiwa hasa, kwa sababu namheshimu kwelikweli, namheshimu kwa mambo mengi, ikiwa ni pamoja na mchango wake kwangu, kufikia hatua hii ya uandishi (sio uhandisi) wa makala gazetini na kwenye blogu.

Katika kujadili naye, bila kutarajia tukajikuta tayari tunazungumzia juu ya mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini. Na kwa kufupisha mada hii, nikuambie tu kitu ambacho huyu mheshimiwa alikisema. Yeye anasema na kuamini kua mfumo wa vyama vingi vya siasa ni ushetani, yaani asili yake ni uasi alio ufanya shetani kwa Mungu. Kwamba upinzani ni roho ya ushetani inayofuatilia na kufanya kazi katika mfumo huo. Wewe msomaji unasemaje?

Mwenzako huyu alianza mbali, anasema eti shetani kabla hajawa shetani alikua chini ya utawala wa Mungu. Kwamba alipotaka kuwa juu ya Mungu au kwamba hakufurahia kuwa chini ya utawala wa Mungu, akaamua kuanzisha kampeni za kumpindua Mungu. Hapo ndipo alipolaaniwa na kutupwa chini (duniani) ambako laana ile bado inaambukizwa kwa wengine wakiwemo wanasiasa.

Kwamba CCM ndio wamekua watawala wa nchi hii, na viongozi wa vyama vya upinzani hasa wale waasisi wanaendeleza mfumo wa kishetani, hii ndio kusema kwamba waasisi kama vile Mabere Nyaucho Marando wa NCCR-MAGEUZI, Abdallah Fundikira wa CUF na wengine wengi unaowajua ni walaaniwa. Pengine Fundikira anehesabika kama ‘mtakatifu’ maana ametubu dhambi yake ya uasi na kurudi nyumbani kwa watawala, yaani CCM. Lakini dhambi hiyo ya Fundikira na wengine wapotevu wameitubia wapi? Maana CCm si miungu wale, maana nao bila shaka wana mengi ya kutubu. Hebu tuachane na hayo badala yake turudi kwenye mada na tuchimbe kwa ufupi historia.

Ni muhimu kukumbuka kuwa, tunapoizungumzia CCM, tunazungumzia mtoto aliyezaliwa mnamo mwaka 1977. Alizaliwa na wazazi wawili waitwao Afro Shiraz Party (ASP) na Tanganyika African Union (TANU) Sijui nani kati ya wazazi hawa alikua mama na mwingine alikua baba, maana majina yao hayaonyeshi jinsia!

Huyu mtoto yaani CCM, alizaliwa na wazazi ambao kila mmoja ana asili yake. TANU kwao ni Bara na ASP kwao ni kuleeee visiwani. ASP akiwa kwao alikua chini ya mtawala mwarabu, ukipenda mwite Sultani. ASP akakua, baadae akaona mwarabu anafaidi sana akitawala visiwa vya Pemba na Unguja (Zanzibar) akaanza mapambano ya kumng’oa mtawala wake. Sijui ni kwa sababu ya uzee, Sultani akashindwa mapambano.

Haya tuendelee, TANU naye kwao walikua chini ya mtawala Mwingereza, naye roho ikaota kutu, wakajisikia vibaya kuona Mwingereza anakula nchi, wakaona anafaiiiiiiidiii kukalia Tanganyika, aeti wakaanza kudai kujitawala wenyewe! Wakafunga safari mpaka Umoja wa Mataifa – New York kuwashitaki Waingereza (watawala wao)

Sasa niambie hawa wazazi wa CCM tunawapa jina gain kwa mujibu wa yule mheshimiwa? Bila shaka ni waasi, wameasi watwala wao, ni kama vile shetani alivyotaka kumpindua anayestahili kile kiti cha Enzi, YEHOVA Mungu Mkuu! Kwa kusema hivyo basi ni walaaniwa? (nauliza) Kwa yeyote anayeamini kama yule mheshimiwa anavyoamini hawezi kujizuia kuamini kuwa TANU na ASP walifuatiliwa na ile laana ya Ibilisi. Na kwa sababu walikuwa wapinzani wa watwala wao, serikali zilizokuwapo madarakani kwa wakati huo, basi hawawezi kukwepa kuitwa mashetani.

Kwa bahati mbaya au nzuri sana, wale wazee, yaani ASP na TANU hawapo tena, lakini hawakuwa wagumba, walibahatika kuacha mtoto mmoja wakamwita CCM. Na kwa kua mtoto wa nyoka ni nyoka tutaepukaje kuamini kuwa mtoto wa shetani ni shetani, tutachekwa tukisema mtoto wa shetani ni kuku au samaki kwa kutaka kulazimisha watu kuamini yale tunayoamini sisi hata kama kwao ni sumu. Kwa hiyo hoja yangu hapa ni kwamba kama kuna watu wachache, kwa maslahi yao binafsi wnataka kupotosha umma kuwa upinzani ni ushetani hawajui kuwa anatushawishi sisi wengine na kutufumbua macho, na kutufichulia siri iliyofichika kwamba CCM ni ushetani uliokubuhu, ushetani uliokomaa, maana ni tangu wazazi wake TANU na ASP, ndiyo! Si waliwapinga watawala wao, waliwapindua! Pengine CCM bara watakua na la kujitetea, hivi kule visiwani CCM inaweza ikasimama kama mkereketwa huyu mmoja anavyoweza kusimama kuwa upinzani ni ushetani? Eti kwa sababu tu wanakipinga chama tawala? Je wanaweza kuepuka kuitwa mashetani baada ya wao kumpindua mtawala wao Sultani?

Mimi sitaki kuamini hivyo, lakini huwezi kunizuia kuamini kuwa, ikiwa vyama vya upinzani ni ushetani basi asili yake ni CCM.

Nitumie fursa hii kuwaomba baadhi ya wanachama, wapenzi, viongozi na wakereketwa wa chama cha mapinduzi, ambao hawafurahii uwepo wa vyama vya upinzani bila kujua umuhimu wake, kwamba wasijaribu kuupotosha umma kwa namna yoyote iwayo. Wapambane kwa hoja na si kuwatisha wananchi. Pengine yule aliyeibua mjadala huu hana cheo chochote ndani ya chama hicho, kiasi cha kwamba anaweza akasambaza upotofu huo. Lakini si ajabu kesho huyu jamaa atapewa uongozi wa ngazi yoyote katika chama hicho, na huku bado akiwa na chuki na vyama hivi, bila shaka utakuwa wakati muafaka wa yeye kutisha wananchi.

Nimeona niiseme mapema maana si ajabu, kuna watu wanauchukulia upinzani kama utapeli, wizi na propaganda, kama Shahibu Akwilombe, naibu katibu mkuu wa CHADEMA alivyosema mjini Tanga hivi karibuni.

Ninawaomba wanasiasa watumie majukwaa yao vizuri na hasa CCM. Hatuwezi kamwe kubeza ukweli kwamba kunaweza tokea siku ambayo CCM itaitwa chama cha upinzani. Kwa kuhofia hilo, tusitumie mbinu chafu kuwazuia raia kuwa wanachama wa vyama wanavyovipenda. Kwamba kuwatisha kuwa upinzani ni ushetani ni dhambi, kuwaambia vyama vya upinzani vina matatizo si haki, maana hakuna chama kisicho na matatizo, nasema hakunaaa!!

Nashauri kwamba kusitumike mbinu chafu kudhoofisha upinzani nchini, mchango wake ni mkubwa kwa maendeleo ya nchi hii, hata kama hawatakuwa watawala wan chi hii. Wacha kuwepo na ushindani wa halali, tabia ya kuwarubuni na kuwanunua viongozi na wanachama wa vyama vingine ni dalili tosha za kuisha kwa enzi za chama husika. Kama kweli kuna pesa zinatumika kuwahonga na kuwanunua wapinzani, bai hakuna tena demokrasia ya kweli katika nchi hii, na tu wadhambi hata mbele za Mungu na wadanganyifu kwa jamii ya kimataifa.

Najua ukweli huu si kila mwanasiasa ataufurahia, lakini kwa kweli hatuna jinsi, ni lazima tuukubali. Nasema hivi kama wana CCM wanaitakia mema nchi hii hawana budi kuacha mtindo wa kuwarubuni na kuwatolea mijicho wapinzani na kuwashawsihi kurudi huko. Tabia hii haitaigharimu CCM kwa upande wa maslahi, itatugharimu watanzania hasa wa nyonge.

Kwa nini? CCM ikae ikijua kuwa itakapokuwa madarakani kama chama pekee cha siasa nchini, ni wazi kwamba italewa, itajaa kiburi na kuzalisha udikteta ambao ndio ule nasema utatugharimu watanzania. Nani atakua na ujasiri wa kuizodoa CCM ndani ya CCM, leo tunao wakina Mtikila, Mbowe, Mbatia na wengine wengi kwa sababu wako nje ya CCM. Huko wangeambiwa wangoje vikao, vikao saa ngapi wakati nchi inaharibika? Vikao vipi wakati wanyonge wanazidi kudidimizwa?

Ujasiri wa kina Mbowe na wenzake unatokana na kwamba hakuna kamati yoyote ya CCM itakayomwita kumhoji kama mwanachama wake, aliyesemea mambo ya chama nje ya chama. Ndio hapa tunauona umuhimu wa vyama vingi nchini, na hili ndilo somo wanalopaswa kulijua watanzania walioanza kulishwa kasumba kwamba upinzania ni ushetani!

Najaribu kuwaza, kama kweli James Mbatia ndiye alitoa wazo la kuanzisha mfuko wa elimu nchini na ukaanzishwa, je ingekuaje kama asingekuwa mpinzani? Je angesikilizwa ndani ya CCM? Hilo ni swali, jibu lake sote tushirikiane kulitafuta kama tunadhani litatusaidia.

Pia nawaza (pengine kipuuzi) kwamba kama upinzani usingekuwepo nchini, hii nchi ingekuwaje kiuchumi na kisiasa? Jaribu kufikiri haya mambo, usiyachukulie kirahisi. Fikiria tu siasa za Tanzania zilivyo sasa, hasa kwa upande wa demokrasia, angalia hali ya uchumi wa nchi hii, fikiria wapinzania wasingekuwa wanafanya vitu ambavyo Makamba anaviita kelele za mlango au za chura, fikiria tu, pembua katika mawazo, usimjibu mtu, jijibu mwenyewe, kwa mtazamo wako, ijibu nafsi yako, uwe shahidi wa wewe mwenyewe, jiambie ukweli, hii nchi ingekuwaje?

Maneno ya kejeli kama ya Makamba na wana CCM wengine ukitafakari sana utakuta ni hofu tu iliyojengeka. We angalia watu wanapopigana kwa kutumia mikono (ngumi) mmoja anapozidiwa utakuta si ajabu akaamua kutumia silaha kinyume cha utaratibu kwa lengo tu la kujihami na kumshinda mpinzani wake. Hatutaki wana CCM wafike huko, na wapambane kihalali kabisa na wapinzani wao kisiasa. Kudai kuwa CCM ni ushetani hayo ni matumizi ya silaha haramu kwa kujihami. Haikubaliki hata kidogo!

Hebu fikiria! Je ni ushetani kwa mtu kudai haki yake na ya mwingine? Ni ushetani kuandamana kupinga maamuzi yasiyofaa ya serikali? Ni ushetani kudai marekebisho ya katiba inayojichanganya? Katiba inayozungumzia nchi ya ujamaa na hali ujamaa haupo? Au bado kuna ujamaa hii nchi?

Kuna madai kuwa mara kadhaa CCM imeiba kura (haya ni madai ya wapinzani) CCM wamekuwa wakikanusha tuhuma hizo, lakini fikiria kuwa kweli wameiba lakini ni kwa vile tu mwanadamu hawezi kukiri kosa kirahisi wanakataa, sasa kama kweli waliiba, je huo si ushetani?

Hebu nisiwe kasuku hapa, tuonane wiki ijayo kwa neema ya Mungu!


Wednesday, May 30, 2007

HIMA WATANZANIA, AMKENI KUMEKUCHA!


Hapa Rais Kikwete akiomba kura kwa Watanzania!





Hawa si unawajua? - >
Kuna msemo wa wazungu unasema ‘information is power’ Kwa Kiswahili rahisi kabisa tungeweza kutafsiri msomo huo kama, taarifa ni nguvu. Mtu mwenye taarifa nyingi au kidogo hawezi kufanana kamwe na yule ambaye hana taarifa na wala hapendi kusoma kwa lengo la
kujihabarisha.
Nimebahatika kusoma baadhi ya magazeti, napenda sana kusoma magazeti, na sio kwa lengo la kujipa burudani bali kujihabarisha ili kupata taarifa.

Pengine kwa mara ya kwanza kwa upande wangu wiki iliyopita nilisoma magazeti mawili tofauti yenye makala zinazofanana kana kwamba waandishi wake walipanga kuandika ujumbe unaofanana.

Magazeti hayo ni Mwananchi na Tanzania Daima, kwenye Tanzania Daima nilikuta tahariri moja na makala tisa za waandishi tofauti. Pamoja na utofauti huo wa waandishi wake na vichwa vya makala zote hizo, ukisoma kwa makini utagundua kuwa zote zina ujumbwe mmoja! Hii ni kwa mtazamo wangu.

Jaribu kupitia magazeti hayo ambayo ni Tanzania Daima toleo namba 908, Mei 30, 2007 na Mwananchi namba 02543 la siku hiyo hiyo, pengine utagundua kitu nilichogundua mimi. Katika kupembua makala hizo, mwenzenu nimegundua kuwa ujumbe wa makala zote nimeupa jina la UKOMBOZI WA MTANZANIA!

Sio siri makala hizo zimenitia moyo sana, kupitia makala hizo nimejifunza kwamba kuna mambo mawili au matatu yanatokea kwa pamoja hapa nchi sasa hivi!

Mosi; watanzania tumeanza au tayari tumegundua jinsi hali ya hewa ya nchi hii inavyokwenda, tumeanza kuelewa nini kinafanyika nyuma ya pazia la Taifa letu, na hasa katika suala zima la siasa na utawala. Inatia moyo kwamba yale ambayo tulidhani kuwa hayapo, yapo. Na yale ambayo wahusika walidhani kuwa watanzania hawayajui na hata kuhakikisha kuwa wanayaficha yanakuwa siri, ukweli ni kwamba hakuna siri tena. Nasema watanzania wamenaza kung’amua mambo.

Je unataka kuamini kuwa sasa tunaanza kuujua ukweli, msome Absalomu Kibanda katika makala yake ya wiki iliyopita, anasema hivi
“…Leo hii najiona mwenye bahati kulitambua hilo na kufahamu namna majemadari hawa wa CCM walivyo tayari kucheza rafu za kila aina kuwanyonga wapinzani wao wa kisiasa…..”

Huyu ni mhariri wa gazeti la Tanzania Daima, hapa najiuliza swali, je ni wahariri wangapi leo wanaweza kusimama kwa uajsiri kusema aliyoyasema Kibanda katika makala yake ile? (tafadhali kaipitie) Je ni wahariri wangapi wamegundua yale aliyoyagundua Kibanda?

Msome pia Elias Msuya aliyeandika kwenye gazeti la Mwananchi ukurasa wa 12 siku hiyo, yeye anasema

“Na kwakuwa watawala wanaujua udhaifu wetu, basi wanaamua kuwekeza kwenye biashara hii. Chama tawala sasa kimekuwa maficho ya matajiri na mafisadi. Walio walafi wanajitolea kufadhali chama ili walindwe, hawa wanaangalia maslahi yao kulik yale ya nchi”

Unaweza kuona kuwa. Elias naye amegundua ukweli wa mambo ulivyo katika chama tawala, chama kilichpewa dhamana ya kuliongoza Taifa hili. Hakuishia hapa, Elias pia amegundua kwa upande mwingine kuwa Watanzania na sisi tuna tatizo, huu ni ugunduzi na utambuzi mzuri sana, anasema

“….Je ni kweli hali ya maisha yetu zinaboreka hata tushawishike kukipa ushindi wa kishindo chama tawala kila tunapoingia kwenye uchaguzi? Je wapiga kura wetu wanaelewa wakifanyacho? Au kwa kapelo na fulana zinatosha kuwazubaisha kwamba kweli dhamira ya chama tawala ni maisha bora kwa kila Mtanzania. Je hivi Watanzania ni mambumbu wa kiasi gain? Je ni kwa nini waendelee kuruhusu wanaisasa wachezee akili, hisia zao na maisha yao kila mara?”

Huyo ni Elias Msuya. Nimewahi kusema mara nyingi, nab ado nasisitiza kuwa kwa sehemu watanzania tunashiriki kulihujumu taifa hili, ikiwa ni pamoja na kuwapa kura viongozi wasiostahili, kwa kudanganywa na maji ya uhai ya shilingi miatano, doti za kanga, kofia na mafulana, haya ambayo baadae yanatugharimu kwa miaka mitano au kumi. Watanzani tuna kasumba ya kurudirudia makosa tuliyofanya awali. Hili ni tatizo la viongozi wetu pia, kwamwe baadhi yao hawajifunzi kutokana na makosa.

Katika mfululizo huo, kana kwamba waliambiana, Boniface Makene naye anagundua jambo, anasema;

“Chama hiki kwa sasa kina kundi kubwa la wanachama wasio kifahamu vema. Wengi wa hawa ni wafanya biashara na kundi jingine linasaka madaraka”

Makene anaongeza kusema;

“Kuingia kwa awamu ya nne kunaambatana na kuibadili CCM kuwa chama cha wafanya biashara na wawekezaji”

Bila shaka Makene anafahamu vema madhara ya chama cha siasa na hasa kile kilichopewa dhamana kuongoza nchi kuhodhiwa na wafanya biashara!`

Pili; baada ya watanzania kuanza kung’amua ukweli wa mambo, sasa inaonekana dhahiri kuwa wamechoka, nasema tena kuwa wamechoka! Wamechoka visa, dhuluma, ulafi na uroho wa wachache. Wamechoka kufanywa wajinga na watoto wadogo, siasa za maneno matupu yaisyojenga nchi, wamechoka kila aina ya vituko vya baadhi ya watawala na wanasiasa. Kauli zao zinathibitisha haya;

Angalia Kristofa Kidanka anavyosema hapa;

“Mengi yalitufanya tunyamaze, mojawapo ni kuwa rais Kikwete alisema Uingereza bado wanachunguza kwa kina suala hilo (rada) na kwamba tutadai ‘chenji’ yetu iliyozidi katika ununuzi ule……Tunataka maelezo kutoka kwa mzee Mkapa, na katika hili tunamuomba Rais Kikwete akae pembeni. Asimkingie kifua. Tunataka atueleze japo kifupi sana, kwa nini alitumia muda aliokuwa Ikulu kufanya biashara”

Hivi unapata somo hapa wewe? M.M.Mwanakijiji naye hakubaki nyuma, utadhani wameambiana na Kidanka, Mwanakijiji ansema;

“Kwa bahati nzuri (mbaya kwa serikali) nyakati za kunyamazisha watu kuhoji matendo ya serikali zimepitwa na wakati wa wa wananchi kuona aibu kuwaambia viongozi wetu ukweli umekwisha. Tutawaambia hata kama hawapendi kuusikia na kwa hakika tutapaza sauti zetu zaidi ili hata waliotia pamba masikioni mwao na watusikie”

Watu kama M.M.Mwanakijiji ni picha halisi ya watanzania wengi wasio na sauti za kusema “TUMECHOKA”
Hivi unaweza ukathubutu kusema hawa watu walipanga kwa pamoja waandike ujumbe mmoja siku hiyo, tena kwenye magazeti tofauti? Kama sivyo, unapata picha au somo gain hapa? Ni rahisi, ni kwamba, watu wameanza kugundua ukweli, maana ukweli haufichiki, ukweli haufi, hata ungeamua kuuzamisha ndani ya bahari ya Hindi pale Dar es salaam, kuna siku utapata taarifa kuwa umetokea kwenye bahari hiyo hiyo ya Hindi kule Tanga au Mbombasa. Omba tu asiwepo anayependa ukweli akauona, maana kwa hakika ataufuata, kuuchukua na kuutumia.

Niliwahi kusema kuwa nchi hii inahitaji mapinduzi, nilisema mapinduzi haya hayahitaji mitutu ya bunduki wala mabomu, hayahitaji mizinga wala mapanga, hayahitaji lugha za matusi.

Ndugu zangu, nasema pengine tunahitaji kidogo sana nacho ni mapinduzi ya kifikra. Fikra zetu kubadilika, zisafishwe upya, ziyeyushwe, maana zimeganda. Wansiasa na hasa wale watawala wamechangia kugandisha fikra zetu. Kugundua tatizo ni hatua moja kubwa sana kwa ajili ya utatuzi wa tatizo hilo.

Ushauri mdogo ninaoweza kukupatia hapa jinsi ya kubadilisha na kusafisha fikra ni kupenda kujihabarisha juu ya masuala mbalimbali yanayolihusu Taifa lako. Anza kupenda kusoma magazeti yanayokujengea moyo wa uzalendo, kuwa mfuatilialiaji wan chi jinsi inavyokwenda. Nunua katiba ya nchi yako, humo utaelewa haki na wajibu uliona kwenye taifa hili.

Kupitia Katiba utajua nini cha kuhoji kuanzia kwa mjumbe wako wa nyumba kumi mpaka rais wako. Kwa mfano kifungu cha 18 (2) kinasema “Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii”

Soma kifungu hicho kisha linganisha na taarifa za vyombo vya habari kuhusu mikataba ambayo nchi hii inaingia na wawekezaji wa nje

Acha kusoma magazeti yanayonajisi fikra zako, huu si wakati wa anasa na burudani zilizokithiri, huu ni wakati wa kujenga nchi hii.

Acha kuharibu fikra yako kwa kutazama na kusikiliza vipindi vinavyokupumbaza na kusahau wajibu wako kwa Taifa hili. Sikatazi watu kutazama wakina Rebecca na Kamila, isipokuwa nakumbusha tu kuwa wale jamaa walishajenga nchi zao, hatufanani nao kabisa. Mtu mmoja akaniambia kuwa wenzetu wametupita miaka 400 mbele!

Wewe unayekwenda kwenye Internet, usilihujumu Tiafa lako kwa kuangalia na kusoma vitu vinavyo najisi fikra zako. Nchi inahitaji watu makini ikiwa ni pamoja na wale wanaopenda kujihabarisha, kwa sababu “information is Power”